Polisi kuingia mikataba ya utendaji kazi.



Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, amepokea ripoti ya tathmini ya namna ya Jeshi la Polisi linavyoweza kuboresha huduma katika jamii (PDB) kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kwa kuanza na mkoa wa kipolisi Kinondoni.
 
Katika utekelezaji wa mambo yaliyoanishwa katika ripoti hiyo ambayo imeandaliwa kwa miezi sita kwa kushirikisha wadau mbalimbali, watumishi wa jeshi la polisi kaunzia ngazi ya juu hadi chini wataingia mkataba.
 
Mkataba huo utaanza kuingiwa kati ya Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi na Mkuu wa Jeshi la Polisi ambaye naye ataingia mkataba na makamanda wa mikoa ya kipolisi nchini na wao kuingia mikataba na watendaji wa chini yao hadi ngazi ya mwisho.
 
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo jijini Dar es Salaam jana, Kitwanga alisema mpango huo utagusa ngazi zote na anatarajia utatekelezwa kikamilifu kwa yale waliyojipangia.
 
"Sitegemei kusikia askari ameshindwa kutekeleza wajibu wake kwa kigezo cha vikwazo, kama mkiweza kutekeleza vyema jukumu hili katika mkoa wa Kinondoni ni wazi kuwa utafanikiwa nchi nzima kwa sababu mkoa huu umekuwa na matukio mengi ya kihalifu," alisema.
 
Hata hivyo, hakusema mambo yaliyoanishwa katika ripoti hiyo ambayo yataingiwa mkataba,na inaelezwa kuwa wananchi wataelezwa namna utendaji kazi utakavyotekelezwa wakati wa uzinduzi wa mpango huo.
 
Pia aliagiza kupatiwa  ripoti ya utendaji kila siku ya Ijumaa ili aweze kuzifanyiakazi mwishoni mwa wiki.
 
“Tena mnikabidhi zile zenye alama nyekundu na njano zinazomaanisha kushindwa na zile za mafanikio zaa kijani mumpe Mangu mwenyewe,  sitarajii mshindwe kazi hii maana polisi mnatakiwa kupambana,” alisema.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu,  alisema jumla ya vituo 13 vya polisi vya vinavyohama (mobile stations) vitaanzishwa katika mkoa wa kipolisi Kinondoni na kufanya kazi kwa saa 24 ili kutekeleza jukumu la kudhibiti uhalifu na ulinzi wa raia na mali zao.
 
Alisema gharama za mradi huo zitaanishwa siku ya uzinduzi wa mradi huo na wananchi wataelezwa namna utendaji kazi utakavyotekelezwa.
 
Naye Mtendaji Mkuu wa BRN,  Omary Issa, alisema utafiti huo ulishirikisha jamii nzima katika kuandaa ripoti hiyo na kwamba waliamua kuanza na mkoa wa kipolisi Kinondoni kama mfano baada ya utafiti kuonyesha unakabiliwa na uhalifu mkubwa.
CHANZO: NIPASHE



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: