Mbali na kazi ambazo wamekuwa wakizifanya baada ya kuanza kutumikia adhabu ya kifungo hicho, pia watakuwa msaada katika kutoa ushauri kwa idara za hospitali hiyo kulingana na taaluma na uwezo wao ikiwamo kupanga bajeti.
Mramba na Yona kitaaluma ni wachumi na wamekuwa watumishi wa serikali kwa taaluma hiyo kwa miaka mingi.
Ofisa Mazingira wa Hospitali hiyo, Miriam Mongi, alisema jana kuwa usafi wa mazingira ni kazi ambayo imepewa kipaumbele zaidi kwa Mramba na Yona, lakini pia watakuwa wanapangiwa kufanya kazi katika idara zingine.
Nipashe jana lilishuhudia Mramba na Yona wakiwa wanafanya usafi katika sehemu ya nyuma ya jengo la wazazi, wakikata majani ya miti, kutengeneza maua na kufagia.
Miriam alisema tangu waanze kutumikia adhabu katika hospitali hiyo, wameonyesha juhudi katika kazi kwa kuhakikisha wanawahi na kufanya kazi wanazopangiwa kila siku.
Alisema utendaji wao wa kazi unaridhisha na wameonyesha moyo wa kujituma na wameikubali kazi yao, tofauti na walivyotarajia kwamba huenda ingekuwa ngumu kwao.
“Yaani hata tunavyozungumza nao na hata wanavyofanya kazi zao, wanaonekana wamezoea na wameikubali. Hawasumbui kabisa, wanafanya kazi kwa makini na vizuri na kila siku wakimaliza kazi yao inakaguliwa na kurekodiwa. Pia yupo mwendesha mashtaka ambaye hufika kila siku kuangalia kama wanatekeleza," alisema.
Aliongeza kuwa katika idara ya usafi hospitalini hapo, kuna upungufu wa wafanyakazi, lakini ujio wa Mramba na Yona umesaidia kuongeza nguvu, ikiwamo kumaliza kazi mapema.
Miriam alisema tangu waanze kutumikia adhabu hiyo tayari wamekwishafanya usafi wa aina mbalimbali ikiwamo kudeki katika majengo, kulima, kufyeka, kufagia na kuzoa taka.
Januari 5, mwaka huu, Yona na Mramba walihukumiwa adhabu hiyo ya kifungo cha nje na kupewa adhabu ya kufanya usafi katika maeneo ya jamii.
Kabla ya kubadilishiwa adhabu ya kifungo cha nje, walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka mwili kila mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11 kwa kutoa msamaha wa kodi.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment