Kaka yake Gavana maarufu achezea kichapo cha Polisi



KAKAKE Gavana wa Kiambu William Kabogo, Bw Joseph Kang’ethe anauguza majeraha anayodai yalisababishwa na polisi.
Bw Kang’ethe anauguza majeraha ya kukatwa usoni, kuvimba shavuni, goti lililoteguka na jeraha baya kwa uti wa mgongo.

Mwathiriwa ambaye aliongea na Taifa Leo muda mfupi baada ya kutibiwa katika zahanati ya Athi River, alieleza kuwa alikuwa akiendesha gari kwenye barabara ya Mombasa eneo la Mitchell Coats, alipoanza kuhangaishwa na magari mawili.
“Muda tu magari hayo yaliponikaribia, nilipunguza kasi lakini waliokuwa ndani waliniashiria kuwa niondoke kwa barabara, lakini nilipopinda gari upande wa kushoto ili kupatia gari hilo nafasi. Nilipitia njia ya chini ya kuelekea uwanja wa ndege, na nikiwa ninakaribia kituo cha reli cha Syokimau, Mercedes Benz ilikuwa ikisimamishwa mbele yangu na polisi wawili walitokea wakiwa kwa viti vya nyuma, na mmoja akiwa na bunduki aina ya AK47 na mwingine akiwa na redio ya polisi,” alieleza Bw Kang’ethe ambaye alikuwa akiendesha gari aina ya Mercedez Benz S Class.
Kisha anasema walimvuta kutoka kwa gari na kumzaba kofi kabla ya mwanamume aliyekuwa ameketi kwa gari nyuma kutoka na kuwaagiza waache kumchapa.
Aliongeza kuwa wanaume hao walionekana kuwa wamembeba mtu mashuhuri ambaye hakuweza kumtambua.
Bw Kang’ethe alisema baada ya hapo ndio waliamua kurudi kwa gari lao na kuondoka lakini aliamua kuwafuata kujua ni kina nani waliokuwa kwa magari hayo na sababu yao ya kuhangaisha wenye magari.
Kuwafuata
“Kwa hivyo, niliamua kuwafuata na nilipokaribia, nilimwambia rafiki yangu achukue picha za magari hayo, na inaonekana wanaume hao walituona.
“Tulipokaribia duka kubwa la Mulley Supermarket, Mercedes Benz hiyo ilikuja ikatuzuia kwa mbele na wanaume wanne walitoka wakiwa na bunduki za AK47 na mmoja alianza kutupiga kwa upande mmoja wa bunduki hizo huku wengine wakiweka ulinzi wakiwa na bastola zao,” alieleza Bw Kan’gethe.
Katika hali hiyo, alieleza umma uliingilia kati na watu hao waliingia kwa magari yao na kuondoka.
Bw Kang’ethe alipokea matibabu katika zahanati ya Athi River ambapo aliruhusiwa kuondoka kabla ya kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Athi River.
Hata hivyo, aliapa kuwa lazima atahakikisha watu hao wanachukuliwa hatua huku akiondoa hofu kuwa huenda kulikuwa na jambo lililochangia tukio hilo.
Polisi walikuwa hawajathibitisha kama walipokea ripoti za tukio hilo kufikia wakati wa kwenda mtamboni.

Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: