Kujitambua
ni ile hali ya mtu kuelewa kwamba yeye yupo kama yeye tofauti na mtu mwingine. Ni kuelewa kuwa wewe ni wa pekee, kutambua mambo yanayofanya wewe uwe wewe. Ni kutambua uwezo na udhaifu wako. Kutambua yale unayoyapenda na yale usiyoyapenda. Kuelewa mwitikio wako kwa kila kichocheo ndani na nje ya mwili wako. Kuelewa jinsi hisia na mihemuko inavyoathiri kwa wema au kwa ubaya, utendaji wa akili na maamuzi yako..Kujitambua kunamfanya mtu aelewe ametoka wapi, kwa nini yuko hapa duniani na kwa kusudi gani yuko hapo alipo. Kujitambua hutoa fursa ya mtu kutambua nguvu zake za ndani na vipaji alivyonavyo, husaidia mtu kujipenda, kujithamini na kujikubali jinsi alivyo na kumuwezesha kufanya mambo kadhaa ili kuboresha hali ya maisha kwa kufanya uchaguzi sahihi. Kujitambua ndiyo kazi inayostahiki kupewa kipaumbele cha kwanza katika utunzaji wa afya, uzuri na urembo wa msichana.
Msichana anayejitambua anatambua kuwa hayuko hapa duniani kwa bahati mbaya. Anatambua kuwa ameumbwa na Mungu na amekusudiwa kuwa kama alivyo kwa sura, umbo, viungo vya mwili wake na akili yake ili atimize wajibu na majukumu ambayo hakuna mwingine wa kuyatimiza isipokuwa yeye. Kila mtu amekuja duniani, ameletwa ili aache alama yake mwenyewe, atoe mchango wake kwa maendeleo na ustawi wa dunia na baadaye siku moja atoe hesabu yake mwenyewe jinsi alivyotumia vipaji vyake na muda aliopewa kuishi.
Watoto wa kike wanayo majukumu ya kijinsia ambayo kwa vyovyote vile ni majukumu ya kike na wanaume hawawezi kuyatekeleza hapa duniani, hayo ni majukumu ya wanawake kwa asili. Hii inafanya mtoto wa kike awe na umuhimu sawa sawa kabisa na mtoto wa kiume.
Msichana anayejitambua anaelewa kuwa yeye ni mtu wa namna gani, yuko katika kundi gani la kijamii, mila zake zinamtaka afanye nini na anauwezo wa kufikia kiwango gani cha maisha. Anajipenda na kuwapenda wengine, anatunza mwili, akili na moyo wake. Anatambua kuwa kila mtu amepewa na Mungu uzuri wake unaotofautiana na uzuri wa mwingine.
Anatambua changamoto, nafasi na fursa zilizoko mbele yake, anatambua vikwazo vinavyoweza kumkwamisha ili asifikiye malengo yake katika maisha. Anatambua jinsi ulimwengu unaomzunguka unavyokwenda, anajiamini, anatambua mambo yanayothaminiwa na yale ambayo ni ya kweli dhidi ya uongo, anafanya uchaguzi mzuri wa mambo, anatambua kuwa dunia imejaa mambo mazuri lakini pia inazo takataka zinazong’aa kama dhahabu kumbe ni sumu ya nyoka.
Msichana anayejitambua anafikiri kabla ya kutenda, natambua kuwa tunakuwa kama tulivyo kutokana na kujifunza. Tabia zetu zinaathiriwa kwa wema ama kwa ubaya na mafundisho ya wazazi, jamii, mazingira, dini pamoja na mambo tunayojizoeza kwa kusoma, kusikia au kuona katika maisha ya kila siku.
Kujitambua kwa msichana pia kunakamilishwa na kuelewa jinsi alivyoumbwa, jinsi mwili na akili zake zinavyofanya kazi pamoja na kutambua hatua za mabadiliko ya kibaiolojia anayopitia siku kwa siku katika maisha yake.
Kutambua mabadiliko ya makuzi
Mungu hakutuumba ili tuendelee kuwa watoto wadogo siku zote, anataka tukue kiakili na kihisia na kuwa watu wazima na kisha kuwa wazee kama mchakato wa kibaiolojia. Msichana ni mtu wa jinsia ya kike anayetoka utotoni kwenda katika utu uzima, anaweza kuwa katika hatua za mwanzoni za kupevuka au hatua za mwishoni za kukomaa kama tunda linavyokomaa kisha linaiva tayari kwa kuliwa, ndivyo ilivyo kwa binadamu pia hupitia hatua mbalimbali za mabadiliko ya makuzi, yanayotawaliwa na mfumo wa kibaiolojia.Mabadiliko haya ya kupevuka na kukomaa katika mchakato wa makuzi yanatawaliwa na utendaji wa tezi iliyopo ndani ya ubongo inayojulikana kama ‘pituitary gland’. Tezi hii huzalisha vichocheo (homoni) vinavyoingia katika damu na kusambazwa mwili mzima na kuanzisha mabadiliko wakati wa balehe. Kabla ya kufikia umri wa miaka 9 tezi hii huwa haizalishi vichocheo vya ukuzi wa kijinsia.
Mabadiliko ya kimwili
Mtoto wa kike anapofikia umri wa kati ya miaka 9 na 15, kama ana afya na lishe nzuri, anaanza kuona mabadiliko ya kawaida katika mwili wake. Kwa kawaida huanza kuota nywele kinenani na kwapani, kukua kwa matiti, kuvunja ungo, kunenepa kwa makalio na kiuno kuwa chembamba. Katika kipindi hiki pia viungo vya sehemu ya siri (uke) vinaongezeka ukubwa na unyevunyevu. Mwili huongezeka kimo na uzito na kuanza kuwa na umbo la mama mtu mzima. Sauti pia hubadilika na kuwa nyororo sana. Ngozi pia hubadilika na kunawili, huwa laini na ya kupendeza sana ingawa wakati mwingine inaweza kuwa na chunusi kiasi au nyingi.Maumbile ya uke na viungo vya uzazi
Viungo vya uzazi vya nje
1. Kinena:
Hii ni sehemu ya mwili iliyo kati ya tumbo na tupu ya mbele. Sehemu hii imefanyizwa kwa nyama yenye mafuta inayofunika fupa la mbele la nyonga. Wakati msichana anapobalehe, kinena hufunikwa na nywele.2. Mashavu makubwa ya nje:
Mashavu haya ni nyama kubwa zinazofunikwa na ngozi pande mbili, upande wa kulia na upande wa kushoto wa uke. Kwa juu hukutana na kinena na kwa chini hukutana juu ya njia ya haja kubwa ili kutengeneza msamba. Nyama hizi pia zimejaa mafuta kwa ndani na zina tezi nyingi zinazozalisha jasho, wakati wa balehe mashavu haya huota nywele kwa nje ingawa kwa ndani hayawi na nywele.3. Midomo midogo ya ndani ya uke:
Hii ni mikunjo miwili ya ngozi iliyo ndani ya mashavu makubwa ya nje kulia na kushoto katika chumba cha mbele cha uchi wa mwanamke. Midomo midogo huungana kwa juu na kutengeneza govi ambalo hufunika kinembe. Kwa chini huungana na kutengeneza nyama laini ijulikanayo kama mwanzo wa msamba.Midomo midogo ya ndani haina nywele hata wakati wa balehe ila ina tezi nyingi za mafuta mafuta (sebaceous glands), nyama zinazovutika, mishipa mingi ya damu na miishio ya mishipa ya hisia na fahamu. Kazi ya midomo hii ni pamoja na kufunika njia ya mkojo na njia ya uzazi, ili zisiingiliwe kwa urahisi na vitu visivyotakiwa kama vile bakteria wanaosababisha magonjwa. Midomo hii pia ni ya muhimu wakati wa tendo la ndoa kwani huongeza hamu na hisia za tendo la ndoa kwa watu waliooana.
4. Kinembe / kisimi:
Hiki ni kiungo kidogo cha mduara na umbo kama harage au kokwa ya korosho chenye urefu upatao sentimita 2.5 hivi. Kiungo hiki kiko juu ya njia ya mkojo. Kinembe kina sehemu kuu tatu yaani kichwa, mwili na miguu miwili (The clitoral crura). Miguu ya kinembe ni sehemu iliyo ndani kushoto na kulia mwa njia ya mkojo.Kinembe kama ilivyo kwa uume, kina misuli yenye uwezo wa kuvutika na kuongezeka urefu na ukubwa wake wakati mwanamke anapopata hamu ya tendo la ndoa. Sehemu hii ya mwili wa msichana na mwanamke ni sehemu nyeti sana, ina mishipa mingi ya fahamu na hisia.
5. Chumba cha mbele cha uke (vestibule):
Chumba hiki kina umbo la pembe tatu linalotengenezwa kwa juu na kinembe, midomo midogo ya ndani kulia na kushoto pamoja na mwanzo wa msamba kwa chini. Katika chumba hiki cha uke kuna matundu manne (4). Tundu la njia ya mkojo – Tundu hili liko katikati ya kisimi na tundu la njia ya uzazi. Kazi yake ni kupitisha mkojo na mara chache hatumika kupitisha kemikali zinazotumika katika uchunguzi wa kitabibu.
Tundu la njia ya uzazi: Tundu hili ni kama bomba kati ya chumba cha mbele cha uke na shingo ya mji wa uzazi.Tundu hili hufunikwa na ngozi laini ijulikanayo kama bikira kama msichana hajaingiliwa na kitu chochote katika tupu ya mbele. Tundu la njia ya uzazi ni maalumu kwa ajili ya tendo la ndoa wakati mwanamke anapokuwa amekomaa, pia hupitisha damu ya hedhi na kazi yake nyingine ni kupitisha mtoto wakati wa kujifungua.
Matundu mawili ya tezi za Bartholin: matundu haya yako kwa chini kila upande wa uchi kulia na kushoto katika eneo ambalo msamba unaanzia. Wakati wa kujamiiana mwanamke akiwa na hamu na utayari wa tendo la ndoa, matundu haya huzalisha majimaji meupe yanayoteleza kama ute wa yai bichi ili kulainisha uchi tayari kwa tendo la ndoa bila kusababisha michubuko na maumivu.
6. Msamba:
Hii ni sehemu ya katikati ya mwili inayounganisha mapaja na kiwiliwili. Ni ngozi laini kati ya mapaja, uke na njia ya haja kubwa.Viungo vya uzazi vya ndani
1. Njia ya uzazi (vagina): Njia hii yenye umbo la bomba imetengenezwa kwa misuli maalumu yenye uwezo wa kutanuka wakati wa tendo la ndoa na wakati wa kujifungua mtoto kwa njia asilia. Njia ya uzazi ina urefu wa takribani sentimeta 7 hadi 9 hivi na kipenyo chake ni kama sentimeta 2.5 hivi. Ndani ya njia ya uzazi kuna chembechembe za mwili (cells) zinazozalisha majimaji meupe yenye uwezo wa kulainisha, kusafisha na kuzuia uambukizo ndani ya tupu ya mwanamke katika hali ya kawaida.2. Mji wa mimba:
Huu ni mfuko maalumu wenye umbo la pembe tatu ambamo mimba hutunga na kukua wakati mwanamke anapokuwa mjamzito. Ndani ya mfuko huu, ndimo damu ya hedhi inamotoka wakati mwanamke anapopata hedhi kila mwezi kama hana matatizo ya kiafya.Mji wa mimba una ukubwa unaolingana sawa na ngumi ya muhusika, urefu wake ni takribani sentimeta 8 hivi na upana wake kwa juu ni takribani sentimeta 5 na unene wa kuta za mji huu ni kama sentimeta 1.25 hivi na uzito wake unakadiliwa kuwa gram 50-80. Chini yake mji wa mimba una shingo yenye mlango (cervix). Sehemu kubwa ya mlago wa mji wa mimba iko ndani ya njia ya uzazi.
Mlango wa mji wa mimba husaidia kuzuia uume usiingie ndani ya mji wa mimba na pia ndio mlango wa kupitisha mbegu za uzazi za mwanaume ili ziingie ndani ya mji wa mimba. Mlango huu pia ndio unaoruhusu mtoto kuzaliwa kwa njia ya asili wakati wa kujifungua.Kazi nyingine ya mlango huu pia ni kupitisha damu ya hedhi ili itoke nje.
3. Mirija ya uzazi:
Kuna mirija miwili ya uzazi, mrija mmoja kila upande kulia na kushoto. Mirija hii inakadiliwa kuwa na urefu wa sentimeta 10 kila mmoja. Kila mrija una matundu mawili, tundu moja liko upande wa mji wa mimba na tundu jingine lipo ubavuni kuelekea mfuko wa mayai. Mirija hii ni midogo kiasi kwamba kipenyo chake hukadiliwa kuwa kati ya milimeta 1 hadi 2 hivi.Kazi kubwa ya mirija ya uzazi ni kusafirisha mayai na kupitisha mbegu za kiume ili vikutane kwa ajili yakutunga mimba. Mirija hii huzalisha majimaji yanayo dumisha uhai wa yai wakati linasubiri mbegu ya kiume kabla ya kuungana kwa ajili ya kutunga mimba.
4. Mifuko ya mayai:
Kuna mifuko miwili inayazalisha mayai, mfuko mmoja kila upande kulia na kushoto, mfuko mmoja unakadiliwa kuwa na urefu wa sentimeta 3 na upana wa sentimeta 2, wakati unene wake ni kama sentmeta 1 hivi. Kazi kubwa ya mifuko hii ni kuzalisha mayai na kuzalisha vichocheo vya ujinsia vinavodumisha hali ya kuwa mwanamke na kuimarisha mifupa.Mifuko hii ina uwezo wa kuzalisha takribani mayai 360 hadi 400 katika kipindi chote ambacho mwanamke ana uwezo wa kuzaa, yaani tangu kuvunja ungo hadi kukoma kwa damu ya mwezi.
Maumbile na ukuaji wa matiti
Matiti ya msichana huanza kukua na kunenepa pale msichana anapofikia umri wa miaka kati ya 9 na 15. Matiti yanaweza kukua na kuwa makubwa, ya wastani au kuwa madogo, yote hiyo ni hali ya kawaida na hutegemea uzalishaji wa kichocheo cha Oestrogeni na vinasaba (genetic traits) ambavyo msichana amerithi toka kwa wazazi wake.Kwa ndani matiti yana tezi zilizosukwa kwa mfano kama ilivyo ndani ya chungwa, tezi hizi hutengeneza maziwa wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha. Ndani ya matiti pia kuna mirija inayopitisha maziwa na vifuko (sinuses) vinavyotunza maziwa. Kwa nje matiti yana chuchu inayozungukwa na ngozi nyeusi (Areola). Ngozi hii huongezeka weusi wake wakati wa balehe. Kwa wastani matiti huchukua takribani miaka minne (4) kukua kikamilifu, ingawa kwa wasichana wengine matiti hukua na kukomaa kikamilifu ndani ya mwaka mmoja baada ya balehe.
Katika hali ya kawaida matiti ya msichana hukua kwa namna tofauti, titi moja linaweza kuwa kubwa kidogo zaidi ya jingine ingawa siyo lazima hali hiyo kutokea.
Matiti ya msichana ni sehemu nyeti ya mwili inayoweza kuzalisha msisimko wa kingono na mwitikio wa hisia. Matiti ya msichana yakitomaswatomaswa, yanaweza kuzalisha hisia za maumivu kidogo, endapo matiti yatashikwashikwa na mtu wa jinsia tofauti kwa ridhaa ya mhusika matiti yanaweza kuzalisha hisia za hamu ya tendo la ndoa na kusababisha mwitikio wa msichana unaosababisha tupu ya mbele kuzalisha majimaji mengi yenye utelezitelezi.
Msichana inampasa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayegusa au kushika matiti yake bila ridhaa yake mwenyewe na kwa sababu sahihi. Ni muhimu kukumbuka kuwa, matiti ya msichana na mwanamke huwavutia sana wanaume hasa vijana, na wanapenda sana kuyashikashika. Msichana anayeruhusu wanaume washikeshike matiti yake anajiweka katika hatari kubwa ya ngono hatarishi na kubakwa.
Hatua za makuzi ya matiti na nywele sehemu za siri kwa wasichana
Umri (miaka) Matiti Nywele za kinenani< 9 Chuchu pekee huchomoza. Vinywele laini (malaika) vinajitokeza.
10-11 Ukubwa wa matiti unaanza, kibonge kinaanza kushikika ndani ya titi. Vinywele laini vyeusi vinaanza kuonekana pembeni hasa kwenye mashavu ya nje lakini kwa uchache sana.
11-12 Titi huchomoza na kuvimba. Nywele nyeusi zinaanza kusambaa kinenani ingawa zinakuwa hazijakomaa kikamilifu.
12-13 Titi linaanza kuchongoka na kuwa na tezi ndani. Nywele zinakomaa na kusambaa kinena kizima.
14-15 Titi huwa la kiutu uzima ingawa linaendelea kukomaa. Nywele komavu zinazosambaa kuelekea mapajani na katika msamba.
Chanzo: Tanner classification
Utunzaji wa matiti
Matiti ya msichana ni mojawapo ya sehemu za mwili wa msichana ambazo zinahitaji uangalizi wa kina. Matiti ya msichana yanaweza kushambuliwa na magonjwa kadhaa, moja ya magonjwa hayo ni kansa ya matiti. Wasichana wengi hawafikirii kuhusu kansa ya matiti, lakini ni ukweli usiopingika kwamba hata wasichana hupata ugonjwa huu ingawa ni mara chache kwa wasichana chini ya miaka 20 kupata saratani ya matiti.Ni vizuri kwa msichana kutambua ukweli huu na kuanza kuufanyia kazi kwa kufanya uchunguzi wa matiti mara kwa mara, ili kuepuka kupata tatizo hili bila habari. Kwa bahati mbaya sana ni kwamba wasichana wanapopata kansa ya matiti huwa ni yenye hatari zaidi na huwa ni vigumu kuitibu ikiwa mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu sahihi mapema.
Mara nyingi uchunguzi wa matiti katika jamii huwalenga wanawake wenye miaka 40 na kuendelea na hii hufanya kundi la wasichana kusahauliwa. Kama msichana atakuwa na tatizo la saratani (kansa) ya matiti huchukua muda mrefu kugundulika na anapogundulika kuwa ana tatizo la kansa ya matiti huwa amekwisha fikia hatua za mwisho za ugonjwa ambazo ni hatari na tiba huwa haiwezekani tena kumponya.
Wanawake wengi wako katika hatari ya kupata saratani ya matiti katika kipindi cha maisha yao. Hatari ni kubwa zaidi kwa wanawake ambao mama au dada zao wamewahi kupata kansa ya matiti. Habari njema ni kwamba kansa ya matiti ni tatizo linalokuwa na kuongezeka taratibu, hivyo basi, kama msichana au mwanamke atajenga mazoea ya kujichunguza matiti yake mara kwa mara, anaweza kugundua tatizo mapema na kupata matibabu kabla hajachelewa.
Uchunguzi wa matiti
Dalili zifuatazo huashiria kuwepo kwa saratani ya matiti au hali ya matiti isiyo kuwa ya kawaida.
• Uvimbe usiokuwa na maumivu ndani ya titi moja au yote.• Hali ya wekundu wa ngozi au kidonda kwenye titi kisichopona baada ya matibabu sahihi ya muda mrefu.
• Kusinyaa na kukunjamana kwa ngozi ya titi inayozunguka chuchu na kufanana kama ganda la chungwa au limao.
• Chuchu inayoingia ndani tofauti na nyingine.
• Titi linapominywa na kutoa damu au majimaji yenye damu au rangi isiyokuwa ya kawaida.
Msichana ni lazima ajenge tabia ya kujiangalia katika kioo kwa lengo la kuchunguza matiti yake ili kuona kama yanatofautiana ukubwa, umbile na hali ya rangi ya ngozi. Ni muhimu pia kuangalia hali ya chuchu na majimaji yanayotoka baada ya kuminya au kukamua matiti.
Unapochunguza matiti anza na titi moja moja, inua mkono wa kulia, tomasa kila sehemu ya titi la kulia kwa kutumia mkono wa kushoto. Kagua kwa kuanza na upande wa nje kuelekea ndani huku ukitumia ubapa wa vidole upande wa ndani ya kiganja. Minya titi taratibu ili kubaini uvimbe au maumivu na uzito usiokuwa wa kawaida. Fanya hivyo kwa matiti yote. Baada ya hapo, lala chini kwenye mkeka au godoro, weka mto chini ya bega la kulia na mkono wako wa kulia weka chini ya kichwa kisha taratibu tomasa titi kama lina kivimbe au donge na fanya hivyo kwa matiti yote.Ukigundua hali yoyote inayotia mashaka onana na wataalamu wa afya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Uchunguzi wa matiti ni bora ufanyike siku chache baada ya kumaliza damu ya hedhi. Na kama msichana anatumia dawa za vidonge vya kupanga uzazi na kuzuia mimba, anashauriwa kuchunguza matiti yake siku ya kwanza anapoanza paketi mpya ya dawa hizo. Uchunguzi wa matiti kwa wasichana na wanawake wapasa kuwa kawaida na mazoea ya maisha yote yaliyobaki. Ingawa siyo kila tatizo la matiti humaanisha saratani (kansa), ni muhimu kuonana na daktari ili kupata ushauri wa kitabibu pale unapoona badiliko lolote lisilokuwa la kawaida katika matiti yako.
Kinga ya saratani ya matiti
Kinga bora ya saratani ya matiti ni zile njia au kawaida za maisha zinazosaidia kupunguza uwezekano wa kupata kansa. Vyanzo vingi vya ugonjwa huu havizuiliki ila vinapunguzwa makali yake ili visitokeze saratani. Kula vyakula vyenye asili ya mimea kama vile maharage ya soya, kabeji na machungwa ni njia inayosaidia sana. Inasadikiwa kuwa kabeji zina dawa aina ya ‘glucobrassicin’ inayo punguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti.Kupunguza matumizi ya simu za mkononi zinazozalisha mionzi ambayo hupunguza kichocheo cha melatonin mwilini, pia husaidia wasichana wengi kuepuka kupata tatizo la saratani ya matiti kwani melatonin ni kinga nzuri dhidi ya saratani ya matiti, kwa vile inapunguza uwezekano wa kupata saratani. Kupunguza matumizi ya pombe na kuepuka utumiaji wa tumbaku pia ni muhimu. Mazoezi ya mwili pia ni muhimu kwa afya ya mwili kwa ujumla.
Maumivu ya matiti
Wakati mwingine baadhi ya wasichana hupata maumivu ya matiti yote mawili au titi moja bila sababu bayana, kama vile uvimbe unaotokana na uambukizo wa bakteria au maumivu ya jeraha. Hali hii kitabibu hujulikana kwa jina la ‘mastalgia’. Maumivu haya hutokea kwa kipindi na mara nyingi huambatana na mzunguko wa hedhi na hutokea pale damu ya hedhi inapoanza. Maumivu haya yaweza kuwa ya wastani au wakati mwingine yaweza kuwa makali sana. Ingawa inasadikiwa kuwa chanzo cha tatizo hili ni vichocheo vya ujinsia hasa wakati wa kupevuka kwa mayai ndani ya mifuko yake, lakini wakati mwingine ni vigumu kuelewa chanzo chake hasa pale maumivu yanapotokea katika titi moja pekee.Katika hali kama hii, msichana anashauriwa kuepuka vinywaji vyenye ‘caffeine’ kama vile majani ya chai, kahawa, cocacola, pepsi, cocoa, na redbull. Pia ni vema kuepuka kula chocolate na vyakula vyenye chumvi na mafuta kwa wingi. Caffeine ina kemikali aina ya ‘methylxanthine’ inayotanua mishipa ya damu na kuongeza zaidi maumivu ya matiti. Chumvi huongeza mkusanyiko wa maji katika matiti na kuongeza ukubwa wa tatizo.
Inashauriwa kula vyakula vyenye vitamini E kwa wingi kama vile karanga, mboga za majani, mayai na nafaka ili kusaidia uponaji. Kutumia vidonge vya uzazi wa mpango na kuvaa sidilia inayobana vema, kunapunguza maumivu hasa wakati wa kufanya mazoezi. Mazoezi husaidia kukabili athari za msongo wa mawazo ambao pia huchangia ukubwa wa tatizo.
Maumivu yakizidi ni bora kuonana na daktari kwa uchunguzi zaidi na matibabu. Dawa za kutuliza maumivu kama Paracetamol na Diclofenac gel ya kupata zinaweza kutumiwa ili kupunguza maumivu. Dawa kama Danazol, Bromocriptrine au Tamoxifen Cictrate zinaweza kutumiwa chini ya uangalizi wa daktari ili kukabiliana na tatizo hili.
Kupevuka kwa mayai
Kila mwezi mifuko ya mayai ya msichana hupevusha yai na kuliachilia ili liingie katika mirija ya uzazi kwa ajili ya kutunga mimba kama litakutana na mbegu za kiume. Kitendo cha kupevuka kwa yai hutokea takribani siku 14 kabla ya kuona damu ya hedhi au kabla ya kuvunja ungo. Hii ina maana kuwa msichana akifanya ngono isiyo salama mara kwa mara kabla ya kuvunja ungo, anaweza kupata mimba bila kuona damu ya hedhi kwa mara ya kwanza.Kupevuka kwa mayai katika mifuko ya mayai hutegemea utendaji wa tezi ya pituitary katika ubongo inayozalisha vichocheo vya kupevusha mayai pale msichana anapoanza kubalehe. Kila mfuko wa mayai unakuwa na mayai mengi machanga ingawa machache yanayotazamiwa kupevuka katika kipindi chote cha umri wa mwanamke anapokuwa na uwezo wa kuzaa.
Kuvunja ungo na damu ya hedhi
Kuvunja ungo ni tukio la kuona damu ya hedhi kwa mara ya kwanza msichana anapofikia umri kati ya miaka 9 na 15. Hii hutokea kwa msichana bila kupata jeraha lolote katika sehemu ya tupu ya mbele. Wasichana wengi hupata hofu wanapoona hali hii kwa mara ya kwanza, lakini ukweli ni kwamba hii ni hali ya kawaida na ya muhimu katika makuzi na kupevuka kwa msichana. Ikitokea hivyo msichana anashauriwa amwambie mzazi wake au mlezi wake, au matron ikiwa yuko shuleni, ili amuelekeze jinsi ya kukabiliana na hali hiyo kiafya.Ikitokea kuwa uko peke yako na hali hiyo imekutokea wewe msichana, huna sababu ya kubabaika. Nenda kanawe kwa maji safi na sabuni kisha vaa pedi au kitambaa safi chenye asili ya pamba. Badilisha pedi au kitambaa hicho mara kwa mara kulingana na wingi wa utokaji damu.
Hali ya damu ya hedhi kwa kawaida inaweza kudumu kwa kipindi cha siku 3 hadi 5. Ni busara kwa msichana kuweka kumbukumbu za tukio la kuvunja ungo maishini mwake, maana ni tukio ambalo husaidia katika maswala ya utabibu kuhusiana na matatizo ya hedhi na maswala ya afya ya uzazi kwa ujumla hapo baadae wakati daktari anapochukua historia ya kitabibu. Andika tukio hili muhimu katika daftari la kumbukumbu (notebook) na uhifadhi vizuri kwa ajili ya rejea hapo baadaye na ikiwezekana jizoeze kuikumbuka tarehe hii kichwani.
Damu ya hedhi humtokea mwanamke takribani kila baada ya siku 28 toka siku ya kuona damu ya hedhi kwa mara ya kwanza hadi umri wa miaka 45 au zaidi. Ingawa kuna uhusiano wa vichocheo vinavyopevusha mayai na tukio la damu ya hedhi, lakini inaweza kutokea kabla mayai hayajapevuka.
Damu ya hedhi bila mayai kupevuka hutokea mara nyingi kwa wasichana, wakati wa kipindi ambacho mwanamke amejifungua karibuni au wakati mwanamke anakaribia kukomaa kuona damu ya hedhi kwa sababu ya uzee (perimenapausal period).
Mzunguko wa damu ya hedhi hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke. Wanawake wachache zaidi hupata damu ya hedhi kila baada ya siku 35, ingawa walio wengi hupata kila baada ya siku 28, na wengine wachache huingia kila baada ya siku 21.
Wakati wa hedhi au siku chache kabla ya kuona damu ya hedhi wanawake wengi hupata hisia zisizo za kawaida ambazo huambatana na mabadiliko ya utendaji wa mwili na hupoteza raha na furaha ya mwanamke. Wasichana wengi katika kipindi hiki hupata msongo wa mawazo na sonona.Wengine hupata maumivu ya kichwa, misuli na tumbo.
Katika kipindi hiki pia wasichana wengi hupata tatizo la chunusi usoni, kukosa usingizi, uchovu wa mwili na hali ya kukasirikakasirika bila sababu za msingi. Sababu kubwa ya mabadiliko haya ni kukosekana na ulinganifu na usawaziko wa vichocheo vya ujinsia mwilini, kichocheo cha oestrogen huongezeka zaidi kuliko kichocheo cha progesterone. Pia katika kipindi hiki kiwango cha sukari katika damu hupungua kiasi cha kuchangia kutokea kwa baadhi ya dalili.
Baadhi ya matatizo ya hedhi
1. Ukosefu wa vipindi vya hedhi:
Ukosefu wa vipindi vya hedhi unaweza kusababishwa na msongo wowote wa mawazo. Msongo unaweza kupindukia au kuwa mkali sana kutokana na utumiaji wa dawa, sigara, pombe na dawa za kulevya. Ukosefu wa vipindi pia unaweza sababishwa na ugonjwa wowote wa muda mrefu au ongezeko la ghafla la uzito wa mwili. Mabadiliko ya homoni pia yanaweza kusababisha tatizo la ukosefu wa vipindi.Ni vizuri msichana au mwanamke kutunza kumbukumbu ya siku ya kwanza ya hedhi yake ya kawaida ambayo ameipata kwa mara ya mwisho (last normal menstrual period). Kumbukumbu hii ni muhimu katika maswala ya kitabibu hasa yale yanayohusiana na afya ya ujinsia na uzazi.
2. Utokaji wa damu kwa muda mrefu :
Mtiririko wa damu unaweza kuwa mrefu kuliko kawaida kutokana na mabadiliko ya homoni, magonjwa ya tezi, ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya ini, magonjwa ya figo, saratani ya damu au magonjwa yanayoathiri uwezo wa damu kuganda.Yote haya yanaweza kusababisha kupindukia kwa urefu wa muda wa mtiririko wa damu.Ieleweke kuwa damu ya hedhi inayodumu zaidi ya siku 8, siyo hali ya kawaida na inahitaji uangalizi wa kitabibu haraka ili kuondoa uwezekano wa msichana kuwa na saratani (kansa) ya mlango wa mji wa kizazi au magonjwa mengine.
3. Maumivu makali ya tumbo wakati wa hedhi:
Katika kipindi hiki wanawake hasa wasichana ambao hawajazaa wanaweza kupata maumivu makali ya tumbo. Hii hutokea kwa sababu mwili huzalisha vichocheo viitwavyo ‘prostaglandins’ ambavyo husisimua nyama za mji wa mimba au kizazi ili usinyae na kujiminya kwa lengo la kusukuma nje damu ya hedhi. Kama vichocheo hivi vikizalishwa kwa wingi husababisha maumivu makali ya tumbo wakati wa hedhi.Matunzo ya afya wakati wa hedhi
Katika kipindi hiki cha hedhi, wasichana hupoteza kiasi cha kutosha cha damu pamoja na madini chuma mwilini. Hali hii inaweza kusababisha upungufu wa damu kama msichana hapati lishe bora na ya kutosha. Ili kuzuia upungufu wa damu na madini mwilini, msichana anatakiwa kula vyakula vyenye madini chuma na chokaa kwa wingi kama vile maharage, soya, korosho, mboga za majani, mayai, njegere, maziwa, samaki, dagaa na nyama.Jambo jingine la msingi sana kukumbukwa na msichana katika kipindi hiki ni kutunza hali ya usafi wa mwili, hasa sehemu za siri na usafi wa mazingira kwa ujumla.Tumia vitambaa safi vilivyo nyooshwa kwa pasi au pedi zilizohifadhiwa katika hali ya usafi.
Hakikisha pedi zinabadilishwa mara kwa mara na inashauriwa kunawa mikono kabla na baada ya kubadilisha pedi. Hii itasaidia kuzuia uwezekano wa kupata ugonjwa hatari wa homa na kuzimia (Toxic Shock Syndrome) unaosababishwa na bakteria hatari kama vile Staphylococcus aureus na Streptococcus. Bakteria hawa wanazaliana kwa wingi kwenye damu inayokuwa kwenye pedi au kitambaa kinachokaa sehemu za siri kwa muda mrefu bila kubadilishwa.
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kupanda kwa joto la mwili ghafla, maumivu ya kichwa, kushuka kwa shinikizo la damu, kuharisha, kutapika, kuuma kwa misuli ya mwili, kichwa kuwa chepesi, kuzimia au kupoteza fahamu na kutokwa na vipele mwilini. Dalili zingine ni kuwa na vidonda kooni pamoja na madoa mekundu ya damu machoni au katika ngozi laini ya ukeni.
Ugonjwa huu unaweza kusababisha moyo na figo vishindwe kufanya kazi, kutokwa damu hovyo mwilini, kuchanganyikiwa au kupata kifafa. Mgonjwa mwenye tatizo hili, huhitaji matibabu ya dharura na ya haraka ili kuokoa maisha yake (medical emergency).
Ili kudumisha usafi wa mazingira na kuzuia uenezaji wa magonjwa, hakikisha kuwa pedi zilizotumika hazitupwi ovyo. Tupa pedi hizo kwenye choo cha shimo au zichomwe kwa moto baada ya kumwagia mafuta ya taa kidogo. Kumbuka kuwa pedi zilizotumika zikitupwa ndani ya tundu la choo cha kuvuta kwa maji, zinaweza kusababisha choo kuziba na kusababisha usumbufu na athari mbaya kwa afya ya mazingira.
Jinsi ya kudhibiti maumivu ya tumbo wakati wa hedhi
• Sugua tumbo lako sehemu ya chini ya kitovu kwa kutumia mikono. Hii husaidia misuli ya mji wa mimba iliyosinyaa na kukaza ilegee na kupunguza maumivu.• Kandakanda tumbo kwa maji ya uvuguvugu au weka maji ya uvuguvugu katika chupa ya plastiki na ukande tumbo chini ya kitovu kwa kutumia chupa hiyo.
• Kunywa maji ya moto yaliowekwa tangawizi wakati wa kuyachemsha au weka miguu kwenye beseni la maji ya vuguvugu.
• Tembeatembea au fanya mazoezi, usilale kitandani kutokana na maumivu, kulala kunaongeza ukubwa wa tatizo.
• Minya sehemu za mwili zinazozalisha maumivu kwa dakika 3 hivi, hii itapunguza maumivu ya tumbo. Sehemu ya mwili kama vile katikati ya vidole gumba na kidole cha kwanza au kwenye kifundo cha sikio chini karibu na pale wasichana wanapotoboa kuweka hereni pakiminywa huzalisha maumivu.
• Wakati wa hedhi usile chakula chenye chumvi nyingi na epuka vinywaji vyenye caffeini kama majani ya chai, kahawa, soda aina ya pepsi au cocacola na redbulls. Kula korosho kwa wingi kwa vile madini ya magnesium yaliyomo ndani ya korosho husaidia kupunguza maumivu ya hedhi kwa kulegeza misuli ya mji wa mimba. Maumivu yakizidi ni busara kuonana na daktari au kuenda kupata huduma ya afya ya msingi katika kituo chochote cha afya kilicho karibu nawe.
Mabadiliko ya kihisia
Msichana hupata hisia tofauti na zile alizozoea pale anapo balehe, hupendelea mambo ambayo zamani alikuwa hana haja nayo. Hupenda kutumia muda mwingi na wasichana wenzake kuliko wazazi au watu wa familia yake na huwa ni mtu mwenye aibu na haya nyingi. Msichana hupata hisia za kuvutiwa na wavulana na kutaka mahusiano ya kingono, huwa na tamaa ya kutaka kujitegemea kimawazo, kifikra na kiutendaji. Hupata msukumo mpya na uzoefu tofauti wa kimaisha, hupata hisia kuwa watu wengine hawatambui au kuelewa matakwa yake. Hutaka sana kutambuliwa kuwa na yeye yupo na anaweza. Hitaji la kupendwa na kupenda huongezeka na hupenda sana kujiangalia angalia kama anapendeza.Katika kipindi hiki msichana anapenda kuwajibika katika utatuzi na ufumbuzi wa matatizao yake mwenyewe. Hufikiria sana juu ya hali ya maisha ya baadaye yanayohusu mafanikio na kupenda hali ya maisha ya kifahari. Ni kipindi ambacho msichana anaweza kudanganywa kwa urahisi, huweza kumwamini mtu aliyefahamiana naye kwa siku chache kuliko wazazi wake waliomuonyesha upendo na kumtunza kwa gharama kubwa muda wa miaka mingi. Hujaribu kutatua matatizo yanayohitaji uzoefu wa kiutu uzima kwa uzoefu wake aliokuwa nao katika kipindi kilichopita cha utoto.
Matunzo ya mwili wa msichana
Wakati wa balehe msichana anatakiwa kuongeza jitihada za kutunza mwili wake maradufu ili kuwa katika hali ya usafi muda wote. Katika kipindi hiki ngozi ya msichana huanza kuzalisha majimaji ya mwili kwa wingi kuliko kipindi cha nyuma cha utoto kabla ya balehe. Baadhi ya majimaji yanayozalishwa kwa wingi katika kipindi hiki cha makuzi ya msichana yanaweza kusababisha harufu mbaya ya mwili (kikwapa) kama msichana hataoga mara kwa mara na kusafisha sehemu nyeti vizuri. Kiasi kikubwa cha majimaji ya mwili katika kipindi hiki ni jasho.Tezi zinazozalisha jasho huwa zinaongeza utendaji wake pale msichana anapobalehe. Tezi nyingi za jasho ziko makwapani, sehemu za siri, miguuni na katika viganja vya mikono.Msichana anahitaji kunawa na kusafisha vizuri ndani ya uke, ni lazima kuhakikisha kuwa katikati ya mashavu ya nje na yale ya ndani ya utupu wa mbele kumesafishwa vizuri na kwa uangalifu na umakini mkubwa. Inashauriwa kuwa sehemu ya ndani ya njia ya uzazi kusisafishwe kwa kutumia sabuni au dawa zenye kemikali.
Uchi wa mwanamke kwa ndani kabisa katika njia ya uzazi hujisafisha wenyewe kwa kuzalisha ute laini unaolinda na kutunza nyama na ngozi laini ya ndani. Msichana anaposafisha sehemu zake za siri ni vizuri kutumia sabuni za kawaida za kuogea zisizokuwa na dawa au kemikali zinazoua bakteria au zile zinazoweza kusababisha muwasho sehemu za siri.
Sehemu za siri zikisha safishwa kwa maji na sabuni ni vyema kukaushwa kwa karatasi laini sana au kitambaa kisafi chenye asili ya pamba ambacho ni safi kabisa kisha msichana avae chupi ambayo ni safi na inayopitisha hewa vizuri na kunyonya unyevunyevu. Ni muhimu kuvaa chupi safi kila siku hasa iliyotengenezwa kwa kitambaa cha nguo ya pamba.
Majimaji meupe ukeni
Kutokwa na majimaji meupe yasiyo na rangi wala harufu mbaya (leukorrhoea) katika sehemu za siri ukeni, ni jambo la kawaida kwa wasichana na wanawake wenye afya. Ila majimaji hayo yakiwa mengi sana kiasi cha kuchilizika mapajani na kulowanisha kabisa nguo za ndani, hali hiyo yaweza kuwa sio ya kawaida.Majimaji ya ukeni yanayowasha au kuwa na harufu mbaya au yaliyoganda kama maziwa ya mgando au tui la nazi yanatokana na uambukizo wa kuvu (fungus), trichomonas vaginalis au kisonono. Unyevunyevu sehemu za siri kwa muda mrefu unaweza kutokeza harufu mbaya kutokana na kushambuliwa na bakteria wanaokaa na kuzaliana kwenye ngozi. Harufu mbaya mara nyingi husababisha usumbufu kwa msichana mwenyewe na watu wengine anaokuwa nao karibu. Hali kama hii inapojitokeza msichana hana budi kunawa mara kwa mara kwa maji na sabuni isiyokuwa na kemikali kali na kujikausha kwa kitambaa safi cha nguo ya pamba au karatasi laini sana (Toilet paper).
Kuvaa nguo za ndani zinazonyonya na kukausha unyevunyevu au zinazopitisha hewa na kupunguza joto sehemu za siri kama vile chupi zenye matundu madogo madogo maalumu sehemu ya mbele, ni jambo linalosaidia kupunguza athari za majimaji yanayotoka ukeni. Ni vema kuepuka uvaaji wa chupi zinazobana sana na zile zilizotengenezwa kwa kitambaa cheusi cha nguo aina ya polyster hasa katika maeneo ya joto jingi.
Utunzaji wa nywele zinazoota sehemu ya siri pia ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la unyevunyevu na magonjwa katika tupu ya mbele ya mwanamke. Nywele zilizonyolewa kwa mkasi na kubakia fupi hurahisisha usafi na kuweka sehemu za siri katika hali ya ukavu mara baada ya kujisaidia.Wakati wa kujisafisha baada ya kujisaidia, hasa haja kubwa, ni vema kusafisha tupu ya mbele kwanza kabla ya kusafisha tupu ya nyuma. Hii inasaidia kuepuka kuleta bakteria toka katika njia ya haja kubwa na kuwaingiza ukeni. Kanuni hii isipozingatiwa mara nyingi huleta athari za uambukizo na magonjwa yanayoshambulia njia ya mkojo.
Ikiwa majimaji ya ukeni yanasababisha muwasho sehemu za siri ni vema kujisafisha kwa maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na maji ya limau. Mchanganyiko wa maji na maji ya limao pia unaweza kutumiwa kwa njia ya kuwekwa ndani ya beseni kubwa kisha mgonjwa akae ndani yake kwa dakika 15 kutwa mara mbili, asubui na jioni kwa muda wa majuma mawili mfululizo. Kutumia maji ya moto sana kunaweza kuleta madhara ya kuungua kwa sehemu za siri ambazo ni laini sana na zenye miishio mingi ya mishipa ya fahamu (neva).
Muwasho wa ukeni pia unaweza kutibiwa kwa dawa asilia kwa kutumia vitunguu saumu. Menya punje moja ya kitunguu saumu kwa uangalifu usiitoboe, ifunge vizuri katia kitambaa au katika bendeji iliyo safi. Nawa mikono yako iwe safi, kisha ingiza ukeni kitunguu saumu ulichofunga ndani ya kitambaa. Fanya hivyo kila siku usiku baada ya kuoga na kabla ya kulala kwa kipindi cha majuma mawili mfululizo.Kumbuka kuindoa ukeni dawa hiyo kila asubuhi na kuweka mpya kila siku usiku.
Kunywa juice iliyotengenezwa kutokana na mchanganyiko wa karoti, kitunguu saumu, matango na majani ya kabichi au kunywa maji ya matunda kiasi cha bilauri (glasi) moja kutwa mara tatu kwa kipindi cha majuma matatu mfululizo kunaongeza nguvu na kinga ya mwili ya kupambana na kuvu wanaoleta muwasho sehemu za siri.
Tatizo la chunusi
Chunusi ni jambo la kawaida wakati wa balehe na zinatokea kwa sababu msichana anafikia hatua ya muhimu ya maisha ya kutoka utotoni kwenda katika utu uzima.Wakati wa balehe, tezi za ngozi zinazozalisha mafuta mafuta yanayolainisha ngozi hutenda kazi zake kwa uchangamfu mkubwa na kuzalisha mafuta ya ngozi yaitwayo ‘sebum’Kazi ya sebum ni kulainisha ngozi na kuleta mwonekano wa kisichana unaopendeza na kuvutia. Sebum inapozalishwa kwa wingi inasababisha vinyweleo katika ngozi vizibe na kuleta tatizo la chunusi. Chunusi zikiwa nyingi sana zinatazamwa kama ugonjwa wa ngozi na hili linaweza kuwa tatizo la kurithi. Ikiwa wazazi au ndugu wa msichana walikuwa na chunusi nyingi, kuna uwezekano mkubwa msichana pia kupata chunusi kwa wingi.
Hofu, woga na wasiwasi pia vinaweza kuchangia msichana kupata chunusi. Hii huwatokea wasichana wengi wanaopata hofu wakati wa mitihani au muda mfupi baada ya hedhi. Licha ya ukweli kuwa mahangaiko ya kihisia husababisha chunusi, tatizo la chunusi pia husababisha tatizo la mahangaiko ya kihisia kwa wasichana wengi wanao hangaikia urembo na uzuri wa ngozi ya usoni. Wasichana wengi wanaopata tatizo la chunusi hawafurahii kile wanachokiona katika kioo wanapojipodoa, lakini ukweli ni kwamba chunusi hazitoshi kuwa chanzo cha kumpotezea msichana raha na furaha katika maisha yake. Pale chunusi zinapokuwa tatizo la kihisia, msichana hana budi kushughulikia tatizo hili kwa namna ambayo inadumisha afya ya mwili na akili zake.
Kukabiliana na tatizo la chunusi
1. Safisha uso kwa maji na sabuni kila siku jioni na asubuhi.Fanya hivyo pia unapomaliza kufanya mazoezi au unapotokwa na jasho. Msichana yeyote asikubali kulala usiku bila kusafisha uso au kuoga. Hii itasaidia kuondoa mafuta kwenye ngozi na kupunguza bakteria wanaoshambulia na kusababisha uvimbe wa chunusi.
2. Usikamue chunusi ambazo hazijaiva, pia usizishikeshike ili kuepuka makovu meusi usoni na hatari ya kupata uvimbe wa uso pamoja na ugonjwa hatari wa ubongo (cavernous sinus thrombosis). Mtu akipata ugonjwa wa ubongo unaotokana na kukamua chunusi, anaweza kupoteza maisha kama hakupata matibabu ya haraka na ya uhakika na katika hali kama hii mtu mwenye imani za kishirikina anaweza kufikiri kuwa amerogwa.
3. Msichana mwenye tatizo la chunusi imempasa kuepuka kutumia vipodozi vyenye mafuta na vichocheo vya steroidi hasa katika sehemu zenye kuathiriwa na chunusi. Nywele zisafishwe kila siku na mitindo ya nywele inayosababisha
nywele kugusana na ngozi ya usoni au mgongo iepukwe.
4. Pata nafasi na muda wa kukaa kwenye mwanga wa jua kila siku hasa wakati wa asubuhi ili sehemu zenye chunusi zipate mwanga wa jua kwa muda wa wastani. Mwanga wa jua unasaidia kuimarisha afya ya ngozi na kuuwa bakteria wanaosababisha chunusi kuvimba. Tahadhari ichukuliwe kuhusiana na jambo hili kwani kukaa kwenye mwanga wa jua kwa muda mrefu hasababisha ngozi kuzalisha mafuta kwa wingi na kuongeza tatizo la chunusi. Jambo hili pia linaweza kusababisha saratani ya ngozi, kuzeeka kwa ngozi mapema au ngozi kuwa na mikunjo na kukaukiana.
5. Kula vyakula vyenye asili ya mimea, matunda, nafaka na mboga za majani huusaidia mwili kupambana na tatizo hili. Kunywa juisi ya karoti glasi moja kutwa mara tatu kila baada ya saa 8 kwa kipindi cha mwezi mmoja, husaidia katika udhibiti wa chunusi.Unaweza pia kupaka usoni karoti zilizopondwapondwa na kuziacha zikae usoni kwa zaidi ya dakika 20 kila siku kabla ya kuziondoa kwa kunawa maji. Karoti zina vitamini A inayosaidia ngozi ili isipate makovu meusi yatokanayo na chunusi. Kunywa maji mengi kila siku na hakikisha pia unapata mapumziko na usingizi wa kutosha kila siku.
6. Epuka matumazi ya dawa za uzazi wa mpango zenye vichocheo vya ujinsia kama vile vidonge na sindano. Tumia dawa za kusafisha ngozi kama vile ‘benzoyl peroxide cleanser, anza na 2.5%, 5% na hatimae 10%, kusafisha sehemu zote zenye chunusi. Hii husaidia kupunguza bakteria wanaoshambalia chunusi juu ya ngozi na kuifanya ngozi iwe kavu na kupunguza mafuta katika ngozi.Kama chunusi zinazidi hata baada ya kutumia tiba hiyo hapo juu, onana na daktari kwa matibabu zaidi.
Tatizo la harufu mbaya mwilini
Harufu mbaya ya mwili inaweza kuwa ni kikwapa, harufu mbaya ya mdomoni au harufu ya uchi na miguu iliyoshambuliwa na kuvu (fungus). Harufu mbaya ya mwili wa msichana ni tatizo la kiafya, pia hutia doa katika urembo wake. Hali hii isipodhibitiwa inaweza kumsababishia matatizo ya kisaikolojia na kudhuru afya mwili.1. Kikwapa:
Kikwapa ni harufu inayotokana na jasho pamoja na majimaji mengine ya mwili yanaposhambuliwa na bakteria wanaozaliana kwa wingi kwenye ngozi hasa sehemu za mwili zisizopata hewa ya kutosha na zile zenye unyevunyevu kama vile kwapani, sehemu za siri na miguuni katikati ya vidole.Tatizo la kikwapa pia linaweza kuwa na uhusiano wa karibu na sumu zinazotoka mwilini baada ya mtu kula au kutumia kwa wingi vyakula kama nyama, samaki pamoja na viungo vyenye harufu kali kama hiliki, mdalasini, tangawizi na vitunguu saumu. Kunywa maji kidogo na kutokuoga mara kwa mara hasa sehemu zenye joto jingi pia huchangia kutokea kwa tatizo la kikwapa.
Yapo magonjwa yanayosababisha mwili kuwa na harufu mbaya. Magonjwa ya ini, figo au utumbo yanaweza kusababisha sumu zisitolewe mwilini kwa njia ya kawaida na badala yake hutoka kupitia kwenye ngozi na kusababisha harufu mbaya ya mwili. Ugonjwa wa kisukari pia husababisha mgonjwa kutoa jasho jingi ambalo hutoa mchango mkubwa katika harufu ya mwili. Magonjwa ya kuvu ukeni na miguuni pia husababisha mwili kutoa harufu mbaya.
Hali ya wasiwasi, woga, msongo wa mawazo na sononeko hufanya utendaji wa tezi za jasho hasa zilizopo kwapani na sehemu za siri kuzalisha jasho lenye protein, wanga na mafuta mengi ambayo huwa chakula cha bakteria wa ngozi na kusababisha harufu mbaya na kali.
Ulaji wa vyakula vyenye amila nyingi, vilivyokaangwa, vyakula vyenye upungufu wa viini lishe vya madini hasa magnesium na zinc pamoja na hali ya kutopata choo kama kawaida vilevile kunachangia ukubwa wa tatizo la harufu mbaya ya mwili. Hali ya kutokupata choo vizuri husababisha sumu nyingi kubakia mwilini na kutoka kwa njia ya jasho, ambalo hutoa harufu mbaya.
Jinsi ya kukabiliana na tatizo la harufu mbaya ya mwili
• Vaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa kitambaa cha pamba zinazonyonya jasho kwa urahisi.• Kunywa maji mengi na maji ya matunda kwa wingi kila siku.
• Badilisha nguo, chupi na soksi kila siku, ikiwezekana badilisha mara kwa mara.
• Hakikisha nywele za kwapani na sehemu za siri zinakuwa fupi kadri inavyowezekana wakati wote.
• Oga mara kwa mara na tumia dawa ya Aloe vera ya kupaka kwapani. Epuka vipodozi vyenye harufu kali.
2. Harufu mbaya mdomoni:
Tatizo la harufu mbaya mdomoni linaweza kuwa na uhusiano wa karibu na kuzaliana kwa wingi kwa bakteria ndani ya mdomo, kuoza kwa meno, uvimbe wa fizi, mapengo au matundu kwenye meno ambayo hung’ang’ania mabaki ya chakula kwa muda mrefu. Matatizo ya afya mbaya ya kinywa yanaweza kusababisha tatizo hili kwa takribani asilimia tisini[90%]Tatizo hili pia linaweza kusababishwa na utendaji mbaya au wa polepole wa mfuko wa chakula tumboni au utendaji mbovu wa utumbo mwembamba. Uambukizo wa bakteria kooni au puani, vidonda vya tumbo, ugonjwa wa figo, ugonjwa wa ini, ugonjwa wa kisukari au minyoo tumboni pia yanaweza kusababisha tatizo hili.
Jinsi ya kudhibiti tatizo hili
• Kunywa maji mengi na juice ya matunda kwa wingi kila siku.• Safisha kinywa mara tatu kwa siku hasa kila baada ya kula chakula chochote. Safisha ulimi, meno na fizi kwa uangalifu. Tumia dawa ya meno yenye dawa asilia ya aloevera au maji ya chumvi kidogo. Sukutua koo mara kwa mara kwa maji ya uvuguvugu yaliyoongezwa chumvi kidogo.
• Ziba meno yote yaliotoboka au tumia dawa aina ya ‘hydrogen peroxide mouth wash’ kila siku kwa ajili ya kusukutua mdomoni.
• Usile nyama nyingi, sukari nyingi, vyakula vyenye mafuta mengi, mayai au maziwa kwa wingi. Epuka vinywaji vyenye kaffein. Kula karoti na matofaa (apples) kwa wingi pamoja na kunywa juice ya papai, chungwa au nanasi. Kula maboga na asali pia vinasaidia.
• Tumia dawa aina ya vitamin B-complex na vitamin C, epuka matumizi ya dawa zinazokausha mate kama vile dawa zinazosababisha kukojoa sana (diuretics) na dawa zinazotibu au kupunguza mzio kama vile piriton (Chlorphenamine maleate) au ephedrin.
Tatizo la kula vitu ambavyo si chakula
Hili ni tatizo la kupenda kula vitu ambavyo si chakula kama vile udongo, sabuni, mkaa, chaki, karatasi, kucha, majivu na vitu vingine. Mtu yeyote anapotamani kula au kula kabisa vitu hivi kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja endapo umri wake ni zaidi ya miezi 24 (miaka miwili) ni wazi kuwa ana tatizo la ugonjwa ujulikanao kitabibu kama ‘PICA’.Ugonjwa huu huwapata sana wanawake na wasichana hasa pale wanapokuwa wajawazito. Kula udongo na vitu vingine ambavyo si chakula kunaweza kusababisha madhara ya kiafya kutokana na ukweli kuwa udongo unaweza kuwa na sumu za dawa za mimea na mbolea. Sumu kama lead, dioxin na madini mengine yenye hatari yanayopatikana kwenye udongo uliochafuliwa, husababisha matatizo ya kiafya.
Tabia hii ya kula vitu ambavyo si chakula imekuwa ni chanzo cha magonjwa kama vile saratani ya tumbo, minyoo na madhara ya kiafya yatokanayo na kuharibika kwa ini. Watu wanaokula vitu hivi hukabiliwa na tatizo la kujaa kwa tumbo na kuvimba, kutopata choo na tumbo kuuma kwa siku nyingi bila sababu bayana. Mara nyingi udongo huchafuliwa kwa vinyesi na mikojo ya binadamu, ndege na wanyama kama mbwa nk, hii husababisha udongo kubeba vimelea vya magonjwa.
Kwa nini wasichana wengi hupata tatizo hili
Wasichana wengi wanaokula vitu ambavyo si chakula hukabiliwa na tatizo la upungufu wa madini chuma na zinc mwilini. Hii ni kutokana na lishe duni au kupoteza damu nyingi wakati wa hedhi au upungufu wa madini chuma kutokana ugonjwa wa minyoo ya safura. Ulaji mbaya kama vile kunywa chai yenye majani ya chai au kahawa wakati wa kula huzuia madini ya chuma kufyonzwa au kusharabiwa na kuingia mwilini. Upungufu wa dawa ya kuyeyusha chakula tumboni (hydrochloric acid) pia husababisha tatizo hili.Tatizo la kula vitu ambavyo si chakula pia huusishwa na magonjwa ya akili hasa kwa watoto wadogo. Kwa akina mama watu wazima tatizo hili pia linaweza kusababishwa na kutokwa jasho jingi kila siku. Jasho jingi hupoteza takribani gram 15 za madini chuma mwilini kwa kipindi cha mwezi mmoja. Vyanzo vingine vya upoteaji wa madini chuma mwilini ni kupotea kwa damu muda mrefu na kidogo kidogo wakati wa hedhi isiyo na mpangilio, saratani ya mji wa kizazi, malaria sugu, kichocho, bawasili (haemorrhoid), kuharisha damu na vidonda vya tumbo. Mimba za mara kwa mara na kunyonyesha pia hupoteza madini ya chuma mwilini. Inakadiliwa kuwa mwanamke anayejifungua inamchukua miaka miwili kurejesha gram moja ya madini chuma yaliyopotea toka mwilini wakati wa kujifungua na kunyonyesha. Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa wasichana wanaopata mimba katika umri mdogo.
Jinsi ya kudhibiti tatizo hili
• Kula vyakula vyenye madini chuma na zinc kwa wingi kama vile maharage, korosho, mboga za majani hasa spinach, mayai, nyama, samaki, mbegu za maboga na matunda.• Kutibu minyoo kwa kumeza dawa za minyoo angalau mara moja kwa mwezi.
• Kunywa juice ya spinach na karoti bilauli moja kutwa mara tatu kila siku. Kunywa supu ya mbogamboga na mchele.
• Usinywe vinywaji vyenye caffeine wakati wa kula chakula.
• Meza dawa zinazoongeza madini chuma mwilini kama vile ferrous sulfate nk.
• Safisha misumali kwa maji moto, iloweke kwenye maji ya limao kisha tengeneza juice kwa maji haya na unywe mara kwa mara au pika chakula kwa kutumia sufuria ya chuma.
Chagua kiongozi bora ili kuleta mabadiliko
0 comments:
Post a Comment