Suala la muhula wa Tatu limekuwa mwiba kwa baadhi ya marais hususani Barani Afrika kutokana na viongozi hao kuwa na tamaa ya kutaka kuendelea kuongoza nchi zao licha ya kuwa katiba katika nchi hizo ikiruhusu mihula miwili pekee.
Nchi zilizokumbwa na viongozi wake kupingana na katiba kwa kutaka kujiongezea muhula wa tatu ni Burundi ambapo machafuko yametokea na kusababisha mamia ya wananchi kuomba hifadhi Tanzania, Suala hilo limechipuka tena nchini Congo-
Brazzaville ambapo Rais wa taifa hilo Denis Sassou Nguesso ametangaza kuwa taifa hilo litaanda kura ya maamuzi kuamua iwapo ataruhusiwa kuwania kwa muhula wa tatu.
Suala la iwapo marais wanafaa kuruhusiwa kuwania kwa muhula wa tatu katika nchi ambazo katiba inasema kiongozi anafaa kuwa madarakani kwa mihula miwili pekee linazidi kuchipuka katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Nchini Tanzania, Rais Jakaya Kikwete amepongezwa na mataifa mbalimbali duniani kwa uamuzi wake wa kuruhusu kufanyika uchaguzi mkuu kufuatia muda wake wa kukaa madarakani kukaribia mwisho ambapo anatarajiwa kuondoka madarakani oktoba,25, 2015 ambapo uchaguzi mkuu wa rais wabunge pamoja na madiwani utafanyika.
Pongezi za Rais Jakaya Kikwete kukubali kuachia madaraka zimetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mhe. Anthony J. Blinken ambaye amemwambia Rais Kikwete kuwa uamuzi wake wa kuheshimu Katiba ya Tanzania kwa kukabidhi madaraka ya uongozi wa nchi baada ya kumaliza vipindi viwili vya uongozi wake, unatuma ujumbe mzito, dhahiri na unaosikika sana katika Bara zima la Afrika na Kanda ambako Tanzania ipo.
Naye Mheshimiwa Ken Wallack, Rais wa Taasisi ya National Democratic Institute (NDI) ya chama cha siasa cha Democratic amemwambia Rais Kikwete: “Tuseme hivi kwa kutilia maanani yanayotokea katika dunia ambako unaishi na unatokea, sote tunakushukuru na kukupongeza kwa msimamo wako wa kuheshimu Katiba ya nchi yako
Mheshimiwa Balozi Mark Green, Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) ya chama cha siasa cha Republican amemwambia Rais Kikwete, ”unaacha mfano kwetu sisi sote katika kupigania na kulea demokrasia duniani na hasa katika Bara la Afrika.
Mwingine ni aliyekuwa waziri mdogo wa Mambo ya Nje Marekani aliyeshughulikia masuala ya Afrika, Mheshimiwa Johnnie Carson amemwambia Rais Kikwete: Chini ya uongozi wako, Tanzania imeendelea kuonyesha mfano usiokuwa na kifani katika ujenzi wa demokrasia na umeheshimu sana Katiba ya nchi yako. Sisi katika Marekani, tunakupongeza sana.”
Licha ya Marais kutaka kujiongea madaraka,suala la marais kukaaa madarakani muda mrefu limezidi kuota mizizi katika nchi mbalimbali barani Afrika. Hawa ndio viongozi waliokaaa madarakani kwa muda mrefu zaidi,
Miaka 36: Teodoro Obiang Nguema Mbasogo – Equatorial Guinea, alichukua madaraka kupitia mapinduzi ya serikali mwaka Agosti 1979
Miaka 36: Jose Eduardo dos Santos – Angola, alichukua uongozi baada ya kifo cha rais wa kwanza wa taifa hilo Agostinho Neto Septemba 1979
Miaka 35: Robert Mugabe – Zimbabwe, alishinda uchaguzi wakati wa kujinyakulia uhuru kwa taifa hilo Aprili 1980
Miaka 32: Paul Biya – Cameroon, alichukua uongozi baada ya kujiuzulu kwa rais wa kwanza wa nchi hiyo Ahmadou Ahidjo, Novemba 1982 Miaka 30: Denis Sassou Nguesso – Congo, aliwekwa uongozini na jeshi mwezi Oktoba 1979 na akaongoza hadi mwezi Agosti 1992. Alirejea tena Oktoba 1997 na kuendelea hadi sasa.
Miaka 29: Yoweri Museveni – Uganda, alichukua uongozi rais baada ya kundi lake la waasi kuchukua madaraka mwezi Januari 1986.
Ni dhahiri viongozi wengine barani Afrika wakajifunza kutoka nchini Tanzania kwa kuwa ni moja ya nchi inayofuata misingi ya Demokrasia kwa kiongozi wake mkubwa ambaye ni Rais kukubali kuachia madaraka kwa kuitisha uchaguzi mkuu, kwani siasa ya kuachiana madaraka ndiyo inayopeleka mbele gurudumu la maendeleo kwa kuruhusu fikra mpya, mawazo mapya kwa kumpa ridhaa kiongozi mwingine.
Chagua kiongozi bora ili kuleta mabadiliko
Blogger Comment
Facebook Comment