Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Kamati ya Siasa Mkoa wa Arusha, Francis Ikayo, amejiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mwanasiasa huyo aliyekuwa mmoja wa wana CCM waliowania uteuzi wa kuwania ubunge Jimbo la Longido mwaka 2010 na kuangushwa na Mbunge wa sasa Lekelu Laizer, alijiunga Chadema jana, akitaja sababu kuu tatu zilizomfanya kuchukua uamuzi huo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Namanga, mpakani mwa Kenya na Tanzania, muda mfupi baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Ikayo alisema amevutiwa na mikakati ya chama hicho ya kutetea haki za wanyonge.
“Nina sababu kuu tatu za kuhamia Chadema. Mosi ni kwa sababu chama hiki kimejipambanua kuwa watetezi wa wanyonge, pili kuna uhuru na demokrasia ya kila mtu mwenye uwezo kugombea bila kuwekewa mizengwe na tatu kinapiga vita rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya mali na fedha za umma,” alisema Ikayo.
Wazee watatu kutoka jamii ya wafugaji wa Kimasai anakotoka Ikayo, Lekishoo Loodo, Moi Lesingo na Laidinga Nangoro, walimkabidhi rungu na usinga mwanachama huyo mpya wa Chadema, ikiwa ni ishara ya kukabidhiwa majukumu ya Kiuongozi.
Akihutubia mkutano huo, Ikayo aliitaka jamii ya wafugaji kuamka na kuacha kuwa mtaji wa ushindi wa CCM nyakati za uchaguzi, kwa kile alichoeleza chama hicho kimewatelekeza kwa kuruhusu maeneo ya malisho kuvamiwa, huku wafugaji wakilazimika kuhangaika na mifugo yao kutafuta malisho.
Kwa upande wake, Lema aliwataka watu wote wenye umri na sifa za kujiandikisha kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura, ili kupata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Jashua Nassari aliwaomba wachungaji, maaskofu na masheikh kote nchini, kuacha kupokea fedha haramu zinazotokana na wizi wa fedha na mali za umma zinazotolewa makanisani na misikitini na wasaka madaraka.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment