Wakulima wa korosho waliokusanyika kusikiliza hatma ya malipo yao Kibiti, Pwani
Wakulima wa Korosho Mkoa wa Pwani wamelalamikia kutolipwa kwa wakati baada ya kufanyika mnada wa zao hilo na kwamba wamekuwa wakipigwa danadana kuhusu malipo yao hali inayowakosesha amani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakulima hao wamesema, zao hilo limekuwa likinunuliwa na matajiri ambao hawalipi fedha kwa wakati na hivyo kuwasababishia maisha magumu.
Aidha wameilalamikia serikali kwa kutofuatilia malalamiko yao na kuahidi kuwa iwapo watapata wasaa wa kukutana na waziri mkuu itabidi wamweleze matatizo yao ya kulipwa kwa wakati.
Naye Meneja wa Bodi ya Korosho, Mangire Maregesi akijibu malalamiko hayo amesema, kuanzia msimu ujao mwakani, wakulima wa korosho Mkoa wa Pwani watatakiwa kutekeleza mfumo stahiki wa Stakabadhi ghalani, sambamba na kuvitaka vyama vya msingi kuchukua jukumu la kukusanya korosho kutoka kwa wakulima.
Aidha amesema, mara baada ya kukusanywa kwa korosho hizo zipelekwa kwenye ghala kwani katika ghala hizo kuna mwendesha ghala na vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia na kuboresha korosho hizo.
Meneja huyo amewataka wakulima hao wa Korosho mkoani Pwani kuiga mfano wa wenzao wa Kusini na Ruvuma ambao hutunza vyema korosho vyao, na kuongeza kuwa ni wazi kwa msimu huu wakulima hao watapata hasara kutokana na utunzaji mbovu wa korosho hizo ambazo zitashuka ubora.
Hadi sasa wakazi hao ambao wako katika mnada wa mauzo wa tatu bado hawajalipwa fedha zao za awali na hivyo kutaka majibu sahihi kutokan kwa mamlaka husika.
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment