Gari inaondolewa eneo hilo huku kundi dogo la watu waliokuwa wamenijalia ninawaona wananicheka bila kufahamu mwenzao nimetingwa na jambo gani.
Ninamtazama dereva wa gari ninavuta kumbukumbu usoni mwake, lakini sikumbuki kabisa kama nimemuona wapi mtu huyu. Yeye amenyamaza kimya anatia gia tu hana habari na mie. Ninataka kumsemesha mara moyo wangu unapatwa na mstuko, nyuma ya kiti nilichokaa ninasikia sauti ikinisemesha.
“Dobe hatimae leo tumekutana tena!”
Ninaugeuza uso wangu nyuma kwa haraka, ninamuona mtu alienisemesha akiwa anatabasamu! Mwili wangu unaingiwa na baridi ya ghafla!
13
Unaingiwa na baridi kwa kuwa mtu ninaemuona katika gari hii, nilimkimbia akiwa mjamzito nami wakati huo sikuwa na kazi nikalala mbele. Sasa leo ninamuona tena ishapita miaka saba nyuma, moyo wangu unaingia baridi kabisa.
“Dobe umekuwa hivyo sasa, unatembea na Khanga tu mitaani umepatwa na jambo gani?”
Anaponiuliza swali hilo ninaona vibaya kumueleza kilichonisibu, lakini bado ninakumbuka namna alivyokuwa akinambia ana mimba yangu siku hizo, na mie nikawa ninamsisitiza aitoe, lakini yeye akataka nimpe pesa ili akaitoe hiyo mimba, ila kwa kuwa sikuwa na pesa nikatimkia Dar es salaam, nikimuacha yeye katika mkoa wa Tabora. nilipokuwa naishi miaka saba iliyopita.
“Tatu Matabane, nisamehe sana kwa yote yaliyopita, maisha yashanipiga wangu, naomba radhi kwa yaliyotokea.”
Ninamwambia anisamehe kwani ninamuona sasa hivi yupo vizuri sana.
“Dobe uliponikimbia ulidhani nitaaibika na kufadhaika, lakini mungu analipa hapahapa duniani, leo ninakuona mitaani ukiwa katika hali hii kweli? Wewe Dobe ninaekujua mwenye damu ya nguo unaejua kuvaa, wakuvaa Khanga tu kweli?! Tena upande mmoja”
Tatu Matabane ananambia maneno hayo ninajiuliza mara mbili nimwambie au niuchune ninaona labda kisisema anaweza kunipa msaada wakunifikisha kwangu. Ninapojiuliza sana ninaiona gari ikipinda kulia Tabata Bima, inaelekea Tabata Liwiti.
“Mie ninakaa Tabata Segerea ndipo ninapoishi sasa, madhila ya Dunia yamenifikisha hapa nilipo, ninaomba msaada wako Tatu.”
Ninapomueleza maneno hayo, Tatu anaangua kicheko kikubwa, kisha ananiuliza kwa dhihaka!
“Unataka nikusaidieje dobe?”
Ninamueleza ninachokihitaji kwake kwa sasa. “Kwanza unifikishe Segerea nikavae nguo zangu, lakini pia uni……..!”
“….Ukavae?!”
Sijamaliza kauli yangu, Tatu ananiingilia kati mazungumzo yangu. Anaponiona sina jibu lakumpa, anaendelea.
“Inamaana nguo unazo, ila umetembea na Khanga moja? Hivi wewe Dobe upo sawa kweli?! Maana sikuelewi.”
“ Naam nipo sawa”
Lakini katika hali ya kawaida bado siwezi kwa hali niliyonayo kumridhisha mtu kuwa sina matatizo.
“Haya kama upo sawa, kwa nini uvae Khanga moja mtoto wa kiume, kisha utembee mitaani kule Mawenzi, na wewe unakaa Segerea?”
Hapo Tatu ananibana ninabaki kimya tu sina jibu lakumwambia.
“K,K. Twende Segerea mwaya. Huyu bwana sitomsahau katika maisha yangu, amenifungua bikira yangu, akanionesha utamu wa Sexy upoje, nilimpenda zaidi ya sana, lakini alichonitenda nimekuwa siwaamini tena wanaume. Kwani wanaume wanakupenda ukiwa huna tatizo, ila ukipata tatizo, tena wakati mwengine, walilolisababisha ni wao wenyewe wanakukimbia. Yaani nimelea mimba peke yangu miezi tisa, wazazi nao wakanifukuza kwa vile nimepata mimba isiyokuwa na baba, wakiniambia kuwa nimeitia aibu familia yetu. Hivyo nikawa ninaishi mapamba nje pamoja na mtoto wangu. Miaka saba leo ndiyo ninamuona bwana huyu akiwa na upande wa Khanga, eee Mungu asante kwa kunilipa mtoto wa Matabane.”
Tatu anaposema hivyo machozi yananilengalenga sana.
“Mwanangu yupo wapi tatu?”
Ninamuuliza kwa uchungu kwani ninaona sitoweza tena kupata mtoto ikiwa kweli nimeshaathirika kwani mtoto huyo nitakuja kumpa mateso ya bure tu. Tatu Matabane anaangua kicheko kikubwa kwa mie kumuuliza mtoto wangu.
“Hehee, Kanchomeke!!! Kantangazee imepitwa na wakati babu eee?!!! Dobe leo unamuuliza mtoto wewe, wapiii ushayatupa! mtoto wangu uliemkataa amechukuliwa na mzungu anaishi Ulaya, kwa watu wanaojua kuthamini na kulea, mie nimekuja Africa nina mwezi sasa, tunataka kuwekeza hapa ndiyo nilikuwa nafatilia masuala ya Ardhi na kwa kuwa mie ndiyo mzawa wa nchi hii, Mzungu atawekeza kwa jina langu na mwanangu, tukiwa tunafanya pamoja nae. Mungu hamtupi mja wake, na baada ya dhiki faraja!”
Hakika Moyo wangu, uso wangu vyote vinatahayari kwa majibu hayo.
“Basi Tatu ninaomba ajira mwenzio nimepigika maisha yangu yameingia husda na hasada, sina mbele wala nyuma yaani Mungu amenichapa bakora mbaya, ninadhani ni dua zako mbaya Tatu, nisamehe Mzazi mwenzangu.”
“Mie nishakusamehe bure wewe kitambo ila sitakusahau, ndiyo maana leo hii ninatoka kwa shoga yangu huyu Tabata Kimanga, nikakuona nikamwambia Kudrat Kenny au KK asimame ili nihakikishe kama ndiyo wewe Dobe ninaekufahamu au siyo.”
Wakati huu, huyu dada anaeiendesha hii gari niliemfahamu kwa jina la Kudrat Kenny au KK, alikuwa yupo Sanene tunaelekea Segerea.
“Ninaomba nijue tu basi, mwanangu anaitwa nani au ungenionesha japo picha yake tu.”
Ninamwambia huku nikitia huruma sana kwani sasa Tatu ni mambo safi na mie ndiyo choka mbaya sana majalala ya chokoraa!
“Dobe wewe huna mtoto wala sitokuonesha hata picha zake, na kwa taarifa yako tu ni kwamba, huyo mzungu niliempata amemfanya mwanangu kuwa ndiyo mwanae, hivyo hata mwanangu anatambua baba yake ni huyo mzungu, hivyo wewe huna chako Dobe kama ulivyomkataa akiwa tumboni. Tena hili ndilo litakuwa fundisho kwako na kwa wanaume wenzako wanaokataa mimba kisha wanataka watoto”.
Kudrat anafika kituo cha kiitwacho kwa Bibi anapinda kona kisha ananiuliza.
“Segerea ipi unayokwenda?”
“Pale Sheli utapinda kulia kisha ukishafika pale kituoni, utapinda kushoto hadi katika msikiti, kwenye ukuta wa msikiti utapinda kulia unanyoosha hadi utatokea nyumbani kwangu.”
Ninapomwambia hivyo Kudrat Kenny, au KK anatikisa kichwa kuonesha ameelewa nilivyomuelekeza, anakanyaga mafuta hadi Sheli anapinda kulia anapofika kituoni Segerea mwisho wa mabasi anapinda kushoto, ananyoosha hadi msikitini anapinda kulia ananyoosha ninamuelekeza nyumba ninayokaa anaegesha gari hapo, ninaiona nyumba ninayokaa imefungwa mlango.
“Hapa ndipo nilipopanga, karibuni sana pia asanteni sana kwa msaada.”
Ninawashukuru huku nikishuka kuelekea mlangoni ninaujaribu mlango ninauona umefungwa. Ninagonga mara kadhaa lakini sipati jibu.
“Dobe kwa heri eee”
Tatu Matabane ananiambia ameshusha kioo, kisha ninamsikia anamwambie KK atoe gari waondoke wakawahi mishe zao. KK anatia gia wanaondoka nami ninabaki peke yangu na Khanga yangu maungoni.
Ninavuta subira labda Baby atatoka hospitali ili aje afungue mlango lakini muda unazidi kuyoyoma. Watu nao kwa umbea wamejaa mabarazani mwao, wananishangaa utasema nimefanya kituko gani sijui. Ingawa majirani wote wanadhani nimeachiwa Polisi. Isipokuwa hakuna hata mtu mmoja, si mwanamke wala mwanaume aliekuja kutaka kujua hali yangu au kilichonisibu zaidi ya kunitazama tu. Sasa ninachanganyikiwa vibaya itakuwa vipi kama Baby akilazwa asirudi nyumbani nitakuwa mgeni wa nani mie?
Ninaendelea kusubiri kwa muda mara ninaiona gari ikija katika nyumba nilipo inafunga breki mlangoni. Wanashuka wanawake wawili, huku wakiwa na haraka mmoja ninamuona anatoa ufunguo na kufungua mlango. Ninaipata faraja kwa kuweza japo kuingia ndani ili nichukue simu yangu niweze kuwa na mawasiliano, lakini pia nivae nguo badala ya kukaa na Khanga. Ninapiga hatua kadhaa ninawakaribia hawa wanawake ambao sasa wameshaufungua mlango wanaingia ndani. Ninamuona dada mmoja anaruka na kuogopa mara anaponiona ameshituka sana. Bila shaka namna nilivyo anadhani labda mie ni punguani.
“Pole sana dada kwa kukushitua mie ni mpangaji katika nyumba hii.”
Ninajitambulisha kwao ili wasiwe na wasiwasi na mie.
“Makubwa haya, Marehemu Mwanamtama alipangisha hadi wendawazimu?!”
Ninamshangaa sana huyu dada siyo kwa kunifananisha na mwendawazimu, hasha wa kala. Bali anapomtaja Mwanamtama kuwa ni marehemu ananifanya niishiwe pozi kabisa.
“Eti umesema mwanamtama ni Marehemu?!!!”
Ninapouliza swali hili, wananishangaa sana kwani bado sijawaridhisha kuwa mie siyo mwehu.
“Wewe Mwanamtama unamjua?!”
Swali hilo lenye kushangaza ndani yake, linadhihirisha dhahiri shahiri kuwa mie ninahisiwa kuwa ni punguani kamili.
“Sasa nisimfahamu vipi wakati nimewaambia kuwa mie ni mpangaji wake. Basi labda kwa faida yenu tu, mie pia ndiyo baba mwenye nyumba hii.”
Ninaposema maneno hayo, ninawaona hawa madada wanatizamana, kisha wanatoka nje mbio huku wakiogopa sana. Ninapowafata nje ili niwafahamishe zaidi wao ndiyo wanazidi kuchimba mbio! Yaani ninachogundua ni kule kumtangaza Mwanamtama kuwa ni mtu wangu na kuwa baba mwenye nyumba wao ndiyo wakapigia mstari jibu lao kuwa mie hasa ni Chizi Majuzubu.
Ninarudi ndani kwani nimepasubiri kwa muda mrefu sana, ili nikavae nguo. Ninaelekea chumbani kwangu ninavaa tayari, kisha ninachukua simu yangu ninaiwasha mara inaingia ujumbe mfululizo. Ninazitazama kwa haraka haraka zile meseji, mara ninaiona iliyotumwa karibuni ni ya meneja. Ninaifungua na kuisoma kwa wahaka mkubwa.
“Dobe nilikuahidi kuwa nitafanya, na nimefanikiwa kufanya. Haya sasa tuone utakaa wapi?!”
Ninairejea kuisoma mara kadhaa, lakini bado ninaielewa katika maana ile ile tu si nyinginezo. Nikiwa nimeshangaa, mara ninasikia sauti za watu wanaume zikiingia ndani huku wakizungumza.
“Nyie nae, mwehu mwenyewe yupo wapi?”
Ninatoka sebuleni ninawakuta jamaa wananisalimia na kunihabarisha.
“Habari yako ndugu. Wewe ni mpangaji humu ndani?”
Ninaitika kwa kichwa kuashiria kukubali.
“Sawa. Naomba pokea taarifa kwamba, mwenye nyumba hii, wakati huu tunapozungumza na wewe, ni nusu saa tu imepita tangu roho yake imeacha mwili wake! Yaani Mwanamtama amefariki Dunia. Sie ni ndugu zake tumekuja kufunga chumba chake, msiba na taratibu za mazishi zitafanyika kwa mdogo wake Ilala”
Kwa taarifa hiyo, ninapatwa na ganzi mwili mzima yaani Baby ninamuona mbele ya macho yangu akinipa Matentelee. Baby akinipikia vyakula na kunipa maana zake, Baby akinibeba ananilaza kitandani kwake, Baby akiniahidi kuwa ataishi na mie hadi kifo kitutenganishe ni kweli imekuwa!
Dah Baby Girl, umezimika kama mshumaa?! Oooo Baby ninaumia sana moyoni mwangu kwa kuondoka kwako ghafla. Baby ningeishi na wewe japo umeathirika mpenzi. Hakika umenionesha mapenzi ya dhati, hukujali tofauti kubwa ya umri wetu. Baby kumbe pale kitandani leo ninakuinua mkono wako unaurudisha chini, ndiyo tulikuwa tunaagana? Nisamehe Baby, hakika nimesababisha kifo chako. Siwezi kuishi tena bila wewe Baby. Nge hakukuua nakataa, ila umeuliwa na mwanadamu Baby. Leo nilikuwa nawe asubuhi, muda huu umekuwa maiti?! Ama kweli akhera hakupo mbali.
Mawazo hayo yanapita moyoni mwangu donge limenikaba rohoni. Machozi yananibubujika bila kujizuwia. Mwili wangu unakosa nguvu kabisa ya kuhimili kiwili wili changu, miguu inatepeta ninashindwa kujizuwia. Kichwa kinakuwa kizito, macho yanapoteza nuru ya kuona, ninaanguka mweleka chini, nashindwa kujizuwia ninapoteza fahamu!!!
UCHUNGU MKUBWA UNAMPATA DOBE. AMA HAKIKA KUONDOKEWA KUBAYA, HASA NA UMPENDAE. NINI KITAENDELEA? USIKOSE KUSOMA CHOMBEZO HILI NAMBA MOJA, MBILI, TATU, NA NNE MITANDAONI. KESHO KATIKA MUDA WAKE BILA KUCHELEWA HATA SEKUNDE MOJA!
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment