CHOMBEZO; HEHEEE, KANTANGAZEEE!!! SEHEMU YA 20



Dah Baby Girl, umezimika kama mshumaa?! Oooo Baby ninaumia sana moyoni mwangu kwa kuondoka kwako ghafla. Baby ningeishi na wewe japo umeathirika mpenzi. Hakika umenionesha mapenzi ya dhati, hukujali tofauti kubwa ya umri wetu. Baby kumbe pale kitandani leo ninakuinua mkono wako unaurudisha chini, ndiyo tulikuwa tunaagana? Nisamehe Baby, hakika nimesababisha kifo chako. Siwezi kuishi tena bila wewe Baby. Nge hakukuua nakataa, ila umeuliwa na mwanadamu Baby. Leo nilikuwa nawe asubuhi, muda huu umekuwa maiti?! Ama kweli akhera hakupo mbali.
Mawazo hayo yanapita moyoni mwangu donge limenikaba rohoni. Machozi yananibubujika bila kujizuwia. Mwili wangu unakosa nguvu kabisa ya kuhimili kiwili wili changu, miguu inatepeta ninashindwa kujizuwia. Kichwa kinakuwa kizito, macho yanapoteza nuru ya kuona, ninaanguka mweleka chini, nashindwa kujizuwia ninapoteza fahamu!!!
Ninafumbua macho yangu, ninashangaa nipo kitandani nimelala. Ninajaribu kuvuta hisia mahala nilipo, ninashindwa kung’amua mara moja kuwa nipo wapi na kwa nini.
Ninainua mkono wangu ninauona mzito. Ninautazama kwa nini mzito, ninauona mpira mwembamba ukiwa katika mkono wangu wa shoto! Ninautazama vizuri ninaiona sindano imeuchoma mkono. Ninaufatilia huu mpira ninauona umeelekea juu. Ninainua macho yangu kuutazama ulipoendea, ninauona ulipoishia kuna Dripu ikiingia mwilini mwangu! Ninapata wasiwasi Dripu tena, ninaangaza huku na kule, ninaviona vitanda vingine vikiwa na watu wamelala. Ninawatizama kwa makini ninayaona maandishi meusi katika shuka nyeupe yanasomeka AMANA HOSPITAL. Ninajiuliza ina maana mie nipo hospitali?! Ninavuta hisia imekuwaje hadi niwe hapa, ninakihisi kichwa changu kinauma na kinakuwa kizito!
Ninatulia sijui nifanye nini uzito kwa kichwa changu unazidi kunielemea. Nikiwa nimelala ninamuona mtu anasogelea katika kitanda changu. Ninamtazama kwa makini ninamuona ananikenulia meno yake anatabasamu.
Ninamtazama bila kumsemesha ingawa sura yake siyo ngeni usoni mwangu. Ila kumbukumbu zangu ni chenga tupu.
“Pole Dobe, nimekupigia simu yako imepokelewa na mtu mwengine amenambia umeanguka unapelekwa Amana Hospitali ndiyo nikangoja muda wa kuwaona wagonjwa saa kumi hii jioni, nimekuja kukutazama pole sana.”
Ninamtazama kwa makini na sauti yake ninaiingiza katika mizani yangu ya akili ninaiona kama nimeshaongea nayo kabla ya leo.
“Wewe ni nani kwani na nani alikupa namba yangu ya simu?!”
Ninamuuliza nikimtazama usoni kwake. Ninamuona anatabasamu kijinga.
“Ama kweli Dobe umeumia, hivi ni kweli mie umenisahau?! Inaonesha wewe umeangukia kichwa kwani usingeweza kunisahau hivihivi tu. Namba ya simu umenipa wewe mwenyewe!”
Majibu yake hayo ninavuta tafakari lakini sikumbuki kama nimempa namba yangu.
“Wapi nilipokupa namba yangu wewe?”
Ninamuuliza kwa hamaki lakini ananituliza kwa mkono wake na kisha ananambia kwa utuo.
“Pole sana Dobe utapona tu usijali, mie ninakwenda kulipia matibabu yako kisha niwaulize madakitari kama wanaweza kukuruhusu, ikiwa utaruhusiwa basi tutakwenda sote nyumbani kwangu, sawa Dobe?”
Ninabung’aa tu ninatoa macho sijui nimjibu nini kwani, simkumbuki, kichwa changu kinazidi kuwa kizito sasa ninasikia kama muungurumo ndani ya kichwa.
Ninamtafakari mtu huyu anaponambia akanilipie huduma za matibabu, anazidi kuniumiza kichwa. Ninamuona anaondoka nami ninamtizama kwa nyuma, hadi anaingia katika chumba.
Ninatazama kule ndani ya chumba nikiwa hapa nilipo, ninamuona yule mgeni akizungumza na watu waliovaa nguo nyeupe, wakioneshea kidole kwangu. Mara ninamuona mwanaume mmoja kutoka katika chumba kile akinijia hadi kitandani.
Muungurumo kichwani kwangu na upepo mwingi ninauhisi ukitembea kutoka upande mmoja kwenda mwengine!
“Unaendeleaje sasa hivi?”
Ananiuliza huyu mtu alietoka kwa wenzake.
“Niendelee nini wakati mie ninataka kuwahi kazini kwangu mnanichelewesha tu hapa, hebu kaniwashie mashine yangu nimpe huduma Baby Girl Mwanamtama, yupo hapo ananisubiri!!!”
Ninaposema maneno hayo ninamuona huyu mtu alievaa nguo nyeupe ananikazia macho.
“Mbona unanitisha wewe, mie pia dereva ujue kama wewe vile, unabisha nikuwekee gia sasa hivi?! Mwambie Baby Girl Mwanamtama apande mbele wewe ukae nyuma niwapeleke beach mkapunge upepo!!!”
Kila nikizungumza, ninamuona huyu bwana ananishangaa. Atatingisha kichwa chake kwa masikitiko!
Na mie ninamuigiza kwa kutikisa kichwa changu kama yeye! Ninapofanya hivyo ninamuona huyooo anageuza alipotoka huku akisikitika.
Mara baada ya muda kidogo ninamuona ananijia akiwa ameongozana na wenzake waliovaa nguo nyeupe.
“Dobe hujambo mpenzi wangu?”
Mwanamke mmoja ambae amevalia nguo nyeupe na kikofia kidogo cheupe juu ya kichwa chake ananiuliza.
Kabla sijamjibu ninatabasamu kwa sauti kubwa.
“Karibu tule chakula, kisha umpe na Baby Mwanamtama nae ale.”
Mara ninawaona wakitazamana kisha wakiinua vichwa vyao juu chini kwa pamoja. Nami ninawaigiza pia huku ninacheka sana!
Mara ninawaona wananikamata, kisha huyu mwanaume ananichoma na kitu chenye ncha kali.
“Huyu bado amechanganyikiwa kwa dawa na maumivu ya kichwa. Kwa hiyo bado anachanganya habari, sindano hii itakwenda hadi kwenye ubongo. Atakaa sawa taratibu, fahamu zake zitamrejea.”
Ninayahisi maumivu makali sana, mwili unanilegea, nguvu zinanishia kwa haraka. Kiza kinatanda machoni.
SAA TATU BAADAE.

Ninainuka kitandani ninakaa kitako kitandani huku mwili wangu ukiniuma sana. Ananijia mtu mbele yangu nisiemfahamu.
“Vipi Dobe hujambo?”
“Sijambo nasikia njaa sana, na kichwa nakisikia kizito sana, kwani kimetokea nini?!”
Ninamuona huyu mtu anatikisa kichwa kisha anatabasamu.
“Pole sana Dobe, kwani hakika ulikuwa ni mwehu saa tatu zilizopita. Hapa upo Hospitali Amana, mie ni Daktari Mwaky Shola. Uliletwa hapa ukiwa umeangukia kichwa sehemu ya kichogo, hivyo MEDULA OBLANGATA ilicheza kidogo. Ulianguka mara baada ya kupewa habari za msiba, hii ni kwa mujibu wa watu waliokuleta hapa walivyoeleza.”
Ninamtazama kwa makini huyu bwana, hakika ninamuona amevaa mavazi ya utabibu meupe mwilini mwake. Vifaa vya kupimia mapigo ya moyo, vikining’inia kifuani mwake.
“Dokta umesema msiba, msiba, msibaaa, aaaagh Baby Girl hapana usife mpenzi, bado ninakuhitaji mpenzi. Siamini kama umeniacha hivi”
Kumbukumbu zangu zinanijia kwa kasi. Ninakumbuka msiba wa Mwanamtama, ndiyo uliyonifanya nianguke ila sikutambua kutokea nilipoanguka kilichoendelea nyuma yangu, hadi sasa hivi kumbukumbu zinaponirejea tena.
“Dobe nyamaza kulia, wewe ni mwanaume. Ulimpenda Baby wako, lakini Mungu amempenda zaidi yako. Tumeumbwa kwa udongo, tutarudi kwa udongo. Mbele yake nyuma yetu. Jikaze kwani hili limeshatokea. Ukiendelea kuwaza jambo hili unaweza kudata bure, kwani saa chache zilizopita kama siyo juhudi zetu, hakika ulishakuwa chizi kabisa. Unaulizwa Kunde wewe ulikuwa ukijibu Choroko!”
Ninainua uso wangu ninamtazama daktari kwa uchungu, kisha ninashika kichwa changu, machozi yananitoka mtoto wa kiume. Moyo unaniuma. Kweli kifo kimeumbwa, lakini pia msiba huwa mchungu kwa mtu wako wa karibu.
“Jikaze ndiyo ukubwa huo, kisha hapa hospitali siyo mahala pazuri, kama ukiwa hivyo ulivyo itabidi tukulaze, sasa unaweza kupata maradhi ya kuambukiza hapa bure, matokeo yake ukawa ulikuja na kadha ukaondoka hapa na kadha wa kadha. Jikaze ili ukaugulie nyumbani, kwani hii dripu ikesha tu na hali yako ikiwa hivi unavyo jifahamu, basi tutakupa ruhusa, kwani gharama za matibabu umeshalipiwa tayari hudaiwi.”
Ninamtazama huyu Dakitari anaponambia kuwa gharama za matibabu, nimeshalipiwa ninashindwa kumuelewa.
“Dokta ni nani alienilipia mie gharama za matibabu?”
Dokta ananitazama kisha ananambia.
“Alipokuja kukutazama ulikuwa bado upo kwenye maruwe ruwe ya dawa na maumivu. Hivyo ukashindwa kumfahamu. Ila ametaka jina lake tulihifadhi tusikutajie kwa vile na wewe hukuweza kumtambua alipokuja awali, ila amesema kabla ya kukupa ruhusa tumpigie simu, ili akufate akuchukue kwani amejinadi kuwa wewe ni mtu wake wa karibu sana!”
Maneno ya Dakitari yananifanya nisahau uchungu wa kufiwa na nimpendae, nishughulike na huyo mtu alienilipia ambae kumbe alinijia hapa mie nikiwa nimechanganyikiwa hata nikashindwa kumtambua.
“Samahani Dokta ninaomba unitajie japo jina lake tu, au umbile lake namna alivyo, au jinsia yake tu kwani nipo njia panda hapa.”
Lakini Dakitari anakataa kata kata kunambia kwa madai eti analinda usiri aliowekeana na mteja wao.
Ninakuwa mpole ninasubiri Dripu lishe, mara ninakumbuka simu yangu. Ninajipapasa kuitafuta mifukoni mwangu.
“Unatafuta kitu gani?”
Dokta ananiuliza, bila shaka kunipima kama nipo sawa bado au laa.
“Natafuta simu yangu.”
Ninamjibu kuwa ninatafuta simu, anaingiza mkono mfukoni mwake ananionesha simu yangu anayo yeye!
“Simu yako nimekabidhiwa mie, na waliyokuleta hapa, hivyo mie ndiyo nimeizima ili kukataa usumbufu wa kelele ya simu hapa wodini, lakini pia wewe mwenyewe hukuwa na uwezo wa kumjua mtu aliekutembelea tu, sembuse simu? Hivyo nitakukabidhi ukiruhusiwa mie nipo na wewe hadi saa nne usiku.”
Ninakubali maneno ya dokta kwa shingo upande, kisha ninakaa kimya nikitafakari mustakabali wa maisha yangu. Nilipotoka, nilipo sasa na ninapokwenda.
Ninapata kugutuka kitu, dokta anaitazama Dripu ikiwa inaishia.
“Dokta samahani sana.”
Dokta ananitazama kisha anasogea karibu name kinisikiliza.
“Dokta nimeshafika hapa tafadhali ninaomba unipime Virusi vya Ukimwi kabisa ili nijijuwe.”
Dokta ananitazama kwa makini.
“Kwa nini unataka kupima Virusi Dobe?”
“Ili nijue afya yangu.”
Namjibu kwa mkato. Dokta anatikisa kichwa juu chini.
“Baadhi ya watanzania wanataka kupima Virusi, kwa sababu ya mambo makuu matatu. Kwanza kama mpenzi wake akiwa amemwambia amepima amekutwa na maambukizi. Pili kama amesikia mwanamke/mwanaume aliewahi kufanya nae Ngono zembe amekufa kwa Ukimwi. Na tatu mtu akiwa anakonda na heshi kupatwa na maradhi nyemelezi, ndiyo anataka apime afya yake. Lakini wakutaka kupima ili watambue afya zao ni wachache sana.”
Dokta anaposema maneno hayo ananichoma moja kwa moja moyoni mwangu, kwani mie sababu yangu ya kupima hasa ni baada yakusikia baby Mwanamtama ni muathirika, na ameshakufa tayari.
Dokta anakwenda kuchukua vipimo vyake, kisha anakuja navyo nilipo. Anaitazama Dripu yangu inamalizia matone ya mwisho kadhaa. Anaifungua mkononi mwangu, sindano inatoka na damu.
“Basi imekuwa kheri Dobe damu hii hii inatosha kupimia sitokutoboa tena.”
Anaposema maneno hayo damu yangu anaidondoshea katika kifaa maalumu cha kupimia kama umeambukizwa virusi au laa. Mkono wangu ananiwekea Pamba yenye spirit ananambia niishikilie kwa muda ili damu isitoke, nami ninafanya hivyo.
Anakitazama kipimo changu ananitazama usoni.
“Dobe umeshawahi kupima VVU siku za nyuma?”
“Hapana Dokta sijawahi kupima VVU.”
Ninamjibu hivyo ili asianze kunipa majibu kwa matokeo ya kulinganisha na vipimo vya nyuma bure.
“Ok umeoa wewe?”
“Hapana sina mke.”
“Una mchumba au bibi unaeishi nae?”
“Dokta nambie tu bwana kama nishaukwaa. Unanizungusha bure tu. Mara mke mara mchumba au Bibi, mie mwanaume rijali nitakosa wapi mambo hayo? Nichane tu kama nishaungua nijijuwe.”
Dokta anakitazama kipimo changu, kisha ananitazama.
“Dobe nikikwambia kuwa umzima hujaathirika utafanyaje? Na nikikwambia umeathirika vile vile utafanyaje?”
Yaani hapa napigwa maswali ya mitego tu aaah.
“Dokta haya maswali yenu ya namna hii ndiyo mnawafanya watu wafe kwa presha nyie. Sasa nikiambiwa mzima nifanyeje kama sikufurahia kuwa nimesalimika?! Na ukinambia nimeukwaa ni lazima nitahuzunika, hakuna mtu anaepima virusi vya Ukimwi, kisha aambiwe ameambukizwa akafurahi au akaweka Rusha Roho (KIGODORO) nyumbani kwake, nambie tu nijue moja. Maana unanichosha kabla hata ya majibu”
Ninamwambia huyu Dokta huku mapigo ya moyo yananienda mbio kinoma wahaka umenizonga, mashaka yamenijaa! Jasho linanitoka kama maji. Kifupi sina amani kabisa. Kupima siyo kazi mjamani, bali unapopokea vipimo ndiyo utaijua Junjunlai!













Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: