KATIBU wa Mila wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Mwanasimtwa Mwagongo amesema tukio la kupatwa kwa jua linalotarajiwa kutokea leo katika Kijiji cha Rujewa wilayani hapa ni ishara ya Mwenyezi Mungu kuukubali uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza Tanzania kutokea tukio hilo tangu Aprili 18, 1977 na kwamba tukio kama hilo la kihistoria linatarajiwa kutokea tena nchini Mei 21, 2031.
Mbali ya Rujewa ambako wataona kupatwa kwa jua kwa asilimia 97 sawa na miji ya Makambako, Masasi, Mbeya, Tunduru, Njombe na Sumbawanga, miji mingine ambayo itaona tukio hilo kwa ukaribu zaidi wa asilimia 96 ni Katavi, Nachingwea na Songea ikifuatiwa na Kigoma, Iringa, Mtwara na Lindi.
Akizungumza jana na waandishi habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania (Tajati) nyumbani kwake katika Kata ya Isisi, Mwagongo alisema tukio hilo la kupatwa kwa jua nchini si mkosi, bali ni sawa na taa iliyokuwa imezimika na sasa imewashwa na kuongeza kuwa, ni ishara kuwa Mungu ameukubali utawala uliopo madarakani na ndiyo sababu ametoa giza na kuleta nuru.
Aliwaasa viongozi wa dini zote kote nchini kuliombea tukio hilo ili lifanyike na kupita kwa amani na pasiwepo na uvunjifu wa amani utakaosababisha jamii kutoa tafsiri ya tofauti baada ya tukio hili la kihistoria ambalo litafanyika kati ya saa 4.15 asubuhi hadi saa 8.00 mchana.
Alisema baada ya tukio hilo, wazee wa kimila watachinja ng’ombe kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa neema ya tukio hilo na pia kumwomba aiepushe jamii na madhara yoyote yanayoweza kujitokeza.
“Hapo zamani watoto walikuwa hawaruhusiwi kutoka nje siku ya tukio hili. Wazee waliamini ni ajali ya kugongana jua na mwezi na wanaoumia ni wanadamu hasa watoto kwa kusababishiwa milipuko ya magonjwa mbalimbali,” alisema katibu huyo na kuongeza:
“Lakini kwa sasa tunatambua kuwa ni tukio la kisayansi na kutokea kwenye eneo letu ni neema kutoka kwa Mungu. Kupitia tukio hili dunia itaijua Tanzania, itaijua Mbarali na itaijua Rujewa. Ni tukio ambalo limetutangaza.”
Kwa upande wa walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali mjini Rujewa walionesha kuwa na furaha kubwa ya ujio wa tukio hilo wakisema watapata fursa nzuri ya kujifunza kwa vitendo kwa kuwa watajionea badala ya kusimuliwa au kusoma kwenye vitabu.
Mwalimu wa taaluma katika Shule ya Msingi Isisi, Donatha Nkwera alisema walimu shuleni hapo wamewaandaa wanafunzi kwa ajili ya tukio hilo linalotokea jirani na shule yao.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya huduma za kijamii zimeonekana kukosekana kutokana na wingi wa wageni waliofika wilayani hapa.
Moja ya huduma hizo ni nyumba za kulala wageni ambapo licha ya vyumba kuwa vya shida pia baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo wamepandisha bei za kupanga kutoa Sh 10,000 hadi Sh 30,000.
Kadhalika, huduma muhimu zikiwemo za mawasiliano zilionekana kuwa za shida hadi jana kutokana na umeme kukatika tangu saa mbili asubuhi hadi jioni, hivyo kuleta usumbufu na kukwamisha baadhi ya kazi
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment