Kupatwa kwa jua leo si muujiza


Wanafunzi wakiangalia kupatwa kwa jua kwa kutumia miwani maalumu.

TUMESHATANGAZIWA kuwa leo kutakuwa na kupatwa kwa jua. Kwa hapa Tanzania tukio hilo litatokea kati ya saa nne asubuhi na saa sita mchana.
Tukio hili ni la kawaida ambapo kivuli cha mwezi kinapokuwa kwenye eneo la dunia. Dunia inapolizunguka jua na mwezi kuzunguka dunia, hutokea mwezi ukakaa katikati ya jua na dunia katika mstari mnyoofu na kuzuia mwanga wa jua kufika duniani. Tukio hili hujulikana kama kupatwa kwa jua. Kwa kanuni za mwanga, kuzibwa kwa mwanga kutoka kwenye chanzo husababisha kivuli chenye sehemu mbili, Sehemu ya kwanza ni kivuli kikuu, yaani giza totoro (umbra) kikizungukwa na kivuli chenye mwanga mdogo au hafifu (penumbra).
Kwa sehemu ambayo kivuli cha mwezi ni hafifu huitwa kupatwa kwa mwezi kipete au kwa lugha ya Kiingereza ‘partial eclipse’ ili kukitofautisha na kile ambacho dunia inafunikwa kabisa (umbra) au kwa Kiingereza total eclipse of the sun. Kwa mwaka huu, kitakachoshuhudia nchini mwetu ni kupatwa kwa mwezi kipete (kuonekana kama pete) yaani kinachoitwa kwa Kiingereza, partial eclipse of the sun. Ni hali ambayo huwa haitokei mara kwa mara lakini kwa sasa dunia nzima hali hiyo itashuhudiwa maneo ya mikoa ya Njombe na Katavi.
Wako baadhi ya watu wanaohusisha kupatwa kwa jua na imani za kijamii. Kwa mfano, mjamzito anaambiwa akae ndani wakati wa tukio hilo ili mimba isiharibike. Wengine huhusisha kupatwa kwa jua na uchawi. Kwa wengi mliosoma mnajua kwamba hili ni tukio litokanalo na mizunguko ya magimba huko angani. Unaweza hata kutengeneza mfumo wa jua katika maabara na kuigiza (simulate) mzunguko wa dunia na mwezi na kuchunguza kivuli cha jua la kuigiza.
Vilevile mliosoma mambo haya bila shaka mnajua kwamba hili ni tukio ambalo halitokei mara kwa mara katika eneo moja. Inaweza kuchukua miongo au hata karne kabla halijarudia sehemu fulani. Kutokana na upotofu ambao uko kwenye baadhi ya jamii, kumekuwa na juhudi makusudi za kuelimisha umma kuhusu kupatwa kwa jua. Kwa mfano, Kituo cha televisheni cha Channel Ten wiki chache zilizopita kiliendesha kipindi kuhusu kupatwa kwa jua kutakakoonekana leo nchini mwetu.
Kituo hicho kiliwakaribisha wataalamu wa Fizikia ya Anga (Astrophysics) watatu akiwepo Dk Nooral Jiwaji kulizungumzia suala hilo. Dk Jiwaji ni mtaalamu ambaye hutuandikia sana makala za nyota katika gazeti la Daily News. Dk Jiwaji ameunda kikundi chake kiitwacho ‘AstroContact Group’ ambacho anatarajia kisaidie katika kuelimisha umma katika nyanja ya astronomia.
Katika mchango wake alipokuwa studio, Dk Jiwaji aliitaja siku ya kupatwa kwa jua kwa kusema, “Septemba 1 (yaani leo) kutakuwa na kupatwa kwa jua kipete kuanzia saa 2:13 hadi saa 8:00 mchana kutegemeana na na mahala utakapokuwa.” Alisema hivyo kwa kuwa dunia inajizungusha kwenye mhimili wake na kivuli kinahama sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu ya mzunguko huo.
Aliendelea kuwashauri watu wasitumie miwani ya jua, vionambali (telescopes), kamera n.k. kwa sababu mionzi ya jua ijulikanayo kama ‘ultraviolet rays’ inaweza kuharibu macho yao. Akasema badala yake watumie vioo maalumu vijulikanavyo kama ‘eclipse glasses’. Mmoja wa watazamaji alitaka kujua kama kupatwa kwa jua kuna athari kwa wanyama. Alijibiwa kwamba wakati mwingine kupatwa kwa jua huathiri wanyama wafugwao. Akasema kwa mfano, giza hilo huwafanya kuku warudi kwenye vibanda vyao wakihisi usiku umefika.
Lakini akasema, binadamu asiyekuwa na hii taaluma hujaa hofu hasa kama jua lilikuwa kali (bila mawingu) na ghafla giza likaingia. Wengine wanaotazama jua hilo dakika chache kabla ya kupatwa husema jua linapigana na mwezi. Mwanga wa jua unaporudi wanasema jua limeshinda! Juhudi nyingine ni zile za waandishi mbalimbali walioandika kuhusu kuwepo kwa tuko hilo la kupatwa kwa jua. Kwa mfano, mwandishi wa gazeti hili katika toleo la tarehe 22 Agosti 2016, Theopista Nsanzugwanko aliwakumbusha wasomaji kuhusu siku hiyo.
Pamoja na kutoa maelezo mafupi, alimnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hewa (TMA), Dk Agness Kijazi akisema: “Kiwango cha kupungua kwa joto wakati wa kupatwa kwa jua kunatofautiana kulingana na umbali kutoka katika eneo ambalo jua limepatwa.” Alisisitiza pia kwamba hakuna athari kubwa zinazotarajiwa kutokea. Mkoa wa Njombe ambapo zaidi ya asilimia 90 ya kupatwa kwa jua kutatokea, Dk Rehema Nchimbi, akizungumza na vyombo vya habari aliwaonya watu wasitazame jua wakati wa kupatwa bila kutumia vifaa maalumu.
Aliwaeleza wananchi watakaotaka kutazama jua kuwa vifaa hivyo vya kutazamia vinapatikana. Taarifa hii imetolewa mapema ili watu wajiandae kwa tukio hilo la kihistoria. Dk Nchimbi aliwakumbusha kwamba tukio hilo hutokea baada ya muda mrefu na linaweza lisirudie tena sehemu litakapotokea leo, yaani hapa Tanzania na badala yake likatokea sehemu nyingine ya dunia.
Kituo cha redio cha East African Radio, Agosti 29, kilitoa muda mwingi wa matangazo kuwaelimisha wananchi kuhusu tukio hilo. Lakini la msingi la kuzingatia ni watu kujua kwamba tukio hili si muujiza na kuepuka kuangalia jua bila kuvaa vifaa maalumu




Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: