Kulinda lugha za asili ni kutunza urithi wa dunia

\


HIVI karibuni, Jamii ya Kimataifa iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha Asili, lengo likiwa ni kukuza utamaduni wa lugha mbalimbali ili kuendelea kuhifadhi urithi wa dunia.
Siku ya Kimataifa ya Lugha Asili huadhimishwa Februari 21 kila mwaka ambapo ujumbe wa mwaka huu ulikuwa: “Matumizi ya lugha za asili kama nyenzo ya kufundisha shuleni.” Ingawa Kiswahili ndio lugha kuu ya asili kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, wataalamu wa lugha wanasema Tanzania ina utajiri wa makabila zaidi ya 120, lakini yapo katika hatari ya kupoteza lugha za asili kwa kuwa idadi kubwa ya wazazi wanapuuzia lugha zao na kuwafundisha watoto lugha ya Kiswahili pekee.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lugha za asili ni utambulisho wa makabila mbalimbali duniani na zina umuhimu mkubwa katika jamii. Lugha za asili ndio zinazoifanya Tanzania kuwa na makabila zaidi ya 120 yenye mila, desturi na utamaduni tofauti. Lugha za asili nchini Tanzania hazijumuishi makabila ya wahamiaji wanaozungumza lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kireno, Kigiriki, Kispanishi, Kiarabu na Kihindi.
Wahadzabe, kabila kongwe Mwandishi wa kitabu cha hivi karibuni kuhusu Makabila ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, Gervase Mlola, anasema makabila ya asili yamegawanyika katika makundi mbalimbali kutokana na lugha na historia ya kundi husika. Kwa mujibu wa historia ya makabila, mila na utamaduni, Kabila la Wahadzabe au Watindiga ni kabila kongwe nchini ingawa ni lenye watu wachache.
Mlola anafahamisha kuwa mfumo wa maisha ya Wahadzabe unajenga imani kuwa kabila hilo ni masalia ya binadamu wa kwanza ambaye aliishi kwa kula nyama, mizizi na matunda. Pia utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa masalia ya mifupa ya mwanadamu wa kwanza aliyeishi miaka milioni 4 iliyopita yalipatikana katika makazi ya Wahadzabe katika mkoa wa Arusha. Lugha ya Wahadzabe inajulikana kama Khoisan ambayo ni sawa na watu jamii nyingine zinazozungumza lugha kama hiyo Afrika ya Kusini.
Kabila hilo ni jamii pekee nchini Tanzania inayoishi kwa kutumia mfumo wa binadamu wa kale ambapo wanaishi kwa kutegemea uwindaji pamoja na kukusanya mizizi na matunda ya pori kwa ajili ya chakula. Tofauti na makabila mengine ambayo utamaduni wao uko kwenye hatari ya kutoweka kwa sababu wa mwingiliano wa tamaduni za kigeni, kabila la Wahadzabe linaweza kutoweka kwa sababu kasi ya kuzaliana ni ndogo na halijichanganyi na makabila mengine.
Tofauti na makabila mengine, Wahadzabe hawana shughuli ya kuwaendeleza kiuchumi, wanaishi porini na nyumba sio jambo la lazima kwao. Wahadzabe wana miili midogo, ni weusi na wana chale kwenye mashavu. Makabila ya Kibantu Kundi la pili linajumuisha makabila yanayozungumza lugha ya Kibantu. Mtafiti wa lugha za Kiafrika, John Sutton anasema asilimia kubwa ya makabila ya Tanzania yanazungumza lugha ya Kibantu.
Ingawa utamaduni na desturi za makabila ya Kibantu yanatofautiana kwa kiasi fulani, asilimia 90 wanajihusisha na kilimo, ufugaji na uhunzi. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Wasukuma ambao wanapatikana mikoa wa Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu na sehemu za mikoa ya Tabora na Mara ndio kabila kubwa nchini Tanzania likifuatiwa na makabila mengine yenye watu zaidi ya watu milioni moja ambayo ni Wahaya, Wanyakyusa, Wanyamwezi na Wachaga.
Jamii ya Nailoti Kundi la tatu linajumuisha makabila yanayozungumza lugha ya jamii ya Nailoti ambao ni Wamasai na Wabarabaig. Ingawa kabila la Wamasai sio kubwa, ni maarufu kutokana mfumo wao wa maisha unaotegemea ufugaji wa kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo. Wamasai na Wabarabaig ni maarufu kwa kutunza mila na desturi ngumu ambazo haziingiliani na makabila mengine.
Hata hivyo, mabadiliko ya mfumo wa maisha yameanza kuathiri utamaduni wa Kimasai kwa kuwa baadhi ya vijana wa Kimaasai wameacha kuchunga na hivi sasa wamejiingiza katika kazi za ulinzi na ususi wa nywele. Wazungumzao Kikushi Kundi la nne linajumuisha makabila yanayozungumza lugha ya Kikushi wakiwamo Wairak, Wagorowa, Waburungi, Waalawa na Wambugu.
Historia kwa njia ya simulizi na tafiti za masuala ya za makabila inasema chimbuka la watu jamii ya wakushi linatoka na kizazi cha watu wa kale Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati. Kwa ujumla makundi hayo yamewezesha Tanzania kuwa na makabila zaidi ya 120. Ingawa baadhi ya makabila hayajafanyiwa utafiti wa kutosha, ripoti mbalimbali kuhusu makabila zinasema baadhi ya makabila yana watu wachache wasiozidi watu 2,000 wakati makabila mengine yana watu zaidi ya milioni tano.
Makabila kuficha asili Baadhi ya makabila yenye watu wachache yanazungumza lugha ya kipekee na utaratibu wao wa kuishi unatofautiana na wa makabila mengine na yanatimiza vigezo vyote vinavyojenga kabila. Hata hivyo baadhi ya makabila hayo yanapojichanganya na watu wa makabila mengine wanaficha asili yao kwa kujitambulisha kuwa wanatoka makabila makubwa katika mikoa wanayoishi.
Pia uwiano mbovu wa mawasiliano na huduma inayotolewa na vyombo vya habari katika kutangaza utamaduni na rasilimali za nchi unasababisha makabila machache kufahamika na kupata umaarufu mkubwa na kusababisha majina ya baadhi ya makabila kuonekana kama msamiati mpya wakati yamekuwepo hata kwa muda mrefu.
Makabila yasiyofahamika sana
Makabila ambayo hayafahamiki kwa watu wengi na ambayo hayajapata nafasi ya kutosha katika vyombo vya habari ni pamoja na Waalagwa, Waalawa, Waakiek, Waasa, Waembe, Wabende, Waalama, Wadatooga, Wambugu, Waburunge,Waikoma, Wadhaiso, Waisanzu, Wakahe, Wakami, Wakimbu, Wakwaya, Wakwifa, Wajiji, Wakabwa, Wakagura, Wakisankasa, Wakonongo, Wakutu, Wakw’adza, Wakwaya, Waruri, Wakwavi na Walambya.
Makabila mengine ambayo hayafahamiki ni Wamagoma, Wamakwe, Wamalila, Wamambwe, Wamanda, Wamaviha, Wambugwe, Wambunga, Wamosiro, Wampoto, Wamwanga, Wandonde, Wandendeule, Wangasa, Wangindo, Wangulu, Wangurimi, Wangwele, Wanilamba, Wanindi, Wanyamwanga, Wanyanyembe, Wapimbwe, Wanyiha, Warufiji, Warungi, Warungu, Warungwa, Warwa, Washubi, Wasagara, Wasizaki, Washuba, Wasangu, Wasegeju na Wasumbwa.
Mengine ambayo hayafahamiki ni Watemi, Watongwe, Watumbuka, Wavidunda, Wavinza, Wawanda, Wawanji, Waweware, Wazigula, Wazyoba, Wadoe, Wagorowa, Wamwera, Wandali na Wapangwa. Watu na viongozi wa makabila hayo wanapaswa kuweka mikakati ya kutangaza mila na desturi zao ili Watanzania kudumisha utajiri wa mila na desturi za makabila ya Tanzania.
Makabila yanayosikika sana
Makabila yanayosikia zaidi ni Waarusha, Wabarabaig, Wabena, Wabondei, Wadigo, Wafipa, Wagogo, Wagorowa, Waha, Waahdzabe, Wahangaza, Wahaya, Wahehe, Waikizu, Wairaqw, Wajita, Wakaguru, Wakara, Wakerewe, Wakinga, Wakisi, Wakuria, Wakwere, Waluguru, na Waluo.
Makabila mengine yanayofahamika ni Wamachinga, Wamakonde, Wamakua, Wamatengo, Wamatumbi, Wameru, Wandamba, Wandengereko, Wangoni, Wanyambo, Nyamwezi, Wanyaturu, Wanyiramba, Wapare, Wapogoro, Warangi, Wasafwa, Wasandawe, Wasambaa, Washirazi, Waswahili, Wayao, Wazanaki na Wazaramo.
Ingawa makabila haya yanafahamika, yameanza kupata athari kwa kuwa vijana wanaotoka kwenye makabila hayo yanatumia elimu na mbinu za kisayansi kuendesha maisha yao jambo linaloathiri maendeleo ya lugha za asili, mila na desturi. Kwa kuwa mfumo wa maisha unabadilika, Watanzania wanapaswa kuweka mikakati ya kuwaridhisha watoto lugha na utamaduni wa asili kwa kuwa ipo tofauti kubwa kati ya ukabila na makabila.
Lugha na utamaduni wa asili ni urithi usioshikika na una thamani kubwa kwa Taifa hivyo wazazi wasipuuze lugha zao za asili kwa kisingizio cha kuepuka ukabila. Hata watu wanaozungumza Kiswahili muda wote wanaweza kuwa na ukabila. Kabila maana yake ni kundi la watu wanaozungumza lugha ya aina moja ambao mavazi, chakula na mfumo wa maisha yao ya kila siku unafanana.
Ukabila maana yake ni tabia ya watu wa kabila fulani kujipendelea katika nafasi za madaraka, masomo au fursa za kiuchumi. Suala la kubaguana kwa misingi ya kikabila ni tofauti kabisa na suala la kukuza na kuendeleza kabila. Wakati wa kupigania Uhuru wa Tanganyika Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alihimiza matumizi ya Kiswahili ili kuimarisha mfumo wa mawasiliano na kujenga Taifa lenye nguvu na jambo hilo haliwazuii Watanzania kuendeleza makabila yao.
Makabila na ukabila Baba wa Taifa alikuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukabila ili kudumisha amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania jambo linalowawezesha Watanzania kuishi kama ndugu bila kujali tofauti za rangi, kabila wala itikadi za kidini.
Hata hivyo, Kiswahili hakipaswi kuchukuliwa kama tishio kwa lugha za asili kutokana na ukweli kuwa binadamu ana uwezo wa kujifunza na kuzungumza lugha zaidi ya tatu ikiwa ni pamoja na kudumisha mila na desturi za asili ya Afrika. Taarifa za utafiti unaofanywa na wataalamu mbalimbali wa masuala ya lugha na utamaduni, wanabainisha sababu mbalimbali zinazowafanya wazazi kutowafundisha watoto lugha za asili. Sababu ya kwanza ni dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa lugha za asili zinajenga ukabila.
Sababu ya pili ni elimu na mwingiliano wa watu katika makabila ambapo hata watoto wanaozaliwa vijijini wanalazimika kuzungumza Kiswahili wakati wote kama lugha ya mawasiliano mashuleni na wanapokuwa nyumbani wanapendelea kuendelea kuzungumza Kiswahili. Mfumo wa maisha ya kisasa unaleta changamoto kubwa katika jitihada za kukuza lugha za asili pamoja na kudumisha mila na desturi nzuri za makabila mbalimbali nchini Tanzania.
Pia mwingiliano wa makabila katika ndoa, kukua kwa miji, maisha ya kuhamahama na kukua kwa mfumo wa elimu ni miongoni mwa sababu kubwa zinazodidimiza maendeleo ya lugha za asili, mila na desturi za makabila mbalimbali. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa nadra kuona watu wa makabila tofauti wakioana hivi sasa asilimia kubwa ya wanandoa ni watu wa makabila tofauti jambo linalosababisha watoto kuzungumza lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili.
Maisha ya kuhamahama yanasababisha watoto kutojifunza lugha ya asili hata kama wazazi wao wametoka kabila moja. Pia gharama za usafiri zinakwamisha maendeleo ya lugha ya asili kwa kuwa wazazi waliokuwa na desturi za kuwapeleka watoto wao vijijini wakati wa likizo hivi sasa wameacha kufanya hivyo kitendo kinachowanyima watoto fursa ya kujifunza mambo ya asili.
Kukua kwa miji na mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi kunasababishwa na watu wa makabila tofauti kuacha kutumia lugha zao za asili na kuzungumza lugha inayoeleweka na watu wote pia wanapohamia eneo fulani wanaacha mila na desturi za makabila yao na kufuata mfumo mpya wa maisha kulingana na eneo walilohamia.
Watanzania wanapaswa kuweka mikakati ya kufungua benki za kuhifadhi taarifa mbalimbali kuhusu mila na desturi za kila kabila nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwafundisha watoto lugha za asili na kuwasimulia hadithi mbalimbali juu ya mambo ya kale hususani juu ya mila na desturi ambazo hazina dhana potofu. Kwa kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaadhiri tamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali, wazee wanapaswa kutumiwa kikamilifu ili kukusanya taarifa muhimu na kuziweka katika maandishi.




Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: