Juzijuzi nilikuwa ninasikiliza mazungumzo kati yangu na mwanamuziki marehemu Andy Swebe, ambaye alikuwa mpiga gitaa la bezi aliyepigia bendi za Makassy, Mk Group, Bicco Stars na kadhalika. Mazungumzo hayo tulifanya nyumbani kwake Sinza, nami kwa sababu ambayo sikumbuki niliyarekodi mazungumzo haya. Nilikuwa nimesahau kabisa tukio hili, lakini ghafla katika pitia yangu kwenye maktaba yangu ya kanda za kaseti nikakuta kanda yenye mazungumzo ambayo baada ya kuisikiliza ilinipa maada ya kuandika leo.
Muziki hapa nchini siku hizi umepiga hatua kubwa, najua sentensi hii inaweza ikaanza kupingwa mapema sana na wengi ambao huona kuwa muziki wa siku hizi umerudi nyuma hasa kutokana na dhana kuwa asilimia kubwa ya muziki siku hizi umetengenezwa studio kwa kompyuta na haukupigwa na vyombo halisi. Lakini mimi siko huko, niko katika kuelezea uwingi matumizi na hata urahisi wa kusambaa kwa muziki siku hizi. Ni rahisi zaidi kusambaza muziki siku hizi. Muziki unasikika kwa watu wengi zaidi kwani kuna vyombo vya utangazaji radio na TV nyingi zaidi zinazowafikia watu wengi kuliko hapo awali. Mtu akiwa na simu yake pia anaweza akawa na uwezo wa kusikia muziki popote pale nchini, muziki kutoka redioni au aliyourekodi au hata muziki kutoka kwenye mtandao wa intaneti.
Licha ya maendeleo makubwa katika teknolojia ya kama ilivyotajwa hapo juu, bado kuna mambo mengine makubwa yalifanyika katika muziki enzi hizo wakati wa redio moja tu nchini ambayo hayajafikiwa katika zama hizi. Katika mazungumzo niliyofanya na Andy, alielezea mambo yaliyotokea wakati alipokuwa na Orchestra Makassy. Bendi hiyo iliamua kufanya ziara ya muziki ya wiki mbili nchini Kenya, lakini ziara hiyo ikaishia kuwa ni ya mwaka mmoja, ambapo walizunguka sehemu kubwa sana ya nchi ya Kenya. Je ni kundi gani la muziki linaweza kujisifu kwa kufanya ziara ya namna hiyo leo? Bendi kusafiri zamani ilikuwa ni jambo la kawaida sana, na mara nyingi hii ilifuatia baada ya bendi kurekodi nyimbo mpya ambazo zilirushwa kwa mara ya kwanza katika kipindi kilichoitwa Misakato, mara baada ya hapo kazi ilikuwa kuangalia watu walivyopokea nyimbo mpya na ndipo bendi zilianza safari ambazo kwa kweli zilijulikana mwanzo wake lakini mwisho ulikuwa ni majaliwa. Meneja wa bendi alitumwa kutangulia kupanga maonyesho kwenye miji kadhaa na baada ya hapo bendi ingefuatia nyuma. Katika safari hizi bendi maarufu ziliweza kupiga muziki katika miji na hata vijiji bila kujali umaarufu wa mji jambo ambalo hakika ni nadra siku hizi kwa mwanamuziki maarufu kufanya maonyesho katika vijiji vidogo vidogo. Ziara nyingine zilikuwa ni za kuelimisha, kwa mfano nilipokuwa Vijana Jazz tuliwahi kufanya ziara za kupiga katika vijiji mbalimbali Zanzibar katika kuhamasisha uvunaji bora wa karafuu.
Pamoja na kuenea kwa teknolojia ungetegemea vikundi vya muziki vingeweza kuwa na maonyesho mengi zaidi katika nchi zinazotuzunguka kama ilivyofanywa na Orchestra Makassy enzi ya Andy Swebe, lakini si hivyo, imekuwa ngumu kusikia moja ya bendi zetu maarufu zimeanza ziara ya namna hiyo. Lakini bendi zetu nyingi tu zilikuwa zikifanya maonyesho katika nchi za jirani zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, na hakika wimbo Bujumbura wa Vijana Jazz ni matokeo ya moja ya ziara hizi, Zambia pia ni nchi mojawapo ambao bendi zetu zilikuwa zikifanya maonyesho, ambapo bendi kama JKT Kimbunga na hata Vijana Jazz waliwahi kufanya maonyesho huko, mwanamuziki marehemu Justine Kalikawe na wenzie waliwahi kufanya kazi ya muziki huko kwa kipindi kirefu. Msumbiji na hata Malawi walikuwa kati ya wateja wa muziki wetu.
Mwaka 1988 Radio Tanzania Dar es Salaa (RTD), BASATA, Umoja wa Vijana na CHAMUDATA, Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania waliweza kutayarisha mashindano ya bendi za muziki ambayo hayajawahi tena kutokea mashindano ya aina hiyo na ya ukubwa wa aina ile. Mashindano hayo yaliitwa TOP TEN SHOW. Radio Tanzania ilipita kila mkoa na mashindano yalifanyika ambayo yalirekodiwa na kurushwa kwa masaa kadhaa kila Jumamosi. Mashindano haya hatimae yaliishia kwa bendi bora kukutana Uwanja wa Taifa na bendi kumi bora kutangazwa na kupewa zawadi, shughuli zote hizo zikirushwa hewani na RTD na hivyo kushirikisha nchi nzima katika mashindano hayo yaliyochukua miezi minane. Hakika hili halijafikiwa pamoja na uwingi wa vyombo vya utangazaji uliopo.
Wakati wanamuziki kutoka Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo wakiingia nchini Tanzania, wanamuziki wengi kutoka Tanzania waliingia nchini Kenya na kufanya kazi huko katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, na wengine kuwa watu maarufu sana huko. Bendi maarufu ya Simba wa Nyika ilikuwa ni ya wanamuziki waliotoka Tanzania. Wanamuziki hawa walitokea Tanga, wengi wao wakitoka bendi kongwe ya Jamhuri Jazz Band, wakahamia Arusha na huko kitwa Arusha Jazz wakiwa na mtindo wao waliouita Wanyika, na hatimae wakatua Mombasa, na ndipo bendi ilipojipa jina la Simba wa Nyika. Bendi hii ilianza kugawanyika kuwa makundi mengi sana kama Les Wanyika, na mengineo kama Super Wanyika, Wanyika Stars, Sigalame System na kadhalika, lakini katika makundi yote haya wanamuziki toka Tanzania ndio walikuwa kiini cha vikundi hivi. Si rahisi kusikia mwanamuziki wa Tanzania kuingia nchi yoyote jirani na kufikia ubora na umaarufu wa makundi haya katika zama hizi. Hakika kuna mengi makubwa yaliyofanyika kwenye muziki katika enzi ya teknolojia duni ambayo bado hayajafikiwa japo fursa sasa ni kubwa zaidi
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment