watoto waliotoka kijiji cha Nindi wakiwa tayari wameshapokelewa na uongozi wa Nicopolis Academy
uongozi wa Nicopolis Academy wakiwa na Mwenyekiti wa kijiji cha Nindi pamoja na viongozi wa Umoja Nindi group
Mkurugenzi wa Nicopoli akiwa na meneja wa Nicopolis Academye
viongozi wa Uomja Nindi group wakiwa katika kicha ya pamoja
Mwenyekiti wa kijiji cha Nindi Bi.Zitha Haule
Kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kijulikanocho kwa jina la NICOPOLIS Academy kilichopo wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe kimeanza kuwapokea watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutoka vijiji vya wilaya ya Ludewa kwa lengo la kuwapa matunzo mazuri pamoja na elimu.
Akiwapokea watoto kumi wanaoishi katika mazingira hatarishi kutoka kijiji cha Nindi kata ya Lupingu wilayani hapa jana Mkurugenzi wa kituo hicho Bw.Augustino Mwinuka alisema kuwa mpango huo wa kuwapokea watoto hao ni endelevu kutokana na lengo la uanzishwaji wa kituo hicho licha ya kuwa ukata wa fedha ni mkubwa lakini watapokelewa kwa awamu.
Bw.Mwinuka alisema kuwa watoto hao wa kutoka kijiji cha Nindi wametambuliwa na kikundi cha ujamaa Nindi group chini ya uongozi wa kijiji ni yatima na wanaishi katika mazingira hatarishi lakini kupitia michango ya wanachama wa NICOPOLIS Academy watasaidiwa kuishi kituoni hapo ambapo wataweza kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Alisema richa ya kuwa kituo hicho kinachukua watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na wenye ulemavu wa Ngozi pia wapo watoto ambao wameletwa na wazazi wao kwa lengo la kupata elimu bora inayofundishwa kituoni hapo kwa kulipia gharama nafuu ili kukiendeleza kituo kiweze kujitegemea.
“Kata ya Lupingu na vijiji vyake kuna watoto wengi wanaoishi mazingira magumu lakini kutokana na uhaba wa kifedha katika kituo chetu tumeona tuwachukue watoto kumi kwanza waanze masomo lakini kama tutapata ufadhiri tutazunguka vijiji vyote wilayani Ludewa ili kuwakusanya walau watoto ishirini kila kijiji ambao watanufaika na elimu tunayoitoa kwani wilaya ya Ludewa kuna idadi kubwa ya watoto wa namna hiyo”,alisema Bw.Mwinuka.
Naye Mwenyekiti wa kikundi ya Ujamaa Nindi Bw.Germanus Lukuwi alisema kuwa kikundi chao kinajishughurisha na mambo mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji hivyo kwa kushirikiana na Nicopolis academy kimeona kiwasaidie watoto hao kumi waweze kupata elimu na malezi bora hapo.
Bw.Lukuwi alisema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wilayani Ludewa kutokana na wazazi wao kufariki kwa maradhi mbalimbali lakini wahisani wa kuwasaidia watoto hao bado ni tatizo hivyo kupitia ujamaa Nindi group wakiungana na Nicopolis Academy wameanza kuona ukubwa wa tatizo hilo na kulifanyia kazi.
Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Nindi kata ya Lupingu wilayani Ludewa Bi.Zitha Haule alikipongeza kituo cha Nicopolis Academy kwa hatua waliyoanza nayo ya kuwachukua watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuanza kuwahudumua katika kituo chao kwani kumekuwa na changamoto nyingi inayowakabili watoto hao.
Bi.Zitha alisema kiwa ni vyema vituo na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakaiga mfano wa Nicopolis Academy kwa kuwafikia walengwa moja kwa moja na kuwasaidia kwani kuna baadhi ya taasisi hushindwa kupitia katika Serikali za vijiji zinapotaka kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na baadae huacha lawama kubwa katika Serikali za vijiji kutoka kwa wananchi kuwa kuna upendeleo wa utambuzi.
Mwisho.
@ habari ludewa blog
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment