Pengine nikuulize hata wewe msomaji wangu, unajuaje kama mwenzi wako unayeishi naye au uliyenaye ni mtu sahihi kwako? Una uhakika gani kwamba maisha yako ukiwa naye yatakuwa mazuri na hatakuja kuuvunja moyo wako? Huenda wengi wakakosa majibu zaidi ya kuishia tu kusema: ni mtu sahihi kwa sababu nampenda au ananipenda.
Hata hivyo, upendo pekee hautoshi kukufanya uamini kwamba huyo uliyenaye ni mtu sahihi kwa sababu upendo kama zilivyo hisia nyingine, kuna wakati huongezeka na kuna wakati hupungua au kuisha kabisa kwa hiyo kama unampima mwenzi wako kwa kigezo hicho, ipo siku utahisi kwamba pengine hukufanya uamuzi sahihi.
UTAMJUAJE KAMA NI SAHIHI?
Mtihani mkubwa ni namna ya kugundua kwamba huyo unayeishi naye ni chaguo sahihi katika maisha yako. Yapo mambo mengi unayoweza kuyatumia kumpima mwenzi wako lakini katika makala haya, tutazungumzia mambo manne ya msingi.
UNARIDHIKA UKIWA NAYE?
Jambo kubwa na la msingi linaloweza kukuonesha kwamba upo na mtu sahihi katika maisha yako ni kuridhika. Kuridhika ninakokuzungumzia hapa, ni ile hali ya moyo wako kujihisi kama unapata kila unachokihitaji na huna sababu ya kufikiria kuwa na mtu mwingine.
Kuridhika ninakomaanisha hapa, si lazima mtu awe na uwezo wa kukupa magari, majumba au vitu vya thamani kubwa, hapana. Namaanisha ile hali ya kuridhika kuanzia kihisia, kimawazo, kimapenzi na kimaisha kwa jumla.
Hujawahi kuona watu wanaishi maisha ya kimaskini lakini wana furaha, wanapendana, wanaheshimiana na kudumu? Ni kwa sababu kila mmoja ameridhika na mwenzake. Hujawahi pia kuona wake wa matajiri wanatoka kimapenzi na mahausiboi au vijana wa mitaani? Ni kwa sababu hawajaridhika kwenye maisha wanayoishi, hata kama wanapata kila kitu.
Wakati mwingine, baadhi ya watu hujaribu kufananisha uhusiano waliopo na waliowahi kuishi nao (ex), si makosa kulinganisha lakini isiwe kwa lengo la kubomoa.
Itaendelea wiki ijayo
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment