Karibuni wapenzi wa Jamvi la XXLove katika Jumatatu nyingine kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Mada ya leo itazungumzia namna ambavyo baadhi ya wapenzi wamekuwa wakiwalaumu wenza wao kuwa ni wabahili bila kuangalia uhalisia wa kipato, maisha na mazingira.
Kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya wanawake na wasichana kuendekeza zaidi mapenzi ya fedha kuliko mapenzi ya dhati, suala linaloifanya karne hii ya 21 kuweka rekodi kwa wanadamu wa Sayari ya Dunia kuwa ya mapenzi ya fedha zaidi ya neno penzi linavyotaka.
Nimekuwa nikipata maoni na maswali mbalimbali kuhusu uhusiano, miongoni mwa maswali hayo ni ishu ya jamaa kuachwa na mpenzi wake, kisa kaombwa shilingi elfu ishirini na yeye akatoa elfu kumi. Baada ya kumpatia yule mwanamke shilingi elfu kumi, tangu siku hiyo hajapigiwa simu wala kuulizwa chochote.
Inavyoonekana mwanamke huyo anapokuwa na shida ya kiasi fulani cha fedha basi anataka apewe na kama mpenzi wake atakuwa hana, anaonekana hafai kuwa mpenzi wake.
Ukweli huo siyo uungwana na siyo mapenzi hayo. Kama mwanamke akiwa na tabia hiyo hakika ataendelea kutumika sana kwa kupewa vijisenti na wanaume kwa ajili ya kuzini naye. Hapo ndoa atazisikia kwa wenziye tu.
Kimsingi wapenzi wanapaswa kujuana zaidi kuhusu suala la kipato. Hata kama unamuomba mtu fedha kwa ajili ya kitu fulani basi uwe unafahamu na uwezo wake wa kifedha kwa maana ya kile anachokipata.
Kama utamuaomba mpenzi wako laki moja wakati kipato chake kwa mwezi ni shilingi elfu sabini, unakuwa umekosea. Kwanza ni kumuumiza mwenzio kwa kumtengenezea mazingira magumu ya kutafuta fedha uliyomuomba. Kuna uwezekano wa yeye kujinyima kupita kiasi ili akutimizie lengo lako. Lakini pia kuna uwezekano wa yeye kujikuta akijiingiza katika tabia zisizo njema ilimradi tu apate fedha ya kukutimizia mahitaji yako.
Kama mpenzi wako umemuomba shilingi elfu ishirini na yeye akakupa elfu kumi, sioni kama kuna tatizo endapo atakuambia sababu za yeye kukupa nusu ya fedha uliyohitaji na kama atakuwa amekupa kimyakimya kuna tatizo. Inaonekana hakuna uwazi katika uhusiano wenu.
Hata kama akikupa nusu ya fedha, hakuna sababu ya kumkimbia na kumuhukumu kuwa pengine ana tabia ya ubahili, lah hasha! Jiulize kwa nini amekupa fedha hiyo kwani inawezekana kipato chake ni kidogo.
Ni udhaifu mkubwa sana na hata vitabu vya imani vinazungumza suala la mtu kuidhulumu nafsi yake kwa ajili ya mwingine, yaani kujifanya umeridhika na jambo ili kumridhisha mwingine.
Ingawa kuna wanaume bahili ambao wana uwezo wa fedha lakini hawako tayari kuwajali wapenzi wao, jambo linalosababisha wenza wao kuchepuka. Utakuta mwanaume ana uwezo wa kununua nguo hata za laki tano lakini hamnunulii mkewe au mpenzi wake hata sidiria ya shilingi elfu tatu, wakati huo zile nguo anayezifua na kuzinyoosha ni mwanamke. Hivi unahisi anajisikiaje anapoona wewe una nguo nyingi za thamani lakini yeye humnunulii?
Kama wewe ni mmoja wa watu wenye tabia hiyo, tafadhali jifunze na kuanza upya kuboresha uhusiano wako. Kwa kuzingatia niliyoyaandika hapo juu, usikose mada nyingine wiki ijayo.
Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta: Mimi_na_uhusiano au unaweza kujiunga kwenye group letu la WhatsApp kwa namba za hapo juu
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment