Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakushukuru msomaji wangu uliyetumia muda wako kutoa maoni yako kuhusu mada hiyo.
Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mada yetu ambapo zaidi tutaangalia dalili zinazoweza kukuonesha kwamba uliyenaye ni mtu sahihi baada ya kuwa tumeiona ya kwanza kuwa ni kuridhika ndani ya moyo wako.
ANAKIDHI HAJA ZAKO KIKAMILIFU?
Jambo jingine linaloweza kukusaidia kujua kama upo na mtu sahihi ni kujiuliza kama uliyenaye anakidhi haja zako vizuri? Hapa namaamisha pia haja za kimwili, kiakili na kihisia.
Je, unafurahi kwa kiwango cha juu mnapokuwa pamoja faragha? Hufikirii tena kuwa na mtu mwingine kwa sababu huyo uliyenaye anayaelewa vizuri mahitaji yako ya kihisia? Kama jibu ni ndiyo, basi huyo ndiye mtu sahihi kwako.
ANA UKUBALI UDHAIFU WAKO?
Yawezekana una udhaifu katika eneo moja la maisha au jingine, iwe ni kitabia, kimaumbile au hata kiakili. Je, mwenzi wako anafanya nini kukusaidia kupambana na udhaifu wako? Anakutia moyo au ndiyo anatumia udhaifu wako kukusimanga?
Wapo baadhi ya watu ambao kwa sababu wenzi wao wana kasoro fulani, badala ya kuwasaidia wanatumia kasoro hiyo kama fimbo ya kuwachapia, wakigombana kidogo basi anakuvurumishia neno zito kuhusu udhaifu wako.
Iwe ni udhaifu wa kumudu katika tendo la ndoa, masuala ya fedha, hujasoma kama yeye au umekulia maisha ya kimaskini kama yeye. Je, anatumia udhaifu huo kukuhukumu mara kwa mara? Kama jibu ni ndiyo? Basi unaishi na mtu asiye sahihi.
ANA HURUMA NA WEWE?
Mtu anayekupenda kwa dhati, lazima awe na huruma na wewe katika kila jambo analolifanya. Hayupo tayari kukuona ukiumia, ukiteseka au ukipatwa na jambo lolote baya. Anapenda kukuona muda wote ukiwa salama, kimwili, kiakili na kihisia.
Ukiona unaishi na mwenzi wako lakini kila siku anakuombea ufukuzwe kazi, ufilisike, upate ajali mbaya au hata anakuombea kifo kwa sababu tu mna matatizo fulani katika uhusiano wenu, huyo si mtu sahihi.
Ukiona mwenzi wako anachekelea unapopatwa na matatizo, maana yake hana huruma na wewe na anatamani muda wote kukuona ukipoteza mwelekeo.
Mtu wa namna hiyo, hashindwi kukusaliti au hata kukuwekea sumu, hana huruma na wewe, chukua hatua!
Ni matumaini yangu kwamba utakuwa umejifunza kitu. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment