Kulingana na wataalamu wa matatizo ya usingizi kutoka Brazili akiwemo Dk. Rubens Reimão, inakadiriwa kwamba asilimia 35 ya watu ulimwenguni wana ugonjwa wa kukosa usingizi.
Aidha, licha ya usingizi kuwa ni moja ya kitu muhimu sana kwa afya ya mwanadamu yeyote, wanasayansi wanaamini kulala kunasaidia katika kujenga seli mpya za ubongo, wanaeleza kwamba, usingizi husaidia kuzalisha upya seli za ubongo ambazo nazo hujenga kemikali inayojulikana kama ‘Myelin’ ambayo ni muhimu katika kulinda ubongo wa binadamu.
Taarifa toka vyanzo mbalimbali zinaonyesha wazi kuwa binadamu huhitaji kulala ili kupumzika pamoja na kuufanya ubongo kufanya kazi yake inavyopaswa, lakini pia kumekuwepo na mambo ya kibaiolojia yanayofanyika binadamu anapokuwa amelala.
Kukosa usingizi kunasababisha vifo mapema
Wanasayansi wa Ujerumani na Uingereza mwaka 2011, walifanya utafiti uliolenga bara la Ulaya na kugundua kuwa watu ambao kwa kawaida huwa wanalala masaa machache (masaa 5 hadi 6) wengi wao hupatwa na vifo vya mapema kwa asilimia 12 zaidi ya wale wanaolala kawaida kwa masaa 8 vifo ambavyo hutokea katika umri wa baada ya miaka 25.
Usingizi unavyoathiri afya za watu hadi wakiwa kazini
Pia utafiti huo unaonyesha kwamba kulala zaidi ya masaa 9 pia
kunapelekea vifo vya mapema ingawa kulala huko kunaweza kukawa na
uhusiano na matatizo ya kiafya.
Inapokuwa Vigumu kupata usingizi
Kugeuka-geuka kitandani kwa saa nyingi, ukiwa macho, huku watu wengine wote wakiwa wamelala fofofo ni jambo lisilopendeza kamwe, hata hivyo, ni kawaida kukosa usingizi mara kwa mara kwa sababu ya mikazo na hekaheka za maisha lakini mtu anapokosa usingizi kwa muda mrefu huenda akawa na matatizo ya kihisia (moyo) au ya kitiba na ni muhimu mtu mwenye dalili hizo amuone daktari.
Ikiwa umegundua kwamba una tatizo la kukosa usingizi, usikate tamaa, kutambua kwamba una tatizo hilo ni hatua muhimu ya kulitatua kwani wataalamu wa wanasema asilimia 90 ya watu wenye ugonjwa huo wanaweza kutibiwa na kupona.
Msomaji wa Makala haya ya FikraPevu, ikiwa unaugonjwa huo, ni muhimu kujua hasa ni nini kinachosababisha ugonjwa huo. Uchunguzi wa kitiba unaoitwa Polysomnogram umetumiwa kupima na kutibu magonjwa mengi ya kukosa usingizi.
Ugonjwa huo kwa watu wazima
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kliniki ya Matibabu ya Dawa za Kulevya kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk. Frank Masao, amenukuliwa na FikraPevu akisema mojawapo ya visababishi vya kawaida vya kukosa usingizi kwa muda mrefu miongoni mwa watu wazima ni kukoroma. Anasema wapo baadhi ya watu ambao wamewahi kulala karibu na mtu/watu anayekoroma, wengi wao huudhika sana na hali hiyo.
Anasema kukoroma kunaonyesha kwamba mtu ana tatizo la kuziba koo na hivyo mapafu yake hayapati hewa ya kutosha kwa muda fulani. Hatua za kwanza za kutibu ugonjwa huo zinatakiwa kuanzia ndani kwa kupunguza uzito, kuepuka pombe na kutotumia dawa za kulegeza misuli.
Usingizi ni starehe lakini pia ni afya
“Hali inapokuwa mbaya zaidi, huenda mgonjwa akahitaji kufanyiwa
upasuaji wa kurekebisha koo, taya, ulimi, au pua ili hewa iingie na
kutoka kwa urahisi anapopumua” alieleza mtaalamu huyo.
Usingizi wa nusu saa una faida kwa Mtoto
Katika malezi ya mtoto mchanga, usingizi ni jambo la muhimu katika ukuaji wake, wazazi wengi wamezoea kuwaeleza watoto walale ili wakue. Usingizi wa mchana kwa mtoto humwezesha kukua kimwili na kiakili.
Wanasayansi wanaamini mtoto anayelala angalau kwa nusu saa mchana ana uwezo mkubwa wa kujenga mfumo wake wa kumbukumbu.
Utafiti wa kwanza ulifanywa na Timu ya Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sheffield na cha Ruhr, kilichoko Bochum, Ujerumani, hivi karibuni umebaini kuwapo uhusiano kati ya kulala na maendeleo ya ukuaji wa mtoto katika mwaka wa kwanza wa maisha yake.
Jambo baya zaidi ni kwamba watu wenye ugonjwa huo hawajui kuwa ni wagonjwa. Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Federal huko Sao Paulo, Brazili, asilimia 3 tu ya wagonjwa ndio hupimwa ugonjwa huo.
Wengi huona kukosa usingizi kuwa jambo la kawaida na hivyo wao husinzia-sinzia na kusumbuka mchana kutwa. Imebainika katika utafiti huo kuwa, usingizi wa nusu saa kwa mtoto humwongezea kumbukumbu na kumfanya ahifadhi mbinu mpya alizojifunza muda mfupi kabla ya kulala.
Utafiti huo uliwahusisha watoto 216 wenye afya njema wa umri kati ya miezi sita na mwaka mmoja, ambao walijaribiwa uwezo wao wa kukumbuka mambo mapya waliyojifunza.
Pia watoto wanaweza kupata ugonjwa wa kukosa usingizi, dalili za kukosa usingizi zaweza kuonekana akiwa shuleni, kwa mfano, kushindwa kufaulu mitihani, kuudhika upesi na kukosa utulivu (huenda ikafikiriwa kimakosa kwamba yeye ni machachari).
Umri mkubwa na matatizo ya usingizi
Kwa kadiri binadamu anavyozeeka, ndivyo matatizo ya kupata usingizi nayo yanavyoongezeka. Mara nyingi wazee hulala mapema na huamka mapema, au kulala usingizi usio mnono wa kushtuka shtuka nyakati za usiku.
Lakini pamoja na kukosa usingizi na kuamka kila siku ukijisikia mchovu pamoja na dalili nyingine, kukosa usingizi siyo hali ya kawaida kiafya, usingizi ulio bora ni muhimu katika umri mkubwa kama ilivyo kwa watoto wadogo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Mathayo Kalanga, ameiambia Njenje habari blog baadhi ya wanawake wajawazito huhisi usingizi sehemu kubwa ya siku.
“Hii ni kawaida katika miezi mitatu ya kwanza, miili yao tunawaelekeza kupunguza shughuli na kupumzika. Iwapo mwanamke mjamzito hawezi kulala kwa sababu ya wasiwasi au kuhangaika, anaweza kusaidika kwa kutumia mto, blanketi iliyokunjwana mengineyo” alieleza Dk. Mathayo.
Majibu wa Watabibu
Watabibu wengi huchukulia usingizi kama kipimo cha afya ya mtu husika, kama ilivyo kwa vipimo vingine ambavyo hutumika kumpima mgonjwa hospitali.
Hili ninalokuambia ninamaanisha, ndio maana mojawapo ya maswali yaulizwayo na wataalamu wa afya ni “Huwa unapata usingizi mzuri usiku?” alikaririwa akieleza Dk. Mathayo.
Amefafanua kwmaba wale walio na umri mkubwa na hawapati usingizi wa kutosha wanakuwa hatarini kupata magonjwa kama msongo wa mawazo, upungufu wa kuwa makini na upungufu wa uwezo wa kumbukumbu na pia tatizo la kulala sana nyakati za mchana.
Jinsi ya kuboresha usingizi
Punguza matumizi ya vinywaji vyenye kafeini, pombe na matumizi ya nicotini, vitu hivi vinatajwa na wataalamu wa afya kwamba ni vichangamsho vya mwili na huathiri upatikanaji wa usingizi. Vinywaji vyenye kafeini ni vizuri vikitumika katika nyakati za asubuhi.
Ingawa kunywa pombe kunatajwa kuwa kunaweza kumfanya mtu asinzie, unywaji wa kahawa, Chai, Koko, Chokoleti na vinywaji vilivyo na kola vyapasa kuepukwa usiku kwa sababu vinausisimua mwili.
Baadhi ya picha zikionyesha jinsi usingizi unavyoweza kuathiri afya za watu makazini
Kwa upande mwingine, inashauriwa kuwa watu wazoee kula maembe, viazi
vitamu, ndizi, wali, maharagwe, au njugu huchochea homoni iitwayo
Serotonin na kuweza kuleta usingizi. Imetahadharishwa kwamba kula
chakula kingi usiku sana kunaweza kuharibu usingizi kama tu kulala ukiwa
na njaa.
Pia wataalamu wanasema kwamba unaweza kuzoeza ubongo wako kutambua wakati wa kulala kwa kujilaza kitandani wakati tu unapotaka kulala. Kuutayarisha mwili kwa ajili ya usingizi pia hutia ndani kuwa mwangalifu kuhusu unachokula na kunywa.
Ni vizuri kwa watu walio na umri mkubwa kupata muda wa kuota jua, au kufanya matembezi juani. Mwanga mweupe wa jua husaidia kurekebisha homoni ya iitwayo kwa jina la kitaalamu ‘Melatonini’ na mfumo wa kulala na kuamka (Kwa kitaalam- Circadian Rhythms).
Inashauriwa kwamba ujaribu kupata angalau masaa mawili ya mwanga wa jua kila siku, fungua mapazia ya nyumba yako wakati wa mchana na jaribu kuota jua ndani kwako ukiwa umekaa kwenye kiti ukipendacho.
Je unahitaji msaada wa kitabibu?
Endapo jitihada zako mwenyewe zitashindwa katika kutatua matatizo ya usingizi yanayokukabili, muone daktari aliyekaribu yake kwani anaweza kuwa msaada mkubwa na kukusaidia kuondokana na matatizo ya ukosefu wa usingizi yanayosabishwa na sababu mbalimbali.
Wanasayansi wa Ujerumani na Uingereza wamesema usingizi ni muhimu kwasababu ukosefu wa usingizi unahusishwa na matatizo mengi ya kiafya, kama vile maradhi ya unene na moyo na baadhi ya mifumo ya watu wanayoishi ikiwemo wale wanapopanda tu kitandani husinzia moja kwa moja.
Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi pia navyo vinatajwa kuchangia ukosefu wa usingizi au usingizi wa kukatika mara kwa mara. Hivyo katika kushughulikia tatizo la kukosa usingizi usiku, inashauriwa kujiepusha na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, hasa vile vya kukaanga, muda mfupi kabla ya kupanda kitandani kulala
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment