Fahari ya majina yetu ya asili Tanzania imekwenda wapi?



(71)

HIVI sasa Watanzania tulio wengi majina yetu hayana asili yoyote ya Tanzania. Sana sana tumebakisha majina ya mwisho kuwa ya asili na yale ya mwanzo kuwa ya Kizungu ama Kiarabu. Mfano mzuri ni jina langu mimi.
Natambua fika kuwa majina haya tulio wengi tumepewa na wazazi wetu kwa misukumo mbali mbali ama kwa ajili ya utanda-wizi, masharti ya dini au kwa kufuata mikumbo. Leo hii na sisi tumekuwa wazazi lakini bado tunaendelea kufanya vivyo hivyo.

Swali la kujiuliza sasa je, majina yetu ya asili yamepoteza mvuto ama tunajisikia wa kale pale ambapo tunatumia majina hayo?
Turejee kidogo historia ili tuweze kuona fahari ya majina yetu ya asili ilipotelea wapi. Wakati wa ukoloni mawakala wa kikoloni walitangulia katika nchi za Afrika ili kuja kujionea hali halisi na kuanza kuwa sehemu ya Waafrika.
Mawakala hawa wa kikoloni walikuwa ni wamisionari, wafanyabiashara na wapelelezi ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kubadili fikra zetu ili tuweze kufikiri vile wao wanavyofikiri na kutoa taarifa kwa mabwana wakubwa juu ya hali ilivyo kwa nchi za Kiafrika.
Kati ya mawakala hawa wa kikoloni, wamisionari ndio waliojikita zaidi kubadili fikra zetu ili tuweze kuyaona mambo yetu kuwa siyo ya kistaarabu na ya kichawi. Tukashurutishwa kuacha ibada zetu za kuabudu miti, mito, milima, mizimu na mengineyo tukalazimishwa kupokea aina mpya ya ibada zilizostaarabika.
Katika mapokeo haya ya dini tulijifunza kusoma vitabu vya dini, kuhudhuria ibada, kupata ubatizo na mambo mengine kadha wa kadha.
Hapa ndipo changamoto zilipoanzia. Ili kuonyesha tumepokea dini vile ipasavyo ilitubidi kubatizwa na kupokea jina jipya kama vile ambavyo watakatifu wa dini walikuwa nayo. Hivyo, ilitupasa kusahau majina yetu ya asili na kuchagua majina hayo mapya ambayo hata maana yake hatukuyajua.
Utaratibu huu uliendela hata baada ya nchi zote za Afrika na Tanzania kwa ujumla kuwa huru. Leo hii tunashuhudia vile ambavyo asilimia kubwa ya Watanzania ukikutana nao wana majina ya Kizungu ama Kiarabu.
Leo hii ukipata mtoto na ukienda kumwandikisha hospitalini ama kwenye dini zetu husika kwa jina lenye asili ya kabila lako, kila mtu atakushangaa na kuanza kukuliza “kinachokufanya umpe mtoto jina baya hivyo ni nini”? Hapo ukute umempa mtoto wako jina la Bhoke lenye maana ya ‘asali’ kwa mujibu wa kabila la Kikuria.
Tukumbuke ya kuwa majina mengi ya asili yalitolewa kulingana na matukio ambapo mtoto husika alizaliwa. Ila leo hii wengi wetu tunaona kufanya hivi ni uzandiki na ukale.
Hali hii inadhihirisha fika kuwa bado hatujapata uhuru wa fikra na kuamua mambo yetu binafsi kama Watanzania na huru. Kwanini mpaka leo kwenye jambo rahisi kama hili linalomhusu mtu binafsi tunaamuliwa na mifumo mingine?
Mwanamuziki mkongwe marehemu Bob Marley aliimba kwenye wimbo wake wa Redemption Songs akisema: “Tujikomboe kutoka kwenye utumwa wa fikra, na sio mtu mwingine bali sisi wenyewe tunaweza kukomboa fikra zetu” (Emancipate yourselves from mental slavery; ‘cause none but ourselves can free our minds).
Ni imani yangu majina yenye asili ya makabila mbalimbali ya Tanzania yana maana nzuri kabisa tunayoweza kulinganisha na mazingira yetu. Lakini cha ajabu wengi wetu hatuoni tena ufahari wa kutumia majina yetu ya asili badala yake tunazidi kukumbatia majina kutoka nchi za Magharibi na kuyaona ndiyo yenye tija kwetu.
Kama alivyosema Bob Marley, ni jukumu letu kukomboa fikra zetu kutoka utumwani na tuweze kufanya uamuzi wenye tija kwetu. Hivi ulishawahi kujiuliza, kwanini nchi za Magharibi mpaka leo kila taifa lina majina yake ya asili ambayo yanatofautiana kutoka taifa moja kwenda jingine?
Sasa kwanini sisi tunashindwa kujikomboa katika utumwa huu wa fikra ambapo mpaka leo tunadhani kuwa na jila la Kizungu ama Kiarabu ni usasa na kuwa na jina la asili ni ukale?
Nimejaribu kuzungumza na watu wengi na kuwauliza inakuwaje wanawapatia watoto wao majina yasiyo na asili ya makabila yao. Wengi wao walijibu ni kwa sababu ya matakwa ya dini zao. Sasa swali la msingi linakuja je, ukimpa mtoto jina lenye asili ya kabila lako litamfanya asiweze kumwabudu Mungu wake? Kwani imani na jina vina uhusiano gani?
Nimeamua kujadili mada hii leo ili tuweze kujitathmini katika suala hili la majina na kuangalia ni kwa kiasi gani tuko huru na tumeuacha utumwa kando.
Ni dhahiri wengine wanaweza kudhani majina ni suala dogo na halina madhara yoyote kwenye maisha yetu. Hebu jiulize sasa, utambulisho wako uko wapi kama hata jina lako lenyewe unashindwa kujivunia nalo?
Kama tutashindwa kujikomboa katika jambo dogo kama hili la majina je, tunadhani tunaweza kujikomboa na unyonyaji mkubwa unaondelezwa na nchi za kibepari kwa ubabe mkubwa?
Leo hii inatia simanzi kubwa kuona mtu akiwa anakaribia kupata mtoto badala ya kujua taratibu za kabila lake kwenye kutoa majina utakuta watu wanakwenda kwenye mitandao na kuanza kutafuta majina kutoka kwa watu maarufu kwenye nchi za mabeberu.
Hali hii inadhihirisha kabisa tunaendelea kuwatukuza mabwana wakubwa hawa kwa kila kitu hata kiwe kidogo kiasi gani, tunadhani wao ndio bora zaidi kuliko sisi.
Ni muhimu kufahamu mabepari hawa hufarijika zaidi wanapoona tunausalimisha utu wetu wote kwao kwani inakuwa rahisi zaidi kuendelea kututawala kuanzia kwenye fikra zetu mpaka kwenye rasilimali zetu.
Tukumbuke ya kuwa mabadiliko ya kweli hayaanzi na mtu mwingine zaidi yako wewe mwenyewe.
Ili tuweze kukata minyororo hii ya utumwa katika fikra zetu hebu tuanzae kuenzi na kupenda asili yetu kwani bila kufanya hivyo baada ya muda mfupi tutashtuka hatuna cha kujivunia tena zaidi ya kuendelea kukumbatia kila kitu kutoka kwa mabepari.
Kwa kuhitimisha, hebu sasa tuanzishe mijadala kila mahali tulipo na kuona ni kwa namna gani tunaweza kuleta mabadiliko katika nchi yetu.
Tanzania ni yetu sote na tuanze kuipenda na kuipigania kwa dhati ili kuweza kunusuru utaifa wetu, maana tusipokuwa makini hata hiki Kiswahili tunachoringa nacho punde kitakuwa cha watu wengine.



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: