MIPAMBANO YA NIGERIA V MISRI HAITUHUSU, ILI KUFUZU CAN2017 NI KUISHINDA TENA CHAD, KISHA…





Kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa Taifa Stars kikifanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Chad
Na Baraka Mbolembole
Ushindi wa 1-0 ambao timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imeupata Jumatano hii ugenini dhidi ya Chad si kwamba utatosha kuifanya Tanzania kufuzu kwa fainali zake za kwanza za Mataifa ya Afrika baada ya kusubiri kwa miaka 36, lakini una maana kubwa sana kwa Stars katika kampeni zake ‘zisizopewa nafasi’ kufuzu kwa fainali za Gabon mwakani.
Wakati miamba ya Afrika na timu zinazopewa nafasi kubwa ya kuongoza kundi la 7 (Nigeria v Misri) zikitaraji kuvaana Ijumaa (leo) kisha kurudiana siku ya Jumanne ijayo, Stars imemaliza mechi tatu za mzunguko wa kwanza kwa ushindi dhidi ya timu iliyofungwa pia na Nigeria 2-0, kisha Misri 5-1.
Misri (kabla ya mchezo wa Ijumaa) wanaongoza kundi kwa faidi ya ushindi dhidi ya Stars na Chad. Nigeria ambao watakuwa nyumbani katika mchezo wa kwanza wiki hii dhidi ya Misri wana alama 4 sawa na Stars hivyo watalazimika kushinda pia kabla ya safari ya Cairo wiki ijayo.
Stars haitajali kitakachotokea katika gemu mbili za wababe hao, bali inapaswa kutazama namna ya kuifunga tena Chad siku ya Jumatatu ijayo jijini Dar es Salaam ili kufikisha alama 7 kabla ya kwenda ugenini kucheza na Nigeria.
“Nafasi inawezekana kama tukishinda games zote 3 zilizobakia. Siku ya Jumatatu hakuna kingine zaidi ya kuwafunga Chad kisha kwenda Nigeria kupambania ushindi, ingawa game ya Ijumaa kati ya wakubwa wawili itatoa mwelekeo wa kundi”, anasema mlinzi wa zamani wa Yanga SC na Stars, Ally Mayay ‘Tembele’ wakati nilipomuomba maoni yake kufuatia ushindi wa Stars siku ya Jumatano.
Wengi tunahitaji kuishangilia timu yetu ya Taifa katika michuano ya kimataifa na si kuendelea kubabaikia timu za mataifa mengine ndiyo maana timu inapofungwa lawama zinakuwa nyingi na pale matokeo ya ushindi yanapopatikana tumekuwa na mwamko mkubwa.
Kuifunga tena Chad inakuwa na maana kubwa kwa nchi na wengi wataungana kwa safari ya Nigeria ambayo uhakika wa kupata pointi walau moja utakuwapo.
“Matokeo ya Stars nimeyapokea kwa furaha sana ila mwalimu anatakiwa arekebishe baadhi ya maaeneo ambayo ameona hayako sawa ili tuendelee kupata ushindi katika mechi zingine zijazo. Tutarudiana na Chad siku ya Jumatatu, mechi ijayo ina maana sana kwetu coz ni lazima tushinde ili tujiwekee nafasi nzuri ya kupata nafasi yakushiriki mashindano lengwa.”
Anasema mlinzi wa zamani wa Simba SC na timu za Taifa, Lubigisa Madata Lubigisa ambaye alikuwapo katika kikosi cha Kilimanjaro Stars ambacho kilipoteza mchezo wa fainali wa Challenge Cup mwaka 2002 mbele ya Kenya katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Misri-mabingwa wa kihistoria wa wa CAN hawajafuzu kwa fainali 3 zilizopita, tena ikiwa bingwa mara tatu mfululizo. Sababu za kivita nchini humo zinatajwa kuwa sababu ya kuporokomoka kiwango cha soka katika nchi hiyo kwa kuwa hata klabu za huko hazina matokeo mazuri katika michuano ya CAF.
Stars ilifungwa 3-0 na Misri lakini kuna nafasi kubwa ya kuwashinda katika mchezo wa marejeano hapa nyumbani. Nigeria haikufuzu kwa fainali za mwaka jana pale Gabon, tena ikiwa bingwa mtetezi wa fainali zilizopita.  Kiwango cha mabingwa hao mara mbili wa kihistoria kimeshuka kwa kiasi kikubwa. Matatizo ya kinidhamu na kimaslai katika timu hiyo yamechangia kupoteza makali ya kawaida ya ‘Tai wa Kijani.’
Stars ilifanikiwa kupata suluhu-tasa dhidi ya Nigeria, inawezekana pia kupata matokeo kama hayo ugenini, au yale bora zaidi na si kupoteza mchezo huo. Kufuzu kama mshindi wa kwanza mbele ya Misri na Nigeria si jambo rahisi, lakini hata ikitokea nafasi ya kufuzu kama ‘washindwa watatu bora’ itapendeza sana kwa hakika.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars.


Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: