Na Baraka Mbolembole
Kiungo-mlinzi wa Simba SC, Abdi Banda ameingia katika mzozo usio na maana na kaimu kocha mkuu, Mganda, Jackson Mayanja. Banda hajacheza mchezo wowote ule tangu alipoondoshwa uwanjani kwa kadi mbili za njano katika pambano dhidi ya mahasimu wao Yanga SC, Februari 20.
Inasemekana mchezaji huyo alimgomea kocha wake kupasha misuli moto wakati wa mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Simba ilishinda 2-0 katika game hiyo na Banda akiwa katika benchi inasemekana aliponda kitendo cha Mayanja kutaka kumpumzisha mlinzi wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ baada ya mchezaji huyo kufanya makosa kadhaa ya kiuchezaji wakati matokeo yakiwa 0-0.
SIMBA NI KIRAKA CHA MUDA KWA BANDA’
Wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi Disemba, 2015 inasemekana kuwa, Banda ‘alijipeleka’ Yanga na kutaka asajiliwe katika timu hiyo kwa madai kwamba hathaminiwi katika timu yake ya Simba. Huu ni msimu wa pili kwa Banda klabuni Simba na ni msimu wake wa nne katika ligi kuu Bara.
Mchezaji huyo zao la African Sports ya Tanga alicheza kwa msimu miwili katika timu ya Coastal Union pia ya Tanga na kutangaza kipaji chake kama kiungo-makini-namba 6. Alikuwa mchezaji wa timu za Taifa za vijana hata kabla ya kusajiliwa Simba katikati ya mwaka 2014 akitokea Coastal.
Banda anaelekea kumaliza mkataba wake katika timu ya Simba, haitakuwa rahisi kwa mchezaji huyo kusaini mkataba mpya katika timu yake ya sasa kwa sababu tayari ametazama sehemu nyingine ambayo atakwenda kuendeleza kipaji chake.
Mara baada ya taarifa zake za kumdharau Mayanja zilipotoka na kupokelewa kwa mtazamo tofauti hadi na wapenzi wa Simba, katika moja ya akaunti yake katika mitandao ya kijamii, Banda aliandika sentesi yenye kuelezea kwamba ipo siku ataondoka na kuiacha Simba kwa kuwa yeye ni kiraka wa muda tu katika timu hiyo.
Mimi ni shabiki wa muda sasa wa Banda, ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi kwa pasi zake ndefu timilifu, Banda ni mkabaji mzuri, mtulivu na mwenye nguvu ambazo zimechangia uwezo wake wa kumiliki mpira kuwa juu.
Kama kuna mahali atakwenda na kupata mafanikio zaidi nitamuunga mkono daima, lakini kama mchezaji kijana mwenye mtazamo wa kusonga mbele zaidi na kupata mafanikio katika soka anapaswa kwanza kumfuata Mayanja na kukiri kumkosea heshima mbele ya wachezaji wenzake.
Inawezekana hakuwa na lengo baya wakati aliposema kuwa ‘ Tshabalala hakupaswa kutolewa,’ lakini katika mazingira yoyote yale mchezaji hapaswi kukosoa mbinu za mwalimu wake katika namna ya ‘kejeli-dhihaka-na nadharau.’
Ndiyo, ataondoka Simba lakini bado ana nafasi ya kupata taji kubwa zaidi katika nchi akiwa na timu hiyo ambayo inaongoza ligi kwa alama 7 zaidi ya timu za Yanga na Azam FC.
Banda anaweza kujiunga na Yanga kama anavyohitaji au Azam FC sehemu ambayo atakuwa na nafasi zaidi ya kuthaminiwa na kuendeleza kipaji chake lakini kitendo chake si cha ki-nidhamu na wachezaji wengi wenye tabia za kuwadharau walimu wao hawakuwa na mafanikio endelevu licha ya vipaji vikubwa walivyokuwa navyo.
Rejea sakata la Carlos Tevez na kocha Roberto Mancini. Tevez ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Manchester City aligeuka mchezaji wa kawaida tu mara baada ya kumgomea Mancini kuingia uwanjani kama mchezaji wa akiba katika mechi dhidi ya FC Bayern Munich katika ligi ya mabingwa ulaya msimu wa 2011/12.
Baada ya tukio lile, Mancini ‘alimfungia vioo’ na timu ikawa njiani kushinda EPL bila ya Muargentina. Hadi alipokuja kuomba msahama ndipo akarudishwa na mchango wake katika michezo michache ya mwishoni mwa msimu ulikuwa mkubwa sana na unaweza kusema bila urejeo wake kikosini City isingeshinda ubingwa.
Baada ya kushinda EPL, Tevez aliachana na City na kujiunga na Juventus ya Italia. Ilikuwa lazima aondoke kwa sababu hatamashabiki wa timu yake hawakuwa wakimuunga mkono kutokana na kitendo chake cha dharau kwa kocha Mancini.
Mashabiki wengi wa Simba ambao wanataka ubingwa wa kwanza baada ya misimu mitatu mitupu, waliunga mkono adhabu aliyopewa mlinzi Hassan Isihaka wakati alipomuuliza kocha wake kwanini hakumpa nafasi ya kucheza katika mchezo dhidi ya Yanga na badala yake akampanga katika mchezo wa kombe la FA dhidi ya Singida United.
Na sasa wameendelea kuwa upande wa Mayanja ambaye anataka uongozi wa timu yake kumuadhibu Banda kwa makosa ya kumdharau katika gemu dhidi ya Coastal. Ni kweli, Simba ni kiraka cha muda tu kwa Banda lakini ni vyema akajirudi na kumuomba msamaha kocha wake wa sasa kabla ya kuachana na klabu hiyo
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment