Wakizungumza na Nipashe mjini hapa jana kwa nyakati tofauti, walisema Vyama vilivyobakia katika uchaguzi wa marudio, hakuna chenye uwezo wa kutimiza masharti ya kushiriki kuunda serikali ya pamoja kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Omar Said Shaaban, alisema kama CUF itataendelea kushikilia msimamo wake, SUK itakufa na Zanzibar kulazimika kuundwa serikali ya Chama kimoja, kinyume cha Katiba ya Zanzibar.
Alisema tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, nje ya CCM na CUF, vyama vingine vimeshindwa kupata hata kiti kimoja cha udiwani Zanzibar.
Alisema mashariti ya Katiba ya Zanzibar, ili chama kiweze kushiriki kuunda serikali ya pamoja lazima kiwe na uwakilishi wa viti ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kupata kuanzia asilimia 10 ya matokeo ya uchaguzi huo.
Hata hivyo alisema kuwa ni pigo kubwa kwa Zanzibar kama itashindwa kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu malengo ya kuletwa mfumo huo yalikuwa kuponya makovu ya kisiasa na kujenga umoja wa Kitaifa kwa wananchi wake.
Naye wakili wa kujitegemea Awadhi Ali Said alisema serikali itakuwa na wakati mgumu kuendesha nchi ikiwa imetulia kama SUK itakwama kuundwa kutokana na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kwa wananchi wa Zanzibar.
“Pande zilizokuwa zikivutana zikiwa na nguvu sawa zimeibuka tena na nchi haiwezi kupiga hatua ya maendeleo katika mazingira kama haya.”alisema Awadhi.
Hata hivyo alisema kama Serikali ya Umoja wa kitaifa itakufa chimbuko lake litakuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, aliyefuta matokeo ya uchaguzi na kusababisha mgogoro wa kisiasa.
Hata hivyo, Balozi mstaafu Ali Abeid Karume, alisema hatima ya Serikali ya umoja wa kitaifa ipo mikononi mwa CUF.
Alisema kama CUF kama itashiriki uchaguzi, SUK itaendelea lakini kama itasimamia uamuzi wake wa kususia uchaguzi huo, huenda ukawa mwisho wa serikali hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema chama chake kiko tayari kuunda na chama chochote kama kitakamilisha mashariti ya kikatiba.
Alisema SUK si ya CCM na CUF bali kila chama kina haki kushiriki katika kuunda serikali. Alisema muhimu chama kikamilishe mashariti ya Katiba ya Zanzibar.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ali Mazrui, alisema hatima ya SUK iko mikononi mwa Wazanzibari wenyewe.
Hata hivyo, alisema msimamo wa CUF uko pale pale wa kutoshiriki uchaguzi na kwamba kama SUK itakufa, wahusika wakuu watakuwa CCM.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood Mohamed, alisema njia nzuri ya kulinda SUK ni kwa CUF kufuta msimamo wake na kukubali kushiriki uchaguzi wa marudio.
Alisema kuwa kama vyama vingine vitashindwa kupata viti na wagombea wao kuvuka shariti la katiba la kupata asilimia 10 ili kutoa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, CCM italazimika kuunda serikali peke yao.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment