Suala la kudai fidia pindi ardhi ya kijiji inapotwaliwa linaongozwa na sheria ya ardhi ya vijiji ya 1999. Fidia ni haki pale ardhi ya kijiji inapotwaliwa. Ziko sababu zinazoweza kuifanya serikali kutwaa ardhi ya kijiji kwa mfano kupisha miradi ya maendeleo, kupisha uwekezaji kwa manufaa ya kijiji husika na taifa zima, halikadhalika kuondoka katika eneo ambalo limetangazwa kuwa hatarishi kwasababu za kijiografia au nyinginezo.
Yumkini kwasababu yoyote katika hizi fidia hubaki haki ya msingi kwa mwananchi.
1.MTAPATAJE TAARIFA YA KUDAI FIDIA.
Sheria ya ardhi ya kijiji inamtaka Kamishna wa ardhi kutoa taarifa kuhusu fidia kwa halmashauri ya kijiji pamoja na watu wote wanaokalia ardhi inayotakiwa kutwaliwa.
Huu ni wajibu kwa kamishna na kufanya hivyo hakutegemei hisani yake. Taarifa hiyo itatolewa katika fomu maalum na itakuwa ikieleza eneo rasmi linalotakiwa kutwaliwa huku ikiitaka halmashauri ya kijiji na watu wote watakaoathirika kuleta malalamiko ya fidia pale fomu inapoelekeza.
Hii ina maana hata kama mwanakijiji haijui haki yake ya kudai fidia basi fomu hiyo itatakiwa imweleze kuwa una haki ya kudai fidia na madai yako yapelekwe sehemu fulani.
2. MUDA WA KUWASILISHA MADAI YA FIDIA.
Baada ya halmashauri ya kijiji pamoja na wahanga wanaotakiwa kuondolewa kujaza fomu ya fidia kwa ukamilifu basi madai yao yatatakiwa kuwasilishwa sehemu ambako fomu hiyo imeelekeza. Maombi yatatakiwa yawasilishwe ndani ya siku sitini ( 60).
Siku hizo sitini zinaanza kuhesabika tangu siku mlipopokea taarifa ya nia ya kutwaliwa ardhi yenu. Siku ambayo mnaletewa taarifa na fomu ya fidia ndiyo siku zinapoanza kuhesabiwa.
Ni muhimu kuhakikisha madai yanapelekwa ndani ya muda kwasababu muda huo ni wa kisheria na hivyo kuwa na athari mbaya ukipita.
3. MSAADA WA KUTAYARISHA MADAI YA FIDIA.
Suala la kutayarisha madai ya fidia ni la kisheria zaidi. Sheria ya ardhi ya vijiji inasema kuwa afisa mteule kwa maana ya afisa aliyeteuliwa na serikali kushughulikia suala la ardhi yenu inayotwaliwa ndiye atakayetoa msaada\mwongozo kwa halmashauri ya kijiji pamoja na wahanga wanaoondolewa katika maeneo ili kuandaaa madai ya fidia.
Madai ya fidia ni nyaraka maalum na ya kisheria hivyo si jambo ambalo kila mtu anaweza kuandaa. Kwahiyo suala la msaada wa kuandaa madai ya fidia ni jukumu la kisheria alilonalo afisa anayeshughulikia kutwaliwa eneo lenu.
4. KUKUBALI KULIPWA FIDIA.
Kwa mujibu wa sheria kamishna wa ardhi ndiye mwenye mamlaka ya kukubali malipo ya fidia baada ya madai kuwasilishwa kwake. Hata hivyo pamoja na kuwa mtakuwa mmeelezwa haki yenu ya kudai fidia bado kamishna anaweza kukataa madai yenu na kuamuru kuwa hakutakuwa na malipo ya fidia.
Hii hutokana na sababu mbalimbali za kisheria mojawapo ikiwa ni wananchi kuwa wameingia katika ardhi ambayo imezuiwa. Ikiwa waliingia baada ya ardhi hiyo kuwa imezuiwa kukaliwa basi uwezekano wa maombi yao ya fidia kukataliwa ni mkubwa.
Aidha, Kamishna atatakiwa kutoa majibu ya kukubali au kukataa fidia ndani ya tisini ( 90) toka siku alipopokea maombi ya madai yenu ya fidia. Hivyo ni muhimu kujua kuwa mnapokuwa mmepeleka madai ya fidia kama ilivyoelekezwa hapo juu basi hesabuni mpaka siku tisini halafu kama hamjajibiwa ni wajibu wenu kufuatilia na kujua kulikoni.
Zisipite siku tisini pasi na majibu yoyote halafu mkakaa kimya bila kufuatilia. Hii ni kutokana na athari za kisheria zinazoweza kuwakuta iwapo muda utapita.
5. KULIPWA FIDIA BAADA YA SIKU 21.
Ikiwa maombi ya fidia yatakubaliwa basi kamishna atatoa taarifa kwa Waziri mwenye dhamana akimueleza kukubali kulipwa kwenu fidia na ndani ya siku ishirini na moja ( 21) tangu waziri apokee taarifa, malipo ya fidia kwa wahanga inabidi yatoke.
Kwa ufupi huo ndio utaratibu wa fidia kwa ardhi ya kijiji.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment