NGO ni kifupi cha neno Non Government Organisation. Kwa Kiswahili neno hili humaanisha shirika lisilo la kiserikali. Kawaida serikali huwa ina mashirika yake, kwa mfano shirika la bima, shirika la nyumba,shirika la umeme,mashrika ya vyakula n.k.
Tunapozungumzia NGO maana yake ni kuwa ni mashirika ambayo kwa namna yoyote ile serikali haihusiki na umiliki wake. Ni mashirika ambayo humilikiwa na watu binafsi. Serikali huweza kushirikiana nayo tu lakini si kuyamiliki.
Taratibu za uanzishaji, usajili na uendeshaji huratibiwa bayana na Sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali Na 24, 2002.
1.YAPI YAWE MALENGO YA KUANZISHA NGO.
Malengo makuu ya kuanzisha NGO yawe ni kusaidia makundi au kundi maalum katika jamii. NGO sio shirika la biashara. Sio kampuni ambayo muanzishaji wake hutaraji kutengeneza faida. NGO ni shirika la hisani. Ni shirika la kujitolea kusaidia makundi jamii. Usitegemee kuanzisha NGO kwa ajili ya kutengeneza faida ya fedha.
2. MGAWANYO WA USAJILI WA NGO.
Usajili wa NGO umegawanyika katika makundi makuu manne. Kwa mujibu wa sheria mgawanyo huu umelenga maeneo ya kijiografia. Hata hivyo ada za usajili na mambo mengine muhimu katika usajili hutegemea mgawanyo huu.
Kwanza kuna mgawanyo wa usajili wa ngazi ya wilaya. Usajili wa aina hii huiwezesha NGO kufanya shughuli zake ndani ya mipaka ya wilaya. Husajiliwa hapohapo wilayani na hufanya kazi zake ndani ya mipaka hiyo.
Pili usajili ngazi ya mkoa. Huu huhusisha usajili ngazi ya mkoa na mipaka ya kazi itakuwa ni ndani ya mkoa husika.
Tatu usajili ngazi ya taifa ambao hufanyika makao makuu na mipaka ya kazi ni taifa zima. Nne ni usajili ngazi ya kimataifa ambao huiwezesha NGO kufanya kazi zake katika taifa zaidi ya moja.
3. WAPI UKASAJILI NGO.
Kwa ngazi ya wilaya nenda makao makuu ya wilaya yako, na ulizia afisa maendeleo ya jamii. Hawa ndio huhusika na usajili. Halikadhalika ngazi ya mkoa utaenda makao makuu ya mkoa wako ndipo usajili utakapofanyika.
Aidha kwa ngazi ya taifa usajili hufanyika makao makuu ya wizara kwa msajili wa NGO. Kwa sasa wizara husika ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto. Wasajili wa ngazi zote hupata mamlaka ya kusajili kutoka kifungu cha 22(1) cha sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali.
4. VITU GANI VINATAKIWA KATIKA USAJILI.
( a ) Katiba ya NGO. Hizi hutakiwa nakala tatu zilizojaladiwa( binding).
( b ) Maelezo binafsi ya viongozi watatu wa NGO. Mwenyekiti, Katibu, na mhazini. Maelezo binafsi ni wasifu( CV) pamoja na picha mbili za kila mmoja.
( c ) Mukhtasari wa kikao cha kuanzishwa kwa NGO ukienda sambamba na majina na sahihi za waanzilishi.
( d )Fomu ya maombi ya usajili iliyojazwa ( NGO FORM NO 1). Hii hupatikana kwa msajili. Itatakiwa kubandikwa ushuru wa stempu wa Tshs 1500/=.
( e ) Barua ya utambulisho kutoka kwa afisa maendeleo ya jamii wa wilaya, mkoa husika.
( f ) Taarifa nyingine yoyote ambayo msajili anaweza kuomba kutoka kwako.
5. ADA ZA USAJILI NI KIASI GANI.
Ngazi ya wilaya 80,000/=, ngazi ya mkoa 100,00/=, ngazi ya taifa 115,000/= na kimataifa dola za kimarekani 350.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment