Maiti ya mtoto Mbongo yazuiliwa India kwa deni


Dennis Mwalongo


Marehemu Abel Revocatus Machanga enzi za uhai wake.

Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI
DAR ES SALAAM: Dunia katili! Baada ya kuteseka kwa muda mrefu kufuatia ugonjwa uliompata Abel Revocatus Machanga (pichani) hatimaye amefikwa na mauti Desemba 31, 2015 akiwa kwenye matibabu nchini India, kibaya zaidi, maiti yake imezuiliwa kuletwa Tanzania kutokana na deni analodaiwa hospitalini hapo.

Abel alianza kuugua Novemba 2014, kipindi hicho akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Biashara Dar (CBE), ambapo alivimba macho na kutokeza nje, akapoteza uwezo wa kuona huku pia akipumua kwa shida.

Alianza kutibiwa Hospitali ya Macho ya CCBRT, Dar lakini ikashindikana, akapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako hali ilizidi kuwa mbaya, Novemba 24, 2015, ndugu wakampeleka India kwa matibabu.


Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa mujibu wa baba mzazi, Revocatus Machanga, baada ya kufika India kwa fedha zilizochangwa na wasamaria wema, wakiwemo wasomaji wa Gazeti la Uwazi (habari ya ugonjwa wake ilichapishwa na gazeti hili), alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Columbia Asia nchini humo ambako alifanyiwa vipimo upya.

“Alibainika ana ugonjwa uitwao Amelobeblastoma. Pia aligundulika ana matatizo mengine yakiwemo ya wadudu kwenye meno, pua, macho, kichwani kwenye ubongo na kwenye mapafu.

“Hospitalini hapo alifanyiwa upasuaji wa kwanza na madaktari wakafanikiwa kuondoa asilia 60 ya uvimbe. Alipopata nafuu alifanyiwa upasuaji wa pili, akaondolewa asilia 40 ya uvimbe. Hali yake ikaendelea vizuri ingawa alilazimika kulazwa ICU (Chumba cha Wagonjwa Mahututi) kwani bado alikuwa hawezi kupumua vizuri.”

“Hata hivyo, Desemba 31, 2015 majira ya mchana, mwanangu alifikwa na mauti baada ya shinikizo la damu kushuka kupita kiasi,” anasimulia kwa huzuni mzee Machanga.

Mzee huyo aliendelea kusema fedha walizochangiwa na wasamaria wema Tanzania hazikutosha kutokana na kubainika matatizo mengine na ndiyo hali iliyosababisha Abel aage dunia na kuacha deni la shilingi milioni 35 hospitalini hapo. Achilia mbali gharama za mtu aliyekuwa akimuuguza ambaye ni kaka yake, Christopher Machanga.

Mzee Machanga aliendelea kusema kwamba kutokana na deni hilo, hati za kusafiria za marehemu na ya kaka yake zinashikiliwa na uongozi wa hospitali hiyo huku pia wakikataa kuutoa mwili wa marehemu kwa maelezo kwamba, mpaka deni hilo litakapolipwa ndipo watakapopewa.

“Mpaka leo (juzi Jumapili), mwili wa mwanangu bado upo mochwari India zikiwa zimepita siku 17 tangu alipoaga dunia. Hakuna dalili za sisi kama familia na wanandugu kuchanga mpaka kiwango hicho kitimie kwa sababu uwezo wetu ni mdogo.

“Niliandika barua ya kuomba msaada wa kusaidia fedha za matibabu kwenda kwa katibu mkuu wizara ya afya na ubalozi wa Tanzania, India lakini nilijibiwa kuwa, kwa sababu mwanangu hakusafirishwa kwa taratibu za serikali, ikiwemo kupata rufaa kutoka Muhimbili na kuidhinishwa na wizara, wasingeweza kunisaidia lolote.”

“Nawaomba Watanzania kama mlivyoweza kunisaidia mara ya kwanza, mnisaidie pia kwa hali na mali ili maiti yake iletwe tumzike kwa heshima zote hapa nyumbani Tanzania,” anahitimisha baba wa marehemu, mkazi wa Ukonga- Mombasa, Dar.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipotafutwa kwa njia ya simu Jumamosi iliyopita hakupatikana.

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii, anaweza kuwasiliana na baba wa marehemu kwa simu namba 0713 275740, 0752 275740 na 0784 275740. Kutoa ni moyo! Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: