Kwanza nikutakie heri ya mwaka mpya 2016 wewe msomaji wa safu hii ya kujuzana mambo mbalimbali yanayotokea katika michezo hasa soka. Mengi yamepita katika mwaka 2015, tumshukuru Mungu kuiona 2016.
Bila kuchelewa leo mada yangu inahusu kauli ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwamba, klabu zisiilaumu TFF endapo watapata matatizo ya kutopata leseni kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kutokidhi vigenzo vya kushiriki michuano yake.
Baadhi ya vitu ambavyo klabu inatakiwa kuwa navyo ili kupata leseni hiyo ni kuwa na uwanja binafsi wa mazoezi na angalau kuwa na timu moja ya vijana inayoeleweka.
Tunapozungumzia uwanja wa mazoezi ni ule ambao timu inaweza kufanya mazoezi yake muda wowote bila kuingiliana na klabu nyingine na uwe upo kisheria kabisa siyo ubabaishaji.
Malinzi siku chache zilizopita katika mkutano wake na waandishi wa habari alisisitiza kwamba, TFF isilaumiwe endapo klabu yoyote itaondolewa katika michuano inayosimamiwa na CAF kutokana na kutokidhi vigezo vya kupata leseni.
Nionavyo ni kwamba, Malinzi anakimbia jukumu lake kwani klabu zinazoshiriki michuano ya CAF kutoka Tanzania Bara ni mbili tu Yanga na Azam FC. Yanga inashiriki Ligi ya Mabingwa na Azam itacheza Kombe la Shirikisho.
Kwa nini Malinzi asizikomalie klabu kuhusu kutimiza masharti ya kupata leseni mapema mpaka anapoibuka hivi sasa na kutoa onyo hilo? Kuna kitu amekiona mbele na hivyo anaanza kujihami mapema asionekana mbaya.
Ukitazama kanuni za Ligi Kuu Bara, kuna sehemu ya klabu kupatiwa leseni na ili upate leseni ni lazima uwe na vitu nilivyotaja hapo juu yaani uwanja wa mazoezi na timu ya vijana inayoeleweka.
Sasa kwa nini TFF inaziruhusu timu kucheza ligi kuu huku zikiwa hazijatimiza masharti ya leseni? Upuuzaji wa vigezo vya leseni ulianza kwa TFF kwa kuziogopa timu vigogo hasa Simba na Yanga na kuziacha ziendelee kucheza ligi bila ya kutimiza masharti hayo.
Naamini kama TFF ingekuwa makini na kuzikomalia Yanga na Simba kutimiza masharti hayo ya kupata leseni leo hii Yanga ingekuwa imetengeneza pale Kaunda na Simba ingekuwa tayari ipo Bunju.
Tatizo lililopo ni TFF kuruhusu mambo kufanyika kienyeji bila kufuata kanuni zinasemaje, leo hii kuna michuano ya Kombe la Shirikisho (Kombe la FA), hapo timu za Ligi Daraja la Pili, la Kwanza na Ligi Kuu zinachuana kupata timu moja itakayocheza Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018, lakini bado hakuna kinachoeleweka kuhusu ishu ya leseni au kukidhi mahitaji ya CAF.
Chukulia mfano, timu ya daraja la pili inachukua ubingwa na kupata nafasi hiyo ya CAF, je, itakuaje linapokuja jambo la kukidhi mahitaji ya CAF? TFF itatoa tena tamko la kutohusika endapo timu itazuiwa kushiriki michuano hiyo.
Kwa kutoa kauli kwamba wasilaumiwe endapo klabu itaondolewa katika michuano ya CAF ni sawa na kukimbia lawama, kwani kabla ya CAF ni TFF iliyokuwa na mamlaka ya kuzizuia klabu hata kucheza ligi kuu kwa kutokidhi mahitaji ya kupatiwa leseni.
Maofisa wa CAF siyo wanaokuja kuzikagua klabu, bali ni TFF yenye wajibu huo hivyo kabla ya CAF kufikia uamuzi wowote TFF ilipaswa kuwa ya kwanza kuzifungia klabu kutocheza ligi kuu kwa kutokidhi vigezo.
Lakini kutokana na soka letu kuendeshwa kisiasa zaidi, TFF inashindwa kuthubutu kutoa adhabu kwa klabu za ligi kuu tena bila sababu ya msingi na sasa wanaibuka na kauli za kujihami.
Malinzi na timu yake asikimbie majukmu yake kwani alipaswa kulitazama mapema ili jambo na kuzipa onyo klabu na ikiwezekana kuzizuia kucheza ligi hadi zitimize masharti hayo.
Kwa jinsi mambo yanavyoenda, adhabu ya CAF inaweza kutua Yanga kwani Azam tayari ina viwanja vyake vya mazoezi hadi mechi ndiyo maana Malinzi anaanza mapema kujivua ili asionekane mbaya.
Hapa Malinzi hawezi kuepuka lawama kwani aliacha mwenyewe timu ikacheza hadi ligi kuu bila ya kukidhi mahitaji ya leseni na sasa anaona CAF ipo makini ndiyo anataka kukwepa lawama.
Tuwe wakweli tu kwamba, klabu ikizuiwa kucheza mechi za CAF, itakayolaumiwa ni TFF na siyo mtu mwingine.
Niwatakie kheri ya mwaka mpya 2016.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment