Katumbi amrudisha Manji Yanga



Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji. 
TP Mazembe ndiyo klabu bora zaidi Afrika. Ubora wa klabu hiyo unatokana na miundombinu yake pamoja na utajiri na uwekezaji wa bilionea Moise Katumbi.
Tajiri huyo ameiwezesha timu hiyo kusajili wachezaji bora wa ndani na nje ya Afrika ambao pia wamemuwezesha kucheza Klabu Bingwa ya Dunia kwa mara mbili.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, ametamka kwamba atagombea nafasi yake kwa mara nyingine na ni lazima ahakikishe Yanga inafanya kitu kipya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kama Mazembe ya Katumbi na haoni sababu ya kushindwa.
Manji amesisitiza kwamba tayari Yanga ina wachezaji wa maana na aliowanunua kwa fedha nyingi kama anavyofanya Katumbi, lakini ambacho bado ni kutengeneza uwanja wa maana wa Yanga pamoja na kuhakikisha inatisha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hata zaidi ya Mazembe.
Kiongozi huyo amesisitiza kwamba atatimiza mipango hiyo kwa kugombea kwa mara nyingine ndani ya Yanga na vilevile kutumia nguvu yake ya kisiasa kuishawishi serikali ili kuharakisha ujenzi wa uwanja huo na kuiimarisha Yanga kiuchumi.
Akitumia dakika 40 katika kueleza sababu ya kujiuzulu kwa Katibu wake Dk. Jonas Tiboroha Manji alisema: “Nitagombea, kama kuna mtu anataka kugombea asiogope aje tu tushindane mimi siogopi changamoto, lakini hata kama nikishinda sidhani kama nitamaliza kipindi changu, kuna mambo machache hasa hili la uwanja ndiyo ninalotaka kulipigania.
“Hatuwezi kufanya vizuri katika mashindano haya makubwa kama hatuna uwanja hata wa mazoezi, naona kuna watu wamejenga kule mbele lakini Yanga tulizuiwa hiyo si sawa.”
“Nimeweka dhamira ya uchaguzi ufanyike kwa haraka, katika maisha yangu sijawahi kutanguliza au kupigania cheo, ndani ya Yanga maendeleo yanaonekana lakini wapo watu ndani ya Yanga wanaona mandeleo yapo kwake. Basi tuache demokrasia itawale, lakini na mimi nitatangaza kugombea tena nafasi hiyo.”
ISHU YA TIBOROHA
Manji ametoa ufafanuzi juu ya sakata la kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Dokta Jonas Tiboroha. Miongoni mwa mambo aliyozungumza mwanasiasa huyo ni pamoja na suala ya Tiboroha kuipotosha Kamati ya Utendaji kuhusiana na sakata la Haruna Niyonzima.
NIYONZIMA
“Baada ya kuupitia uamuzi wa Kamati ya Nidhamu kuamua sababu kuvunja mkataba kati ya klabu Yanga na mchezaji Haruna Niyonzima, nilihisi kulikuwa kuna kasoro hasa kwa mchezaji anayelipwa mshahara wa Sh6 milioni anaweza vipi kupuuzia maisha yake na kuanzisha mgogoro usiokuwa na tija kwa maisha ya kipato,” alisema.
“Niliamua uchunguzi wa ndani ufanyike katika suala hilo zima na mwisho, Jonas Tiboroha alibainika kuwa hakuwasilisha ushahidi wa mawasiliano sahihi kwa Kamati ya Nidhamu kuhusiana na Haruna Niyonzima, hali iliyosababisha kamati kuchukua uamuzi ambao haukuwa sahihi kwa sababu; Kulifanyika mambo ambayo hayakuwa sahihi, mfano barua za Niyonzima kutoka kwa Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) ambazo zilitumwa TFF na kupokelewa kama ambavyo Azam FC walipokea ya mchezaji wao kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wao. Lakini barua ya Niyonzima kuja Yanga, ilionekana haikupokewa kama ilivyokuwa kwa barua yake ya utetezi na ile ya kuomba radhi alizoandika, nazo zilipokewa lakini hazikuwasilishwa kwenye Kamati ya Nidhamu na hili, mhusika ni Tiboroha.”
Kamati ya Utendaji (Excom), bada ya kupitia kwa kina iliona uamuzi iliouchukua haukuwa wa haki kutokana na kupotoshwa na Tiboroha.”
MAPATO
“Ndani ya miezi yake 12 ya uongozi amechangia kushuka kwa kasi kubwa kwa mapato ya klabu huku matumizi ya klabu yakipanda mara nne zaidi kutoka Sh milioni 500 kwa mwaka hadi sasa takriban Sh2 bilioni.
GHANA
“Wakati Fifa ilipoialika Yanga kwenye semina ya mafunzo iliyofanyika Ghana, Tiboroha alijichagua mwenyewe asafiri kwa niaba ya klabu bila kuitaarifa kamati, halafu akachukua “Cheti cha ugonjwa” na kukiwasilisha kwa mwajiri wake Yanga ili apate nafasi ya kusafiri kwenda nchini Ghana. Kujichagua yeye mwenyewe, ilikuwa ni kutofuata weledi.
DAKTARI
“Daktari (jina linahifadhiwa) aliajiriwa kwa ajili ya mechi dhidi ya Mgambo likiwa ni pendekezo la Tiboroha, lakini baadaye Kamati ya Mashindano (baada ya kuwa imesababisha tatizo ndani ya Klabu), iligundua daktari huyo alikuwa ni mwanachama tena mwenye kadi wa Simba, akaondolewa pia.
NGOMA
“Ngoma alipewa taarifa na Tiboroha kwamba anatakiwa kwenda kufanya majaribio na klabu moja nchini Uturuki. Tiboroha alifanya hivyo akijua Ngoma alikuwa anakwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, mbaya zaidi hakuwa amewasiliana na kamati kabla kumfahamisha mchezaji.
“Baadaye Kocha Mkuu (Hans Pluijm), alilalamika kwamba kufanya vile ilikuwa ni kuondoa morali ya mchezaji, kocha alisema, Ngoma alicheza chini ya kiwango katika michuano hiyo, akiamini Yanga inamzuia kusonga mbele kimaisha.”
“BDF ya Botswana iliazima dola 5,000(Sh10.7 milioni) ambazo hadi sasa hazijarejeshwa. Kamati iligundua taarifa kuhusiana na deni hili, imekuwa ikifichwa na hakuna maelezo mrejesho kuhusiana na hilo kutoka kwa Tiboroha ambaye amekuwa na ukaribu na wahusika kutoka Botswana.”
AKAUNTI
“Hakufuata ushauri aliopewa na wataalamu wa TRA, hali iliyosababisha akaunti za Yanga kufungwa, hivyo mimi kulazimika kuanza kutoa fedha zangu za mfukoni katika uendeshaji wa Klabu kwa kipindi chote na wakati huo wachezaji walikuwa wakidai mishahara na tuko katikati ya msimu.
KUJIUZULU
“Nilitoa ushauri kwamba vizuri akachukua hatua ya kujiuzulu mara moja na huenda ingekuwa vizuri aeleze ana matatizo ya kifamilia pia kiafya, lengo ilikuwa ni kumpa nafasi ya kuachana na Yanga kwa amani, lakini nilimtaka ahakikishe zile fedha tunazowadai BDF kutoka Botswana, mara moja zinawasilishwa klabuni na baada ya hapo, rasmi atakuwa amejiondoa.Tiboroha alikubaliana na hilo na kuandika barua ya kujiuzulu aliyoiwasilisha Januari 22, 2016.”
UTEUZI MPYA
Baraka Deusdedit atashikilia nafasi hiyo ya Katibu Mkuu wa klabu. Omar Kaya atachukua majukumu yanayohusiana na wanachama wa klabu.
CHANJI
Manji amepingana na wanachama wanaomshinikiza kumwondoa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Mhandisi Issac Chanji.
“Chanji? Siwezi kumwondoa. Mimi namjua zaidi kuliko hao wanaosema atoke, nimesikia kwamba wanasema nikikataa nitoke naye lakini mimi nasema kwamba bado ni mtu ambaye natambua uchapaji kazi wake ndani ya hii klabu, anaipenda hii klabu hivyo ataendelea kuwapo.”

UTETEZI
Tiboroha aliliambia Mwanaspoti jana Jumapili kwamba hawezi kujibu tuhuma yoyote kwa kukurupuka mpaka atakapokaa na kuzisoma kwa kina.




Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: