Aliyekuwa
kocha wa Simba, Dylan Kerr ameandika waraka kwa vyombo vya habari na na
mashabiki wa Simba kuelezea mambo mbalimbali yaliyotokea katika klabu
hio ndani ya muda wa miezi sita aliyokaa.
” Wapenzi na Mashabiki wa Simba Sports Club,
Huu ni waraka wangu rasmi na tamko langu la mwisho kwa vyombo vya habari na mashabiki wa Simba Sports Club.
Uongo
mwingi umezungumzwa, na kuna wakati zimetolewa kauli za kuumiza kwenye
vyombo vya habari kunihusu mimi na kazi yangu katika timu ya Simba,
hivyo basi waraka huu utakuwa ni wakujitosheleza juu ya hoja
zilizotolewa.
Ninajisikia vibaya sana kuona nimekuwa na mwisho wa ghafla kiasi katika Klabu hii.
Miezi
sita niliyokuwepo Simba SC iligubikwa na changamoto nyingi za kimwili
na kiakili, lakini pamoja na hayo niliweza kufurahia maisha.
Mashabiki
wa Simba SC na Watanzania wote kiujumla nimeishi nao vizuri,
wamenikarimu na kunifanya nifurahie maisha na kuifurahia nchi nzuri ya
Tanzania.
Nilikuwa
nina mkataba wa miaka miwili na timu ya Simba SC, mkataba ulio bayana
na wa kisheria, “ningehukumiwa kwa nafasi yangu katika msimamo wa Ligi
Kuu ya Vodacom mwishoni mwa msimu 2015-2016 (kushinda lilikuwa jukumu
langu) na utendaji kazi wangu katika ligi ya mabingwa barani Afrika
2016-2017 ambayo tulikuwa na uwezekano mkubwa wa kushiriki”
Katika
mkataba wangu, hakuna mahala palipoainishwa utendaji kazi wangu kwenye
mashindano ya kombe lolote, hata mashindano ya hivi karibuni huko
Zanzibar hayakuelezwa kama moja ya mashindano yatakayopima kazi yangu.
Ninaamini
pasipo na shaka, kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku
tukiwa na uwezekano mkubwa wa kupanda nafasi ya pili au ya kwanza,
nilikuwa mbioni kufikia malengo yaliyowekwa na uongozi wa timu.
Nimekuwa
kwenye fani hii kwa miaka 32, nimecheza ligi kubwa Uingereza na kupata
mafanikio kama mchezaji, lakini kadhalika nimepata mafanikio katika
nyanja ya ualimu wa mpira.
Nina
sifa za kutosha na weledi wa hali ya juu, nina beji za shirikisho la
soka barani Ulaya (UEFA), pamoja na uzoefu mkubwa katika nyanja ya mpira
wa miguu bila kusahau ngazi ya timu ya Taifa.
Mimi
sio aina ya mwalimu anayeweza kufanya kazi huku akiingiliwa na watu
wasioujua mpira, wasio na vyeti, wasio na uzoefu, wasiokuwepo katika
bodi ya mpira wa miguu, ambao sio tu kwamba wanataka kuwa juu ya timu,
bali pia wahusike na majukumu ya kusajili na kufukuza wachezaji na
kimsingi hili haliwezi kuiendeleza timu.
Vilevile,
wimbi kubwa la waalimu walioajiriwa na Klabu ya Simba kwa miaka ya hivi
karibuni inaonesha dhahiri kuonesha mahala tatizo lilipo, Klabu
inatakiwa kufanya maamuzi magumu, pia kubadili utamaduni huu haraka
iwezekanavyo vinginevyo timu hii haitaendelea na badala yake watazidi
kurudi nyuma.
Klabu
nzima ya Simba imekuwa haina kiongozi hata mmoja mwenye cheti cha Mpira
kinachotambuliwa na vyama kama UEFA au CAF, ni kwa mara ya kwanza
kiongozi mmoja tu hivi karibuni amehitimu mafunzo ya awali ya ualimu wa
mpira.
Klabu
hii itazidi kuporomoka kama haitampata na kumteua kiongozi mmoja aliye
na cheti kinachotambuliwa na CAF au UEFA na mwenye uzoefu wa kutosha
katika fani ya mpira ili afanye kazi karibu na mwalimu katika masuala ya
usajili, mipango ya mchezo, maandalizi ya ligi, vifaa vya mazoezi,
mkakati wa kuendeleza soka la vijana na mambo yote yahusuyo ufundi.
Wadhifa
wa “mkurugenzi wa ufundi” ni muhimu sana, wakati CAF ikiendelea
kushughulikia leseni mpya za uendeshaji wa vilabu barani Afrika, Klabu
ya Simba inatakiwa kuhakikisha inakuwa na mfumo sahihi wa kiutawala ili
kuweza kufuzu kuipata leseni hii.
Ingawa
nimekutana na matatizo ya kutolipwa mishahara, kwangu mimi na kwa
wachezaji wangu hasa mwezi Novemba na Desemba, niliendelea kufanya kazi
yangu na nilijitoa kwa moyo mmoja.
Nimefanya
kazi katika medani ya mpira wa miguu kwa maisha yangu yote, naelewa
mambo kama haya hutokea, lakini mimi na wachezaji tulijikuta
tunalazimika kuvumilia manyanyaso kutoka kwa baadhi ya viongozi, siamini
kama ilikuwa ni sahihi na sio weledi wa kazi.
Ni
kweli, sote hatukupendezwa na mashindano ya hivi karibuni mjini
Zanzibar, kupoteza mchezo katika hatua ya nusu fainali, lakini ikumbukwe
kwamba lengo langu lilikuwa wazi na mamlaka yangu yanajulikana, Ligi
kuu ilikuwa muhimu zaidi na tulitumia mashindano ya Zanzibar kukitazamia
kikosi kizima na kuwapa nguvu mpya wachezaji ili tuweze kukabiliana na
ligi na hatimae kufikia mafanikio.
Kusikia
kwamba “timu haikuwa fit” hiki ni kichekesho, kucheza mechi mfululizo,
kusafiri kwa basi zaidi ya saa 25, ni kweli wote tulikuwa tumechoka
lakini “kutokuwa fit” ni hoja ya mzaha kabisa.
Mwalimu
wa viungo hakufukuzwa, isipokuwa mkataba wake wa miezi mitatu
ulipokwisha hakuongezewa, na kutokana na tabia zake katika masuala kadha
wa kadha haikushangaza kutokuwa nae.
Klabu
ya Simba haitakiwi kufumbia macho baadhi ya viongozi wanaoichafua
heshima ya Klabu, ambao kwa makusudi wanamuua kuitia aibu timu hii kwa
kutofuata taratibu zinazotakiwa hasa wanapoiwakilisha timu.
Jambo
la msingi zaidi ambalo nataka kuliweka sawa ni kuhusu mwalimu wa viungo
mbalo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara, wapenzi na mashabiki wa
Klabu Simba ni lazima wafahamu ukweli kuhusu mwalimu huyu.
Nilipendekeza
kwa uongozi waalimu wengi wa viungo wenye utalaamu na sifa za kutosha,
walio na beji za UEFA na CAF katika Nyanja ya viungo (lakini
hakupatikana), ingawa hata mimi nimefuzu katika eneo hili kwa maana ya
vyeti vyangu vya UEFA, na ningeweza kufundisha bila mwalimu wa viungo na
hili lingesaidia sana kuokoa fedha za Klabu zisiende bure.
Niwe
mkweli tu, baada ya mazoezi yote ya msingi tuliyofanya wakati
tunajiandaa kuanza Ligi kuu, hatukuhitaji kuwa na mwalimu wa viungo kama
sehemu ya waalimu wa timu hasa ukizingatia ratiba ilivyokuwa, ni
michezo miwili tu kwa juma.
Nimekuwa
nikiusumbua uongozi kuhakikisha nyasi za uwanja wa Taifa zinakatwa ili
kuhakikisha mtindo wetu wa upigaji pasi unaendana na hali ya uwanja,
mtindo ambao mimi na jopo langu tulikuwa tunajaribu kunamaliza maneno
juu ya wachezaji.
Urefu
wa nyasi kwa mara nyingine ulikuwa hatari sana kwa wachezaji , ambao
wamekuwa wakipata majeraha makubwa, ni jukumu la Klabu yeyote ya mpira
inayoendeshwa kiuweledi kuhakikisha inatilia maanani masuala muhimu hasa
linapokuja la ustawi wa timu kwa maana ya wachezaji.
Kuwa na msaada kwa mwalimu wa timu na kwa wachezaji, ni pamoja na kuhakikisha masuala madogo madogo yanayoombwa yanatekelezwa.
Lakini
pia nimekuwa nikiomba katika michezo yetu tutumie mipira bora na halisi
ya Addidas badala ya mipira isiyo na kiwango bora, lakini baadhi ya
viongozi walitulilazimisha kutumia mipira isiyo na ubora ambayo hata
wachezaji waliichukia na hawakutaka kuitumia, lakini ilitulazimu kwani
viongozi wale walifanya ili kutimiza matakwa ya mtu mmoja.
Inashangaza
sana kuona baada ya mimi kuondoka tu, nyasi za uwanja wa Taifa
zimekatwa na mipira halisi ya Addidas imeanza kutumika.
Nasema Bravo Simba!!!!
Kama ambavyo Ce Ce Peniston aliimba “finally”
Lakini najiuliza kwanini iwe sasa hivi?? Baada ya michezo 14 ya msimu huu.
Tuachane na hayo, binafsi napenda kusema haya yafuatayo;-
Niwashukuru
mashabiki wote na wanachama wa Simba Sports Club ambao mliniunga mkono
na kunijali, nisingeweza kumridhisha kila mmoja wetu, lakini huo ndio
mchezo wa mpira ulivyo.
Wanasimba ni watu wenye mapenzi na timu yenu na mnajitolea sana.
Pia
napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mashirika yasiyo ya
kiserikali na vituo vya misaada ambavyo wachezaji na wafanyakazi wote wa
Klabu ya Simba tulivitembelea sehemu mbalimbali ya nchi nikiwa kama
Kocha mkuu wa Klabu, nilifarijika na kufurahi kufika maeneo hayo.
Shukrani
kwa Dereva wangu Dula, benchi la ufundi, na kikosi maridadi cha
wachezaji wote wa Simba SC ambao walifanya kazi kwa kujituma sana,
nitawakumbuka sana.
Kwa
Rais wa Klabu ya Simba, namshukuru kwa dhati kwani mara zote amekuwa
akiniunga mkono, nashukuru kwa nafasi uliyonipatia na pia shukrani zangu
ziende kwa baadhi ya viongozi ambao walijaribu kuniunga mkono.
Kwa
kuongezea tu, naweza kusema Rais wa Simba SC aliagiza nilipwe
mishahara yangu, na ninathibitisha nimelipwa stahiki zangu zote kama
tulivyokubaliana katika mkataba.
Nimeiacha
timu katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, nautazama muda wangu
ndani ya Simba kwa hisia mchanganyiko, nilikamilisha nusu ya kazi.
Mwisho kabisa kwa wanasimba na watanzania wote, niwatakie maisha mema na kila la kheri.
Ahsanteni sana.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment