Ziara hizi za kushtukiza, khaa!



Nikaona nijipange na mimi nifanye ziara kadhaa za kushtukiza katika sehemu mbalimbali zinazonihusu.Nikaona nianze na ziara ya kushtukiza pale shuleni kwa huyu mwanangu, maana kila siku anakunywa chai na kuondoka na daftari zake na mie sijawahi kwenda shuleni kwao tangu nilipomuandikisha shule mwezi Januari.
Nilifika shuleni na kumuona mwalimu mkuu, ambaye alianza kutetemeka nilipomuambia kuwa nimekuja pale kwa ziara ya kushtukiza, sijui alidhani mi ni mmoja wa mawaziri wapya, maana nilimuona jasho linamtiririka ghafla.
Akanikaribisha katika ofisi yake iliyokuwa na vitabu kila kona na kuita walimu wote na kunitambulisha kuwa ni kiongozi nimekuja kwenye ziara ya kushtukiza. Nilipojitambulisha kuwa ni mzazi, walimu wote nikawaona wanaanza kupumua kwa raha.
Nikawaambia kuwa mimi nina mwanafunzi pale na nilifanya ziara ya kushtukiza kujua maendeleo yake. Baada ya mwalimu mkuu kusaka jina la mwanangu naye akaniambia, “Mzee huyu mtoto hajaja shule mwezi wa tatu sasa, tulijaribu kukutafuta ikashindikana, hatujui yuko wapi!” Jasho likaanza kunitoka mimi, yule mtoto kila asubuhi nampa nauli anaenda shule na mara nyingi ananiomba michango kumbe hata shule haji.
Niliondoka bila kuaga presha ikiwa juu. Nikaona niende kwenye genge la mke wangu naye nikamfanyie ziara ya ghafla nimhadithie mambo ya mwanae, nilipofika pale nikakuta kuna mdada mwingine anauza genge. Nikamsalimu na kumuuliza mwenye genge nitampataje, jibu lake lingeniua kama ningekuwa si mkakamavu;
“Mume wake kaja kumchukua na gari wameenda kununua shamba Bagamoyo.” Nikaondoka nimechanganyikiwa, nikajuwa hapa dawa yangu moja tu, nayo ni Sabrina, mtoto wa Kinyaturu pale ambapo nikipata maudhi huwa naenda kubembelezwa. Nikatwanga mguu kwa Sabrina naye nikamfanyie ziara ya ghafla ili anipoze moyo.
Nilipogonga mlango wa chumba chake akatoka mbaba wa miraba minne, akanisalimia kwa upole; “Salama kaka unasemaje?” Jibu likanitoka “Samahani miye nilimkopesha huyu dada wa chumba hiki vitenge, nilikuja kuuliza kama ameshapata hela yangu.” Ziara za kushtukiza zinataka moyo wa chuma jamani!


Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: