Uongozi wa timu ya soka ya Panone FC ya mkoani Kilimanjaro uko kwenye mazungumzo na kocha Felix Minziro ikiwa ni sehemu ya kuboresha benchi lake la ufundi kujiandaaa na mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza ngazi ya taifa.
Tarifa ya kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake Maili Sita wilayani Hai zinadai uamuzi wa mabadiliko hayo unatokana na benchi la ufundi la sasa linaloongozwa na kocha Atuga Manyundo kushindwa kuipatia timu hiyo matokeo mazuri katika michezo ya ligi hiyo ambayo iko mapumzikoni.
Ujio wa kocha Minziro aliyekuwa akikinoa kikosi cha timu ya JKT Ruvu kinachoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara unatarajiwa kuwa suluhu ya changamoto zinazoikabili timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kucheza mpira na uongozi kama mwalimu.
Panone FC imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya kiuongozi hali iliyoplekea baadhi ya viongozi wa chama cha soka mkoa wa Kilimanjaro KRFA pamoja na wadau wa soka kuisusa timu hiyo.
Hata hivyo baadhi ya wadau baada ya kusikia ujio wa mlinzi huyo mahiri wa zamani wa klabu ya Yanga maarufu kama baba Isaya, wametoa maoni yao kuwa kwasasa watu wategemee kuiona Panone FC mpya. Mmoja ya wadau hao ni Godfrey Madegwa amesema jukumu la pili lililopo mbele baada kupatikana kocha Minziro, ni kutafuta wachezaji bora wakati huu wa dirisha dogo la usajili watakaorejesha furaha kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na siyo wachezaji wa kukaa benchi.
Msemaji wa klabu ya Panone FC Kassim Mwinyi amethibitisha juu ya ujio wa kocha huyo na kwamba mazungumzo yanaendelea na muda si mrefu atatia saini na Panone FC kwa ajili ya kuitumikia hivi karibuni.
Ikumbukwe kocha Felix Minziro alikuwa ni miongoni mwa makocha waliokuwa wakipigiwa chapuo kurithi mikoba ya aliyekuwa kocha wa Yanga Charles Boniface Mkwasa anayeitumikia timu ya taifa kwa sasa.
Hivi karibuni Minziro alionekana kwenye uwanja wa Chuo cha Bishara na Ushirika mjini Moshi akifatilia mchezo kati ya Panone FC dhidi ya Polisi Dar es Salaam mchezo wa ligi ya Shirikisho (Azam Federation Cup) ambapo Panone FC ilifanikiwa kusonga mbele kwa hatua inayofuata baada ya kuichapa timu ya Polisi Dar es Salaam kwa bao 2-1.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment