BORA MAGURI APOKEE MSHAHARA KIDOGO MAZEMBE KULIKO KUBAKI DAR AICHEZEE YANGA




Na Saleh Ally
Mshambuliaji Elias Maguri amefanikiwa kufunga mabao 10 kwa msimu huu hadi sasa, jambo ambalo linaonyesha ana mwanga mzuri huko aendako.

Maguri amefunga mabao 9 akiwa na klabu yake ya Stand United, bao moja ameifungia Taifa Stars katika mechi dhidi ya Algeria ikiwa ndiyo mechi yake ya kwanza kurejea katika kikosi hicho pia ikiwa ni mara ya kwanza kukichezea chini ya kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.
Maguri aliondolewa Simba huku ikielezwa Kocha Dylan Kerr raia wa Uingereza hakuwa akivutiwa naye. Hiyo ikawa imeifanya Simba kuweka rekodi ya kuwatema washambulizi wake tegemezi kila baada ya msimu mmoja.
Ilifanya hivyo kwa kumtema Amissi Tambwe na kusema Kocha Patrick Phiri hakuwa akimhitaji. Msimu mmoja kabla, Tambwe alikuwa ndiye mfungaji bora.
Maguri amekuwa jasiri baada ya kuamua kwenda Stand United. Kwa alipokuwa amefikia kutoka katika timu ya jeshi na kujiunga na Simba, tayari alikuwa amepiga hatua.

Angekuwa muoga, huenda angeisha kabisa kisoka. Badala yake akaamini uwezo wake na kujiunga na Stand United, sasa ana mabao mengi kuliko washambuliaji wote waliosajiliwa na Simba msimu huu.
Juhudi za Maguri zimefanya awe lulu, tayari kuna klabnu zimeweka wazi zinamhitaji ambazo ni Simba, Yanga na TP Mazembe pia imeanza kumtupia jicho.

Tayari Maguri ameweka wazi msimamo wake kuhusiana na Simba. Kwamba hawezi kujiunga na Simba kwa kuwa hawakuwa waaminifu kwake na walimuondoa katika hali ambayo ilimshangaza na kumkatisha tamaa.
Fainali inabaki Yanga na TP Mazembe. Yanga inakuwa lahisi kumpata kwa kuwa wako naye hapa, lakini swali moja tu. Kuna tofauti kubwa kati ya Yanga na Simba?
Klabu kongwe zenye tabia zinazofanana, ambazo zinaamini zinajua au bora kwa kila kitu na zisizo na uwezo mkubwa sana wa kujali wachezaji wao.
Yanga na Simba, hazina uwezo wa kusikiliza u kufikiria maumivu ya wengine. Sasa kunaweza kukawa kuna tofauti yoyote ya thamani au kuamini kwamba usipoenda na utaratibu unaumiza watu.

Maguri ameishacheza Simba, kuna siku kama atakuwa na Yanga, basi akikosa kufunga bao, watasema ana mapenzi na Yanga.

Akikosea watasema bado ana uhusiano wa kirafiki na viongozi wa Simba na kadhalika. Jambo litamtokea si baada ya muda mrefu kwa kuwa kama mchezaji, lazima iko siku atakosea tu. Unafikiri Yanga wote ni waelewa kiasi hicho?

Inawezekana mshahara wa Yanga ukawa juu, lakini bora akipata nafasi TP Mazembe kwa mshahara ulio chini aende kama sehemu ya kujifunza na kujipa nafasi ya kujitanua kiuwezo na fikra pia.
Kubaki Tanzania akiichezea Yanga ni kuendelea kuingia kwenye kundi la wachezaji wa Kitanzania ambao wengi wametamba na kuishia hapa nyumbani.
Lazima Maguri awe na hamu ya kutoka, waamini kupambana katika sehemu ngumu ni sehemu ya kukua haraka.
Maguri akibaki Yanga tayari ni staa, lakini akiondoka na kujiunga na TP Mazembe, atajiona hana kitu, atalazimika kupambana kupata namba.
Wakati akipambana itakuwa chachu na changamoto kwake, hivyo ataweza kujifunza zaidi na kuwa bora zaidi kuliko akibaki Yanga ambako nafasi ya kupata namba ni kubwa mno kwa kuwa tayari anaongoza kwa mabao ya kufunga.

Najua Maguri anaangalia maslahi pia, lakini bado atakuwa na nafasi ya kuangalia maslahi zaidi hapo baadaye kuliko sasa halafu iwe kwa kipindi kifupi.



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: