Baada ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili wa wachezaji, kikosi cha JKT Ruvu tayari kimefanikiwa kuinyaka saini ya kiungo wa Stand United ambaye aliwahi pia kucheza kwenye klabu ya Yanga Hassan Dilunga
Kocha msaidizi wa JKT Ruvu Mrage Kabange amethibitisha taarifa hiyo na kuongeza kuwa, tayari Dilunga ameshaanza mazoezi na kikosi cha maafande hao wa Jeshi la Kujenga Taifa.
“Ni kweli Dilunga tayari tumeshamalizana naye na ameshaanza mazoezi na kikosi chetu na kwa kiasi kikubwa tunaona anaweza kukiongezea nguvu kikosi chetu katika nafasi ambayo tulikuwa tunaihitaji”, amsema Kabange.
“Sasa hivi tupo kwenye mazungumzo ya mwisho na wachezaji wengine wawili baada ya wiki moja naweza nikakupa jibu kuhusu wao”.
Kikosi cha JKT Ruvu kimeshindwa kufanya vizuri kwenye michezo yake ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu huu ikiwa imeshinda mchezo mmoja pekee kati ya 10 huku ikienda sare mara mbili na kupoteza michezo saba.
Kikosi hicho kimeamua kujipanga kwa kufanya usajili katika nafasi kadhaa kuhakikisha kinafanya vizuri na kurejea kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara kwani kwa sasa wako nafasi ya 14 kati ya timu 16.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment