MWANDISHI
wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kukuza Utawala Bora na
Uwazi, Edwin Soko anatarajia kuipandisha kizimbani serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania
Soko
amewaambia waandishi wa habari kuwa ana nia ya kuifikisha serikali
mahakamani chini ya kifungu cha. 6(2) Sheria ya mwenendeo wa makosa sura
ya 5 ya sheria za Tanzania juzuu la 2002 , kikisomeka pamoja na kifungu
cha. 3,6(b)c.
Serikali
inatuhumiwa tuhuma za kutunga kanuni ndogo za utangazaji kwenye
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, huku ikijua kuwa inakiuka ibara
ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nimewaita
hapa kwa ajili ya kuwaambia kuwa, ninafungua kesi ya kikatiba dhidi ya
serikali kufuatia kuwepo kwa baadhi ya vifungu ndani ya kanuni ndogo za
maudhui ya utangazaji 2015, zinazokiuka katiba ya nchi na kuminya uhuru
wa mtu na chombo kupata taarifa na kuzisambaza kwa mujibu wa katiba,”
amesema Soko kwenye mkutano huo uliofanyika ofisi za UPTC jijini Mwanza.
Aliongeza
kwamba licha ya kubaki siku chache, kimsingi yeye pamoja na wanahabari
wengine walihitaji muda wa kujiridhisha kwa kina juu ya uwepo wa vifungu
ndani ya kanuni vinavyokiuka haki ya kikatiba kama ilivyoainishwa
kwenye ibara ya 18, kazi hiyo ilihitaji muda wa kutosha ili kufanya
uchambuzi wa kina na kubaini mapungufu.
Alibainisha
baadhi ya vifungu hivyo kuwa ni kanuni ndogo za maudhui ya utangazaji
2015, vinavyokiuka katiba ya nchi baadhi ya vifungu hivyo ni 15(2),6(a)
(7) (a) na (b), 8(2), 10 (10)(a), 9(2), (3) sanjali na utangulizi wa
sehemu ya tatu ya sheria unaosema hakuna kutangaza siku ya upigaji wa
kura, huku kwenye maudhui ya sheria hii inaruhusu matangazo.
Kanuni
hizo zilizotangazwa kwenye gazeti la serikali Juni 26, 2015 zinaminya
uhuru wa mtu kupata na kutoa taarifa kwa mwananchi na pia haki ya vyombo
vya habari vya luninga na redio kupata na kusambaza taarifa, kwani
vinawekewa vizingiti visivyokuwa na lazima kisheria.
Athari
za kanuni hizo kwa mujibu wa maelezo ya Soko, kuwa wananchi
wanapokonywa nguvu ya kikatiba waliyopewa katika ibara ya 18(a),(b),(c)
na (d) kwa kutotakiwa kushiriki kwenye programu na pia vyombo vya habari
vinanyimwa fursa ya kutafuta na kufikisha taarifa mbalimbali za
mwenendo wa uchaguzi kwa wananchi kwa kuwekewa mipaka ya kuripoti wakati
wa kampeni na siku ya kupiga kura.
Athari
nyingine ni kuwa wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na wanahabari
hawapo salama kwa mujibu wa kanuni hizi zenye uwezo wa kuwashughulikia
na matokeo yake yakaonekana kwa wananchi kukosa taarifa muhimu.
Soko
amethibitishia kuwa hatua za awali za ufunguaji wa kesi, ikiwa mosi ni
kutoa notisi kwa serikali, hatua hiyo tayari imefanywa na notisi
zimesambazwa kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA).
chanzo:mwanahalisionline
Chagua kiongozi bora ili kuleta mabadiliko
Blogger Comment
Facebook Comment