TUME
ya Taifa ya uchaguzi imesema itatoa ufafanuzi kuhusu kinachodaiwa kuwa
ni mashine za BVR zilizokamatwa jana kwa ushirikiano wa jeshi la polisi
na Maofisa wa Chadema huku chama hicho kikisema wataalamu wake bado
wanazichunguza wakishirikiana na polisi ili kujiridhisha.
Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva ameliambia MwanaHalisi
Online kuwa tume bado inafuatilia na itatoa taarifa ingawa kwa hatua za
awali wataalamu wa tume wamesema kuwa mashine hizo si sawa na zile za
tume ya uchaguzi ingawa zinafanana.
“Bado
tunachunguza tuweze kutoa taarifa kamili, lakini tunawasihi wadau wetu
wote watulie waache kuingiza hofu kwani zinawachanganya wananchi.
“Vile
vifaa ni kweli vinafanana na vyetu lakini huyo mtu yeye alikuwa na
mashine zake kusajili wafanyakazi wake, naomba itoshe kwa sasa waambie
wananchi taarifa kamili itatolewa,” amesema Lubuva.
Wakati
Lubuva akisema hayo, Wakili kutoka makao makuu ya Chadema, John Malya
amesema wataalamu wake wa IT wapo bega kwa bega na polisi kujiridhisha
iwapo hizo mashine hazihusiani na zoezi la kujiandikisha lililofanywa na
tume ya taifa ya uchaguzi.
Leo
mmoja ya vyombo vya habari nchini (sio MwanaHalisi) liliripoti suala la
kutanda hofu katika kiwanda cha MM Steel cha jijini Dar es Salaam
chenye mashine za kusajili majina ya watu kwa mfumo wa kieletroniki.
Vifaa
hivyo ni pamoja na scanner, computer na kifaa cha kuchukua alama za
vidole, ambavyo Mejena wa Mawasiliano wa kampuni hiyo, Abubakari Mlawa
amesema wameamua kuandikisha wafanyakazi wake kutokana na kukithiri kwa
vitendo vya wizi katika viwanda saba walivyonavyo na kushindwa
kuwatambua wafanyakazi.
Maafisa wa NEC walioripotiwa kuwa eneo la tukio walikiri kuwa mashine hizo zinafanana na zile tume.
“Tulichokiona
ni baadhi ya vifaa ambavyo vinafanana na vifaa vya tume, lakini
hatuwezi kuhakikisha kama ni vyetu au sio, tulichokubaliana na polisi ni
kuchukua vifaa hivyo vifanyiwe uchunguzi zaidi ili tujiridhishe na
vifaa tulivyonavyo,” amesema Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na
Mipango wa NEC, Salvisius Mkwera.
Chanzo:mwanahalisionline
Chagua kiongozi bora ili kuleta mabadiliko