HISTORIA KULEKELEKEA MECHI YA WATANI WA JADI SIMBA NA YANGA


 
KUELEKEA SEP 26: UJUMBE WA MANARA HUU HAPA

Wapendwa wana-Simba wenzangu,
Ninawaandikia ujumbe huu makhsus kuwashukuru kwa mara nyingine kwa kazi nzuri mliyoifanya uwanjani Leo

kwa kuishangilia timu yenu mwanzo mwisho kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Taita.

Mimi  naamini bila ya support yenu Simba haiwezi kufanya vizuri hata siku moja.

Pia kwa niaba ya uongozi wenu tunawashkuru sana wapenzi wetu ambao  hawakujaaliwa kufika uwanjani hii


leo. Sisi tunaamini dua na sala zao zmesaidia kutupa nguvu hii leo na kupata points tatu muhimu.

Na kwa umuhimu wa pekee tuwapongeze sana wachezaji wetu na bench la ufundi kwa kazi kubwa wanayofanya

ya kutupa furaha.hakika hiki ndio wanasimba wanachotaka

Mwisho niwaombe sana.sote wiki hii tuwekeze akili yetu tarehe 26 yaan wiki ijayo.mnajua tuna mechi ngumu

dhidi ya watani zetu. Kwa upande wa uongozi umejipanga kwa kila hali kuhakikisha tunashinda game hyo.iwe

jua.iwe mvua yanga hawatoki Taifa Jumamosi ijayo.

Wapenzi wetu, tunawaomba sana umoja na mshikamano wenu kuelekea game ya Jumamosi.
Kila mmoja ruksa kufanya awezacho kuhakikisha tunawalaza tena mapema vibonde wetu.Narudia RUKSA.

Mwisho ingawa si  kwa umuhimu niwashukuru wanahabari wote kwa kazi nzuri waifanyayo ya kutuhabarisha

habari za mnyama.

Reclaiming our glory
Simba nguvu moja

Imeandikwa na mtumishi wenu
Haji S.Manara
Msemaji wa SSC


,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,



KUELEKEA SEP 26: MURO ATUPA KIJEMBE
muro
Kama ilivyo kawaida yake, mkuu wa kitengo cha habari wa klabu ya Yanga SC, Jerry Muro amerusha kijembe kwa

mahasimu wao Simba SC kuelekea mchezo wa vigogo hao wa soka nchini siku ya Jumamosi hii katika uwanja wa

Taifa. Yanga imeshinda gemu zake zote tatu za kwanza katika ligi kuu msimu huu na kuachana na rekodi yake ya

miaka yote kuanza vibaya na kumalizika vizuri ligi.

Imeshinda 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika gemu ya kwanza kisha wakashinda 3-0 dhidi ya Tanzania

Prisons katika mchezo wa pili, wakaishinda 4-1 JKT  Ruvu na kufikisha alama 9 sawa na timu za Simba, Mtibwa

Sugar na Azam FC ambazo pia zimeshinda michezo yao yote mitatu ya mwanzo msimu huu.

Yanga wanaongoza ligi kutokana na wastani wao mzuri wa magoli 8. Wamefunga magoli 9, wameruhusu nyavu

zao kutikiswa mara moja.

Simba pia wameanza ligi kwa ushindi mfululizo, wameshinda 1-0 dhidi ya Africans Sport, kisha wakashinda 2-0

dhidi ya JKT Mgambo na mechi hizo zote mbili za mwanzo walichezea ugenini, Mkwakwani Stadium, Tanga.

Mechi yao ya kwanza katika uwanja wa Taifa msimu huu walishinda 3-1 dhidi ya Kagera  Sugar FC siku ya

Jumapili iliyopita lakini hilo halimtishi, Jerry ambaye amesisitiza Yanga inahitaji utulivu na muda zaidi kabla ya

kuendeleza ushindi wao siku ya Jumamosi hii.

 “Kama klabu ya Yanga tumejipanga vizuri, niwataarifu tu wapenzi na wanachama wetu popote pale walipo

kuwa timu inaendelea vizuri na kambi yetu ya maandalizi kuelekea mchezo wetu wa Jumamosi” anaanza

kusema, Murro ambaye timu yake imejificha kisiwani Pemba.

 “Hatutakuwa wazungumzaji sana, tunawaomba mashabiki wetu watupe muda wa kujitathimini na tuwe na

wakati mzuri wa kukitayarisha kikosi chetu ili mwisho wa siku tuweze kupata matokeo mazuri zaidi. Maneno

kwetu si yatakayofanya kazi, wanachama na wapenzi wa timu yetu watupe muda tuandae kikosi” .

Kuhusu mahasimu wao Simba, Muro ameifananisha timu hiyo na kisigino ambacho daima huwa nyuma si mbele.

 “Sisi si kama ‘ wamchangani-Simba’ ambao ‘ kutwa’ hawaishi kuongea, utekelezaji hakuna. Niseme wazi

tumeshinda michezo yetu yote na tunaongoza ligi, tunachokifanya sasa ni kuendelea kuwa juu kuhakikisha

tunatimiza wajibu. Nachofahamu mimi duniani kote haijawahi kamwe ikatokea kisigino kikawa mbele. Siku zote

kimekuwanyuma. Haitawahi itokee hao ‘ wamchangani’ wakakaa mbele yetu”


,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,


 MECHI YA 77 SIMBA NA YANGA LIGI KUU TANGU 1965


“KITIMTIMU, mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu kaingiaje!” Naam, hilo ni chagizo la wimbo

maarufu wa mashabiki wa Yanga kila wanapoishangilia timu yao, hasa inapocheza na Simba.
Lakini chagizo hilo litakumbana na kibwagizo cha mashabiki wa Simba, maarufu kama Mchacho Group (ambao

sasa wameongezewa sapoti na tawi la Mpira Fedha) watakaokuwa wakiimba “Amesimama kidedea, eeee

kidedea!”
Timu hizo mbili zinapopambana katika mechi ya Jumamosi hii Aprili 19, kukunja jamvi la Ligi Kuu ya Soka

Tanzania Bara kwa msimu wa 2013/2014, kila mtu anatazama nini kitatokea, iwe uwanjani ama nje ya uwanja.
Mechi baina ya timu hizi mbili kongwe katiba katika historia ya kandanda nchini huwa zinatawaliwa na vituko

vingi mno. Kuvunja nazi, kuoga maji ya maiti, kuruka ukuta, kuingia uwanjani kinyumenyume na mengine kama

hayo hutajwa kwamba ni sehemu ya kuhanikiza ushindani.
Hata hivyo, kwa sasa hawawezi kuruka ukuta kama ilivyokuwa miaka ile ya zamani, wala hawawezi kuoga maji

ya kuoshea maiti au kuvunja nazi hadharani, kwa sababu Sheria za Soka haziruhusu ushirikina na tayari timu hizo

mbili zimekwishawahi kutozwa faini kwa vitendo hivyo.
Simba ikiwa inatokea Zanzibar, na Yanga ambayo ilikuwa Kawe jijini Dar es Salaam, zinapambana Jumamosi hii

zikitaka kulinda heshima tu, kwa sababu ubingwa tayari umekwishachukuliwa na Azam FC iliyofikisha pointi 59

ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.
Ushindi wa Azam wa mabao 2-1 nyumbani kwa Mbeya City Jumapili iliyopita uliifanya iweke rekodi mpya kwa

kuwa timu ya nane katika historia ya soka nchini kunyakua ubingwa huo ambao umekuwa ukitwaliwa na Simba

na Yanga pekee. Mara ya mwisho kwa timu nyingine kutwaa ubingwa (mbali ya Simba na Yanga) ilikuwa mwaka

2000 wakati Mtibwa Sugar ilipotwaa kwa mara ya pili mfululizo ubingwa huo wa Bara.
Lakini pia ushindi wa Azam ulivunja rekodi ya kutofungwa ya Mbeya City kwenye uwanja wake wa nyumbani

katika msimu huu, huku Azam ikiendelea kushikilia rekodi yake nyingine ya kutopoteza hata mechi moja katika

msimu huu. Sijui leo hii hali itakuwaje.
Yanga yenyewe imeshika nafasi ya pili kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Sheikh Amri

Abeid jijini Arusha dhidi ya JKT Oljoro na sasa inahitaji vitu viwili tu – kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0

msimu wa 2011/2012 pamoja na kulinda hadhi yake, huku Simba ikitaka kuendeleza ubabe kwa vijana hao wa

Jangwani kwa kuwa hakuna itakachopoteza katika nafasi yake ya nne iliyoifikia.
Lakini kwa upande mwingine ushindi ni muhimu sana kwa Simba ikiwa inataka kulinda hadhi yake japo kwa

kumaliza ikiwa ya nne, kwa sababu ikiwa itapoteza mchezo huo, basi inaweza kujikuta ikimaliza ikiwa ya sita

msimu huu. Hii ni kwa sababu mpaka sasa ina pointi 37 wakati nyuma yake kuna timu mbili za Kagera Sugar na

Ruvu Shooting ambazo zina pointi 35 kila moja.
Kagera Sugar inayoshika nafsi ya tano ikishinda ugenini kwa Coastal Union na Ruvu Shooting ikiwalazama

maafande wa Rhino Rangers ambao tayari wamekwishashuka daraja, zinaweza kuipiku Simba kimzaha mzaha tu.
Kelele za: “Simba! Simba! Simba!” na zile za: “CCM! CCM! CCM!” zitasikika kwenye Uwanja wa Taifa, lakini

zitahitaji kuangalia matokeo ya uwanjani yakoje, vinginevyo upande mmoja unaweza kuzizima.
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani

ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye

jezi za kijani na manjano.
Mandhari haya ndiyo yaliyokuwepo Jumapili Oktoba 20, 2013 kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, wakati Simba na

Yanga zilipoumana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014.
Wakati Yanga, ambayo ilikuwa inatetea ubingwa wake huku ilikiwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo,

ilikuwa inatafuta ushindi ili kukwea kileleni lakini pia kulipa kisasi cha mabao 5-0 ilichokipata mwaka 2012 katika

mchezo wa mwisho. Jambo hili lilionekana kuwa ni ndoto baada ya kushindwa kuyalinda mabao yake matatu

iliyoyapata katika kipindi cha kwanza, hivyo kuifanya Simba isawazishe na kuleta matokeo ya ajabu ya sare ya 3

-3.
Simba wao walikuwa na mambo mawili: Kwanza, walitaka kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa mwisho

wa Ligi Kuu Mei 17, 2013, lakini pili, walikuwa wanatafuta ushindi ili kujiweka sawa zaidi na kutwaa ubingwa

baada ya kukosa hata nafasi ya pili.
Kama wachezaji wa timu hizo watatulia na kutandaza soka, huku wakiacha ubabe na kufuatisha kelele za

mashabiki jukwaani, hakika hii itakuwa burudani safi ya kufungia msimu.

Mechi zao
Hii itakuwa mechi ya 77 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi ya

Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekeza mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu

gani.
Hata hivyo, katika mechi 76 zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 29,

wakati Simba imeshinda mara 22. Timu hizo zimetoka sare mara 25 huku mabao 162 yakifungwa. Kati ya mabao

hayo, Yanga imefunga 86 na Simba imefunga 75. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi ya

Muungano.

Idd Pazi, Kaseja kiboko
Makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ na Juma Kaseja wana rekodi ya pekee kwenye mechi za Simba na Yanga

kutokana na ukweli kwamba ndio makipa pekee baina ya timu hizo kufunga bao. Pazi alifunga bao la kuongoza

kwa penalti Jumamosi Machi 10, 1984 katika dakika ya 20 na akajitahidi kulinda lango la Simba hadi dakika ya

72 wakati Omar Hussein alipomzidi ujanja na kusawazisha. Matokeo yakawa 1-1.
Kaseja naye aliingia kwenye rekodi hiyo katika mechi ya Mei 6, 2012 ambayo Simba ilishinda 5-0 baada ya

kufunga kwa penalty katika dakika ya 67, likiwa ni la nne kwa timu yake.
Mlinzi Suleiman Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, ndiye pekee aliyewahi kujifunga wakati timu hizo mbili

zilipomenyana kwenye Ligi. Sanga alijifunga katika harakati za kuokoa katika mechi ya Julai 19, 1977 wakati

Yanga ilipokubali kipigo cha mabao 6-0, huku Abdallah Athumani ‘King Kibadeni’ akifunga hat trick (mabao

matatu) peke yake na mengine mawili yakifungwa na Jumanne Hassan Masimenti.

Wafungaji wa mabao
Katika mechi 76 zilizopita na kuzaa mabao hayo 161, Omar Hussein ‘Keegan’ wa Yanga ndiye anayeongoza kwa

ufungaji, akiwa amezifumania nyavu mara sita akifuatiwa na Abeid Mziba ‘Tekero’, Idd Moshi na Jerry Tegete wa

Yanga pia, pamoja na Edward Cyril Chumila na Musa Hassan 'Mgosi' ambao wamefunga mabao manne kila

mmoja.
Waliofunga mabao matatu kila mmoja ni Kitwana Manara ‘Popat’, Maulid Dilunga, Said Mwamba ‘Kizota’ na

Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ wa Yanga, pamoja na Abdallah Athumani ‘Kibadeni’.
Orodha hiyo inaonyesha waliofunga mabao mawili kwa upande wa Yanga ni Salehe Zimbwe, Juma Mkambi,

Rashid Hanzuruni, Said Sued 'Scud', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji’, Issa Athumani, Idelfonce Amlima, Sekolojo

Chambua, Ben Mwalala na Sunday Manara.
Kwa upande wa Simba ni Jumanne Hassan ‘Masimenti’, John Makelele 'Zig Zag’, Malota Soma ‘Ball Jugler’,

Nicodemus Njohole, Dua Said, Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Athumani

Machupa, Emmanuel Okwi.
Wachezaji waliopachika bao moja kwenye mechi hizo kwa upande wa Yanga ni Mawazo Shomvi, Abdulrahman

Lukongo, Andrews Tematema, Emmanuel, Leonard Chitete, Gibson Sembuli, Charles Boniface, Edgar Fongo, Justin

Mtekere, Thomas Kipese, Sanifu Lazaro, Ken Mkapa, James Tungaraza, Akida Makunda, Constantine Kimanda,

Salvatory Edward, Kally Ongala, Pitchou Mwango Kongo, Aaron Nyanda, Said Maulid, Athumani Idd, Stephano

Mwasika, Davies Mwape, Said Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza.
Nyota wa Simba waliofunga bao moja kila mmoja ni Mustafa Choteka, Haji Lesso, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid

'Mchacho', Adam Sabu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Abbas Dilunga, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally, Kihwelu

Musa, Zamoyoni Mogella, Mohammed Bob Chopa, Sunday Juma, Mavumbi Omar, George Masatu, Athumani

China, Mchunga Bakari, Abdallah Msamba, Athumani Machepe, Abuu Juma, Juma Amir, Joseph Kaniki, Athumani

Machupa, Nurdin Msigwa, Emmanuel Gabriel, Moses Odhiambo, Ramadhan Chombo, Haruna Moshi, Uhuru

Suleiman, Hilary Echesa, Idi Pazi, Patrick Mafisango, Juma Kaseja, Felix Sunzu, Amri Kiemba.

Kukimbiana
Mechi za Simba na Yanga hazikosi kuwa na vituko, lakini vinavyojulikana zaidi ni kule ‘kukimbiana’ uwanjani ama

kwa kutopeleka kabisa timu uwanjani, au kwa kugomea mchezo.
Zifuatazo ni rekodi za timu hizo kukimbiana kwenye Ligi Kuu:
05/11/1966: Mchezo ulivunjika katika dakika ya 75 baada ya Yanga kugoma kumtoa mchezaji wao Awadh

Gessani aliyeamriwa atoke nje baada ya kumchezea vibaya yule wa Sunderland. Sunderland wakapewa ushindi

na baadaye kuwa bingwa wa taifa kwa mara ya pili. Kabla ya mchezo kuvunjika Yanga ilikuwa inaongoza kwa

mabao 2-0. Nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’, alifungiwa na FAT kutocheza mpira kwa

miezi 12 na kwamba asipewe cheo cha unahodha, na Awadh Gessani akafungiwa kutocheza mechi tatu. Yanga

ikatishia kujitoa kwenye ligi pamoja na African Sports, lakini baadaye timu hizo zikashauriwa kuendelea na ligi.
30/03/1968: Mchezo ulivunjika baada ya mchezaji wa Sunderland, Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’, kumpiga

mwamuzi Jumanne Salum katika dakika ya 20. Wakati huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na

Kitwana Manara. Mchezo huo ukapangwa kurudiwa Juni Mosi, 1968 ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 5-0.
03/03/1969: Sunderland iligoma kabisa kutia mguu uwanjani, hivyo, FAT ikaipa Yanga ubingwa na kuitoza

Sunderland faini ya shilingi 500, ambazo hata hivyo, hazikulipwa baada ya kulisuluhisha suala hilo.
18/06/1972: Sunderland iligoma kuingia uwanjani kwa kipindi cha pili kupambana na Yanga huku Yanga ikiwa

inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Leonard Chitete. Huu ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Taifa,

ambapo Yanga ilipewa ushindi.
10/08/1985: Simba iligomea penati iliyotolewa na mwamuzi Bakari Bendera wa Tanga katika dakika ya 84 baada

ya sentahafu wake Twalib Hilal kuunawa mpira katika eneo la hatari. FAT ikaipa Yanga ushindi na kuwa bingwa

wa Tanzania Bara.
26/08/1992: Yanga ilikataa kutia timu uwanjani kucheza na Simba katika mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la

Kwanza Tanzania Bara kwa kuwa tayari ilikwishatwaa ubingwa. Simba ikapewa ushindi na kisha FAT ikaipiga

Yanga faini ya shilingi 250,000 ambazo zililipwa na Murtazar Dewji aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea

Pan African.
25/02/1996: Simba iligoma kupeleka timu uwanjani baada ya FAT kukataa ombi lao la kuahirisha mchezo huo

kwa kuwa ilikuwa inajiandaa na mechi ya Kombe la Washindi dhidi ya Chapungu FC ya Zambia, ambayo hata

hivyo, haikuja kabisa. Yanga ikapewa ushindi.


,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,


: Yanga  kuvunja rekodi hizi za Simba


    SIMBA na Yanga ni watani wa jadi. Jambo linalofanyika Simba kwa namna moja ama nyingine litakuwa na

tambo kwa Yanga.

    Simba ikishinda mchezo lazima itatoa tambo zake kwa Yanga na vivyo hivyo kwa upande wa pili. Hayo ndiyo

maisha waliyoyachagua.

    Yanga ndiyo bingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara ikiwa imetwaa taji hilo kwa mara 24 na kuzipiku timu

nyingine zote zinazoshiriki ligi hiyo. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.

    Licha ya rekodi hiyo, Yanga bado inafunikwa na Simba kwenye rekodi nyingine za maana. Simba imefanikiwa

kuweka rekodi kadhaa ambazo Yanga itasota kuzifikia. Makala hii inazungumzia baadhi ya rekodi za Simba

ambazo Yanga inasota kuzifikia na kuzivunja.

    Kucheza fainali Caf

    Simba ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyofanikiwa kucheza fainali za Kombe la Shirikisho la Vyama vya Soka

Afrika (Caf), ilikuwa mwaka 1993 wakati huo likijulikana kama Kombe la Caf. Simba ilicheza fainali hiyo na Stella

Abidjan ya Ivory Coast na kutoka sare katika mchezo wa awali kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2- 0 katika

marudiano jijini Dar es Salaam.

    Licha ya Simba kupoteza mchezo huo ambapo wachezaji wake waliahidiwa zawadi za magari kama

wangeshinda, inasalia kuwa timu pekee kutoka Tanzania Bara iliyofanikiwa kucheza hatua hiyo ya fainali hizo.

Yanga imewahi kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

    Nusu fainali klabu Bingwa Afrika

    Simba inajiweza, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa lugha rahisi baada ya timu hiyo kufanikiwa kucheza

nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974. Simba iliondolewa katika hatua hiyo ya nusu fainali na Mehala

El Kubra ya Misri na kuzima ndoto za kucheza fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.

    Rekodi hiyo ya Simba bado haijavunjwa mpaka hii leo. Yanga kwa upande wake, ilifanikiwa kucheza robo

fainali ya michuano hiyo kwa mara mbili mfululizo mwaka 1969 na 1970 lakini haikuwahi kufika zaidi ya hapo.

    Mbali na rekodi hiyo, Simba bado inajivunia rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Bara kufanikiwa

kuiondosha timu ya Misri katika michuano ya Afrika. Simba ilifanya hivyo mwaka 2003 baada ya kuifunga

Zamalek ya Misri ambayo ilikuwa bingwa mtetezi.

    Ubingwa Kombe la Kagame

    Licha ya Yanga kujivunia rekodi ya kutwaa taji la Kagame nje ya Dar es Salaam, Simba ndiyo vinara wa kulitwaa

taji hilo nchini. Simba imewahi kulitwaa taji hilo la Kagame mara sita na kuwa timu ya Bara yenye historia ya

kulitwaa zaidi kombe hilo.

    Mbali na kuwa timu ya Bara iliyotwaa taji hilo mara nyingi, Simba ndiyo timu inayoongoza kwa kutwaa Kombe

la Kagame kwenye historia ya michuano hiyo na kuzipiku timu zote za ukanda huo.

    Yanga imewahi kulitwaa taji hilo mara tano na kuwa timu ya pili kulitwaa kombe hilo mara nyingi baada ya

Simba hivyo inatakiwa kulitwaa mara moja ili kuifikia rekodi hiyo ama mara mbili ili kuivunja rekodi hiyo kabisa.

    Ubingwa wa Mapinduzi

    Simba imetwaa Kombe la Mapinduzi mapema wiki iliyopita huko visiwani Zanzibar na kuweka rekodi ya

kulitwaa taji hilo mara nyingi zaidi kwenye historia ya michuano hiyo. Simba imetwaa taji hilo mara tatu wakati

watani wao Yanga wamewahi kulitwaa mara moja pekee tangu kuanzishwa kwake miaka tisa iliyopita.

    Azam ni timu ya pili kwenye rekodi hiyo ikiwa imelitwaa mara mbili. Mbali na rekodi hiyo pia Simba inaongoza

kucheza mechi za fainali ya michuano hiyo ikiwa imecheza mara tano wakati watani wao wamecheza mara tatu

pekee.

    Kuzalisha, kuuza wachezaji

    Simba ina wachezaji ambao inaweza kujivunia kuwa ni wao. Licha ya kwamba klabu hiyo inafanya usajili wa

nyota kadhaa wa ndani na nje ya nchi, bado timu hiyo ina wachezaji inaojivunia kuzalishwa klabuni hapo.

    Simba ina wachezaji kama Ramadhan Singano, Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdallah Seseme na William Lucian

‘Gallas’ iliyowaibua na kuwazalisha kuwa miongoni mwa nyota wa soka nchini.

    Ni wachezaji waliozalishwa klabuni hapo na kuendelezwa mpaka sasa. Wapo wengine kama Edward

Christopher ‘Edo’ ambao wanacheza timu nyingine lakini chimbuko lao ni Simba. Yanga hakuna kitu kama hicho.

    Kikosi cha Yanga kimejaa nyota wa kununuliwa kutoka timu nyingine za ndani na nje ya nchi. Achana na Nonda

Shaaban ‘Papii’, hakuna mchezaji mwingine aliyefanikiwa kung’ara au kuuzwa nje ya nchi akitokea Yanga.


    Ni rekodi ya kipekee kwa Simba ambayo itaichukua Yanga miaka mingi kuifikia. Mbali na hilo pia Simba inabaki

kuwa miongoni mwa timu chache nchini zilizofanikiwa kufanya mauzo ya maana ya wachezaji nje ya nchi.


    Simba ndiyo iliyomuuza Mbwana Samatta kwenda TP Mazembe. Timu hiyo ilimuuza pia mshambuliaji wa timu

hiyo, Emmanuel Okwi kwenda Etoile Du Sahel ya Tunisia. Yanga haina utamaduni huo wa kuuza nyota wake.

    Kipigo cha mabao 6-0

    Yanga haitaki kabisa kuukumbuka mwaka 1977. Ni mwaka mchungu kwao. Timu hiyo ilifungwa na Simba

mabao 6-0 kwenye mechi ya ligi shukrani kwa kazi nzuri ya Abdallah ‘King’ Kibadeni aliyefunga mabao matatu

‘hat trick’, Jumanne Hassan ‘Masimenti’ aliyefunga mawili na Suleiman Sanga aliyejifunga bao moja na kupeleka

kilio hicho Jangwani. Kipigo hicho kilifuta rekodi ya Yanga ya mwaka 1968 ilipoifunga Simba mabao 5-0. Ikiwa ni

miaka 37 imepita bado Yanga imeshindwa kufuta rekodi hiyo. Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya kufungwa tena

mabao 5-0 mwaka 2012.

    Msimu bila kupoteza

    Simba ilifanikiwa kuweka rekodi ya kipekee mwaka 2010 baada ya kutwaa ubingwa wa ligi bila kupoteza

mchezo. Ulikuwa msimu wa kipekee kwa Simba baada ya kucheza mechi 22 za msimu huo huku ikishinda 18 na

sare nne. Ilikuwa ni rekodi ya kipekee.

    Azam iliweza kuivunja rekodi hiyo msimu uliopita baada ya kumaliza msimu bila kupoteza mechi na kutwaa

ubingwa wa Bara. Yanga haijaweza kuwa na rekodi kama hiyo na inavyoonekana itachukua miaka mingi kuivunja

rekodi hiyo ya Simba.

..................................................



Mechi ya watani wa jadi ikiwa inachezwa Jumamosi hii, Goal inakuletea kikosi cha wachezaji 11 kinachojumuisha

wachezaji bora toka pande zote

1.Ally Mustapha ‘Barthez’

Huyu ndiyo kipa bora kwa sasa nchini ambaye kiwango alichokuwa nacho anawazidi makipa waliopo kwenye

vikosi hivyo hata Manyika Peter anayeidakia Simba kwa sasa.

2.Hassan Ramadhan ‘Kessy’

Beki wa kulia kutoka Simba amekuwa na kasi na uwezo mkubwa wa kupanda na kushuka na hiyo inafanya winga

wa kulia wa Simba kutokuwa na kazi kutokana na kazi zote za upande wa kulia kumaliza yeye.

3.Hajji Mwinyi

Fulback wa kushoto kutoka Yanga uwezo wake wa kucheza kwa kujiamini huku akipanda mbele kusaidia

mashambulizi anaingia kwenye kikosi hiki bora kinachoundwa na wachezaji wa timu hizi mbili za Simba na Yanga.

4.Juuko Murshid

Beki wa kati wa Simba raia wa Uganda ambaye licha ya kuwa huu ndiyo msimu wake wa pili lakini uwezo wake

umemfanya kuingia kwenye kikosi hichi bora na kuwaweka pembeni wakali wengi kutokana na namna

anavyocheza kwa kujitolea.

5.Nadir Haroub ‘Cannavaro’

Kiwango alichokionyesha beki huyo kwenye mechi nyingi za timu yake na hata timu ya taifa hakuna atakayepinga

kuwemo ndani ya kikosi hiki bora ambacho kinaundwa na nyota kutoka pande zote mbili kwasababu ni mchezaji

ambaye amekuwa akicheza kwa kujitolea kwa muda wote wa dakika 90.

6.Thaban Kamusoko

Kiungo mpya wa Yanga ambaye katika mechi tatu alizoichezea timu hiyo ameonyesha kama kweli anastaili

kuwemo kwenye timu hiyo inayoundwa na nyota kutoka klabu hizo mbili zenye upinzani mkubwa kwenye Ligi ya

Vodacom Tanzania.

7.Simon Msuva

Mchango wake kwa Yanga unamfanya astaili kuwemo kwenye kikosi hiki bora cha wapinzani wa jadi Msuva ndiye

mfungaji bora wa msimu uliopita kasi aliyokuwa nayo imekuwa ikiwashinda wachezaji wengi hata Simon

Sserunkuma wa Simba ambaye aliletwa maalum kuisaidia timu hiyo.

8.Said Ndemla

Kiungo mchezeshaji mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho lakini pia kufunga kwa aina ya uchezaji

wake na namna alivyokuwa mwepesi anastaili kuwepo kwenye kikosi hicho bora cha nyota wa Simba na Yanga.

9.Donald Ngoma

Mshambuliaji hatari wa Yanga Ngoma ameingia kwenye kikosi hiki kutokana na umahiri wake wa ufungaji

aliokuwa nao japo mechi ya watani wa jadi kwake itakuwa mara ya kwanza tangu kuanza kucheza ligi ya

Vodacom lakini kasi yake aliyoionyesha mechi zilizopita inamfanya kuingia kwenye kikosi hiki bora.

10.Hamisi Kiiza

Ni mshambuliaji anaye jua vyema ugumu wa mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga na ameingia kwenye

kikosi hiki kutokana na uwezo aliokuwa nao wa kufunga mabao mengi kadri anavopata nafasi.

11.Haruna Niyonzima

Nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda Niyonzima ameingia kwenye kikosi hiki baada ya uwezo aliokuwa nao wa

kuichezesha timu lakini hata kufunga mwenye anapopata nafasi akitokea popte pale iwe pembeni au katikati na

anawashinda wachezaji wengi wa timu zote mbili wanaomudu kucheza nafasi hiyo


...............................................



Home Unlabelled TANGU 1977 REKODI YA KIBADENI HAIJAVUNJWA SIMBA NA YANGA
TANGU 1977 REKODI YA KIBADENI HAIJAVUNJWA SIMBA NA YANGA



KUCHEZA Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji wa Tanzania. Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji

ambaye atashiriki mechi baina ya timu hizo.
Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga bao au mabao katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya

maelfu ya mashabiki wa timu yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine, hupewa zawadi

kutokana na kufunga kwenye mechi hizo za watani.
Wapo waliolewa sifa na kupotea kwenye ramani ya soka haraka, kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya

kufunga mabao mfululizo kwenye mechi za watani.
Said Sued 'Scud', alifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa

nyavu za Simba dakika ya saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu Mei 18,

mwaka 1991.
Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo, hakika ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo

aliaminika na kuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa ya kuifunga tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano

wa ligi baina ya watani wa jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991, jambo ambalo

lilimfanya awe maarufu zaidi.
Lakini katika mastaajabu ya wengi, Scud hakurejea kwenye kikosi cha Yanga cha mwaka 2002 na huo ukawa

mwisho wa umaarufu wake kwenye soka ya Tanzania.
Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kubwa sana katika historia ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali

kabisa na ukweli, kwani Abdallah Kibadeni (pichani kulia juu), maarufu kama Chifu Mputa ama King, au Ndululu

kama walivyokuwa wakimuita Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la kujivunia katika historia ya

mechi baina ya Simba na Yanga ambalo hadi kitabu hiki kinaingia sokoni lilikuwa halijavunjwa.
Abdallah Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyeweza kufunga mabao matatu peke yake katika mchezo

mmoja kwenye mechi za watani wa jadi katika Ligi.
Hiyo ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati

Yanga ilipotandikwa 6-0 na Simba.
Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa

Msimbazi, yalitiwa kimiani na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na jingine Selemani Sanga wa

Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson 'Jujuman'.
Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia kulipa kisasi cha kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968,

Kibadeni alikuwa ana sherehe binafsi za kutumbukiza tatu peke yake kwenye mechi baina ya watani hao, jambo

ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za Simba au Yanga.
Hakuna cha Sunday Manara 'Computer' wala Maulid Dilunga 'Mexico' aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya King

Kibadeni pekee.




Chagua kiongozi bora ili kuleta mabadiliko
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment