Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa katika vita vya siku 50
vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel
dhidi ya Ukanda wa Gaza
shule saba za umoja huo zilishambuliwa, na Wapalestina 44 waliuliwa kwenye
mashambulio hayo.
Katika barua aliyoandika na kuiambatanisha na ripoti ya
matokeo ya uchunguzi kuhusu vita vya Gaza ambayo ilitolewa siku ya Jumatatu,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema, na hapa
ninamnukuu:"Ninasikitishwa na ukweli huu, kwamba Wapalestina wasiopungua
44 waliuliwa na wengine 227 walijeruhiwa katika mashambulio iliyofanya Israel
kwenye vituo na majengo ya elimu ya Umoja wa Mataifa yaliyotumiwa na watu hao
kama vituo vya kupatia hifadhi ya dharura".
Matukio yanayojiri kimataifa yanaonyesha kuwa jinai za Israel dhidi ya
wananchi wa Palestina zingali zinaendelea kufuatiliwa kimataifa. Kuendelea
kutolewa radiamali dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni ni ithbati na ushahidi
tosha wa kuonyesha kuwa utawala huo ghasibu umeshindwa kuficha na kufifilisha
jinai zake hizo na kwamba jinai za kinyama na za kutisha zinazofanywa na Israel
haziwezi kufutika ndani ya fikra za walimwengu.
Wito ambao umekuwa ukitolewa kutokea pembe mbalimbali za
dunia wa kutaka kuchunguzwa jinai za Israel na kuwachukulia hatua
watenda jinai wa Kizayuni ni ishara ya kushtadi harakati za kimataifa za kutaka
zichukuliwe hatua za kisheria dhidi ya utawala huo usio na chembe ya utu na
unaonuka kimataifa kutokana na jinai zake.
Itakumbukwa kuwa Wapalestina wasiopungua 2,200 walipoteza
maisha na maelfu ya wengine walijeruhiwa wakati wa vita vya siku 50 vya mwaka
2014 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel
dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Aidha nyumba elfu 89 za Wapalestina ziliharibiwa, elfu 15 miongoni mwa hizo
zikiwa zimebomolewa kabisa au kuharibiwa kwa kiwango cha kutoweza kukalika
tena.
Mbali na maelfu hayo ya nyumba za raia, zaidi ya shule 140
na majengo ya viwanda 350 pia yalibomolewa na kuifanya hali ya eneo la Gaza lililowekewa mzingiro na utawala haramu wa Israel iwe
mbaya zaidi. Mwenendo wa Israel
unadhihirisha jinsi utawala huo khabithi usivyojali wala kuchunga mipaka yoyote
katika kutenda jinai zake.
Kitendo cha utawala huo ghasibu cha kupuuza maazimio ya
Umoja wa Mataifa na kukiuka kila mara mikataba ya kimataifa kimeitafiri na
kuichosha Jamii ya Kimataifa. Kuitishwa vikao mbalimbali vya kimataifa
kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni na kutolewa maazimio, taarifa na
ripoti kadha wa kadha za Umoja wa Mataifa na taasisi zenye mfungamano na umoja
huo dhidi ya Israel ni ushahidi kwamba walimwengu wanakabiliana na utawala
afriti na uliokubuhu katika kutenda jinai.
Katika hali na mazingira kama hayo kutochukua hatua yoyote
Umoja wa Mataifa dhidi ya Israel
na kutosheka na kutoa ripoti tu kuhusiana na jinai za utawala huo haramu
hakutokuwa na tija nyengine ghairi ya kushadidisha vitendo vyake haribifu
unavyovifanya kieneo na kimataifa. Kutolewa ripoti ya uchunguzi kuhusu jinai za
Israel katika vita vya siku
50 vya mwaka 2014 huko Gaza ni muendelezo wa
ripoti ya kamati ya kutafuta ukweli iliyoongozwa na Jaji Richard Goldstone
ambayo ilifanya uchunguzi kuhusu vita vya siku 22 vilivyoanzishwa na utawala wa
Kizayuni pia dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo mwaka 2009.
Ripoti hiyo iliyotokana na ushahidi wa nyaraka elfu 20,
picha na mazungumzo ya ana kwa ana na mashaidi zaidi ya 200 ilithibitisha kwa
uwazi kabisa kwamba utawala wa Kizayuni ulitenda jinai za vita katika
mashambulio yake ya siku 22 dhidi ya Gaza.
Lakini pamoja na kamati ya Jaji Goldstone kutoa ushahidi
huo, ukwamishaji uliofanywa na Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi pamoja
na upuuzaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika ufuatiliaji, ripoti
hiyo ya kamati ya kutafuta ukweli haikusaidia kuchukuliwa hatua yoyote ya
kivitendo dhidi ya Israel; na kwa kweli ni mwenendo huo ndio unaozidisha kiburi
na jeuri ya utawala haramu wa Kizayuni ya kuendelea kufanya jinai utakavyo.
Katika hali kama hiyo kutosheka viongozi wa Umoja wa Mataifa
akiwemo Katibu Mkuu wake na kutoa matamshi matupu ya kulaani jinai za Israel
hakutokuwa na matokeo mengine zaidi ya kuufanya utawala huo uendeleze jinai
zake zinazozidi kuungulisha na kusononesha nyoyo za fikra za waliowengi duniani
0 comments:
Post a Comment