MASIKINI! Staa mkali wa
filamu za Kibongo, Kajala Masanja hivi karibuni amejikuta akiwa katika
wakati mgumu na wa hatari kufuatia watu wasiojulikana kuvamia nyumbani
kwake na kutoa onyo kwamba wanampa siku tano tu za kuishi, Amani lina
mkasa kamili.Ishu hiyo ya kushtusha ilitokea usiku wa saa nane ya
kuamkia juzi, Jumanne nyumbani kwa staa huyo, Sinza Mori jijini Dar es
Salaam.
WALIKUWA KWENYE TOYOTA RAV 4
Kwa mujibu wa chanzo
chetu, watu hao wapatao watatu walitinga nyumbani hapo usiku huo mnene
huku wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Rav 4 milango mitano rangi ya
bluu ya kuiva na kumkuta mlinzi getini ambaye yupo kwa ajili ya kulinda
usalama wa msanii huyo mwenye maadui kila kukicha.“Walikuwa watano,
walikuwa kwenye Rav 4 milango mitano, rangi ya blue ya kuiva. Wakamkuta
mlinzi, walimuuliza kama Kajala yupo, mlinzi aliwadanganya kwamba
hayupo.”
MLINZI ALIJUA NI BWANA WA KAJALA
“Lakini mlinzi
alidanganya akijua mmoja wa watu hao pengine ni bwana wa Kajala kwa hiyo
ili kuua soo akasema hayupo lakini ukweli Kajala alikuwepo ndani. Yeye
aliwaambia Kajala alikwenda kumsalimia mama yake, hajarudi.
WAACHA UJUMBE MZITO
“Ndipo mmoja wao
akamwambia mlinzi kwamba, wao walikuwa na shida na Kajala lakini kwa
sababu hayupo, wanaacha ujumbe apewe haraka sana. “Walisema akirudi
aambiwe kuna watu walifika, wamempa siku tano za kuishi na kwamba wao
wametumwa na mtu wa karibu na Kajala, lakini hawakumtaja kwa jina.
“Yaani mlinzi alitumia
akili sana na kuwaambia Kajala hakuwepo ndani, alikwenda nyumbani kwao,
ndiyo ilikuwa salama yake,” kilisema chanzo hicho.
AMANI LAMSAKA KAJALA
Baada ya kuinyaka nyeti hiyo, Amani lilimsaka staa huyo na kumuuliza kama kuna ukweli wa madai hayo.
Awali, Kajala aligoma
katakata kukubali akisema hajui lolote lakini alipobanwa zaidi na
kuambiwa mlinzi wake ndiye aliyenyetisha habari hiyo, alikiri.
Kajala Masanja akiwa kwenye pozi.
MSIKIE MWENYEWE
“Any way, ni kweli ishu
imetokea usiku, lakini siyo saa nane, ilikuwa kama saa sita hivi. Mimi
nilikuwa nimelala, nikaona simu yangu ikiita. Nilipoangalia ni mlinzi,
nikapokea. Akaniambia kuna watu wamekuja, wamemwambia wametumwa
waniletee ujumbe kwamba nimepewa siku tano za kuishi na wametumwa na mtu
wangu wa karibu.
“Mimi sikuogopa,
nilitoka hadi kwa mlinzi, lakini nilikuta gari imeshaishia zake. Kifupi
ni kwamba katika watu si waoga ni mimi, unajua kwa nini? Naishi kwa
kumtegemea Mungu sana. “Kwa hiyo siogopi japokuwa habari hizo
zimenichanganya kupita kiasi, najiuliza ni mtu wangu gani wa karibu.
Basi si mtu wa karibu bali ni adui yangu. Hivi hapa najiandaa kwenda
Kituo cha Polisi Kijitonyama (Dar) kutoa taarifa kwa ajili ya
tahadhari,” alisema Kajala.
Akaongeza: “Unajua wiki
yote iliyopita nilikuwa kwenye harakati za kumalizia filamu yangu ya
Pishu. Kwa hiyo hata usiku wa jana nilichelewa kurudi, ile naingia tu
nadhani ndani ya nusu saa ndiyo watu hao walikuja, kama ningechelewa
zaidi huenda ningekutana nao getini.”
ANAMHISI NANI?
AMANI: “Kajala wewe unajijua, unadhani nani anaweza kukutumia ujumbe kama huu miongoni mwa watu wako wa karibu?”
KAJALA: “Mh! Siwezi
kumtaja hata kama kichwani yupo au wapo! Nitabaki kuwa na hisia zangu tu
kwa sababu sina ushahidi. Ila kama ningewaona kwa sura hao watu na
kuwatambua huenda ningeunganisha.”
Amani: “Huna mtu ambaye hivi karibuni mmetupiana maneno mabaya kwenye simu au laivu?”
Kajala: “Sina. Mimi nipo na watu wangu ni amani tu na ndiyo maana nachangayikiwa.”
Mpaka tunakwenda mitamboni, Kajala alisema ndiyo amewasili kwenye kituo hicho polisi akisubiri kusikilizwa.
0 comments:
Post a Comment