RAIS Jakaya Kikwete amewajibu walimu kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake amefanya kazi ya uboreshaji maslahi yao na kuahidi kumaliza madai yao yote kabla hajang’atuka madarakani Oktoba mwaka huu.
Kikwete alisema hayo alipokuwa akiwajibu walimu ambao waliandika
bango kwenye maandamano ya sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani na
kupita mbele yake na kusomeka kuwa ‘Shemeji Unatuachaje?’ ikiwa ni lugha
ya utani kwa kuwa mke wake Mama Salma ni mwalimu.
Maandamano hayo yalifanyika katika Jiji la Mwanza ambapo Kikwete
alikuwa mgeni rasmi. Katika majibu yake alisema ameboresha miundo ya
utumishi katika sekta mbili za walimu na afya.
Aliwaambia walimu mambo aliyoyafanya ni kuanzishwa kwa Muswada wa
Bodi ya taaluma ya walimu na Tume ya utumishi ya walimu lengo ni
kuwasaidia, kuwainua pamoja, kuwaendeleza na kufanya kila kitu katika
sekta hiyo.
Alisema maandalizi yake yameshakamilika bado kupelekwa bungeni.
Alisema Bodi ya taaluma ya walimu itawaendeleza walimu kitaaluma.
Katika hotuba hiyo kwa wafanyakazi iliyotumia zaidi ya saa moja,
Kikwete alisema anatumia nafasi hiyo kuwaaga ‘shemeji’ zake ambao ni
walimu, kwani imebakiza muda mfupi amalize muda wake.
Alisema muundo wa walimu umeanza Julai mwaka jana wa kulipa
malimbikizo yao lakini haukuenea katika maeneo yote kwa haraka, lakini
mwaka mpya wa fedha jambo hilo litawekwa vizuri.
Alisema malimbikizo ya walimu 30,668 hivi sasa ni Sh 53,155,440,406
na walimu 29,143 wamelipwa Sh bil 25.223 huku madai ya walimu 7,668
ambayo ni Sh bilioni 9.2 yatalipwa mwaka mpya wa fedha.
Lakini baadhi ya madai hayo ya walimu 30,807 ya Sh bilioni 17.3
yamekutwa na dosari mbalimbali na kutaka yarudishwe ili halmashauri
iyahakiki na yalipwe.
“Fanyeni hima dosari zikamilike walipwe. Baada ya kusema hayo nina
uhakika ninawaacha vizuri,” alisema Rais Kikwete.
Pia alielezea furaha yake ya uanzishwaji wa benki ya walimu, ambayo serikali inaiunga mkono na kutoa ushirikiano ili lengo la walimu litimie.
Pia alielezea furaha yake ya uanzishwaji wa benki ya walimu, ambayo serikali inaiunga mkono na kutoa ushirikiano ili lengo la walimu litimie.
Akizungumzia kada ya uuguzi, Rais Kikwete alisema serikali
ilibadilisha muundo mwaka 2010 ambao uliathiri baadhi ya wauguzi kwa
kuwa viwango vyao vya mishahara vilishuka, hilo ni kosa.
“Nimeagiza warejeshewe mishahara yao ya awali na malimbikizo
yalipwe,” alisema. Alisema katika kada hiyo mwaka 2010 watumishi 476,430
walipandishwa vyeo.
0 comments:
Post a Comment