Waziri
wa Ujenzi Dkt. John Magufuli ametangaza kutobomoa nyumba zilizopo kando kando
ya barabara ya Mwanga-Kikweni/Vuchama-hadi
Lomwe km 40.6 na kusema kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa
kutumia upana wake uliopo sasa hivi.
Dkt.
Magufuli alitoa kauli hiyo ya faraja kwa wakazi wa Kikweni Wilayani Mwanga
Mkoani Kilimanjaro kabla ya kuweka jiwe la msingi katika barabara ya
Mwanga-Kikweni/Vuchama-Usangi hadi Lomwe(km 40) itakayojengwa kwa kiwango cha
lami hivi karibuni.
Waziri
wa Ujenzi amechukua uamuzi huo kutokana na maeneo mengi ya milimani ambapo barabara
hiyo inapita kuwa na mashamba ya watu tofauti na sehemu nyingine. “Nikiwa
kama Waziri wa ujenzi katika maeneo haya ya milima sitatumia sheria ya mita 30
kila upande katika ujenzi wa barabara hii ili nyumba na mashamba ya wakazi wa
huku yasiathirike”.
Dkt.
Magufuli aliongeza kuwa ujenzi wa Barabara una sheria zake ndio maana ameamua
kutumia sheria ya barabara namba 13 ya
mwaka 2007 kifungu cha 13 na 20 kinachompa mamlaka kupunguza upana wa barabara.
Aidha,
Waziri Magufuli aliwatoa hofu wakazi wote waliowekewa alama ya X katika nyumba
zao na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwasababu nyumba hizo
hazitabomolewa.
Katika
hatua nyingine Dkt. Magufuli aliwataka watu wote waliojenga vibanda karibu na
barabara ya zamani waanze kuondoka mapema kabla ya ujenzi wa barabara hiyo
kuanza hivi karibuni.
“Nawaomba
wote mlioweka vibanda karibu na barabara mtoe kwa hiari yenu ili tutengeneze
barabara hii bila vikwazo na kwa haraka tofauti na awali ambapo tulikuwa
tunatangaza zabuni kwa kilomita chache” alisisitiza Waziri Magufuli.
Kwa
upande wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama amemshukuru Waziri Magufuli
kwa hatua yake hiyo na kusema kuwa kufunguka kwa barabara hiyo ni mkombozi
mkubwa kwa wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
“Wilaya
yetu hii inapakana na nchi jirani hivyo hata kiusalama ni vizuri barabara hii
ikajengwa kwa lami ili irahisishe mawasiliano kwa haraka zaidi katika Wilaya
yetu hii” alisema Mkuu wa Mkoa.
Naye
Mbunge wa Mwanga ambaye pia ni Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe
ameishukuru Serikali na kusema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutawaondolea
kero kubwa ya usafiri wananchi wa Usangi na mwanga na kuwasaidia kufanya
biashara kwa urahisi zaidi tofauti na awali.
“Kukamilika
kwa barabara hii kutasaidia kuinua uchumi mkubwa uliopo huku Usangi tofauti na
hali iliyopo sasa” Alisema Profesa Maghembe
0 comments:
Post a Comment