SIMBA SC imeendeleza ubabe wake kwa watani, Yanga SC baada ya kuwafunga bao 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Sifa zimuendee mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyefunga bao hilo pekee kipindi cha pili.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Martin Saanya wa Morogoro, aliyesaidiwa Soud Lila wa Dar es Salaam na Florent Zablon wa Dodoma, Yanga SC ilimaliza pungufu baada ya kiungo wake, Haruna Niyonzima kutolewa kwa kadi nyekundu, baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kuifungia Simba SC bao pekee leo Taifa
Niyonzima alionyeshwa kadi ya pili ya njano kwa ‘kujitakia’ baada ya kuupiga kutumbukiza nyavuni, wakati tayari refa Saanya amekwishapuliza filimbi ya kusimamisha mchezo.
Okwi alifunga bao hilo dakika ya 52 kwa shuti la umbali wa zaidi ya 22 baada ya pasi ya Said Ndemla akiwa pembeni kidogo mwa Uwanja kulia, akimtungua vizuri kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.
Mshambuliaji Danny Mrwanda aliikosesha Yanga SC bao la wazi dakika ya 28, baada ya kupewa pasi nzuri na Simon Msuva, lakini akazubaa na mpira ndani ya boksi hadi akapokonywa na Juuko Murushid.
Tukio hilo lilimkera kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm ambaye alimtoa mchezaji huyo dakika mbili baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.
Simba SC ilitawala kwa zaidi ya asilimia 10 dhidi ya Yanga SC mchezo huo, kutokana na kulundika viungo wengi uwanjani.
Ushindi huo, unaifanya SImba SC ifikishe pointi 26 baada ya kucheza mechi 17 na kupanda hadi nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 30 na Yanga SC 31.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment