WINGA Simon Msuva amefunga mabao matatu na kupika moja, Yanga SC ikiifumua mabao 4-0 Taifa ya Jang’ombe katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi, uliofanyika Uwanja wa Amaan usiku huu.
Msuva alizawadiwa mpira baada ya mechi na bahati nzuri zaidi kwake, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar (ZASWA) kikamteua kuwa mchezaji bora wa mechi.
Dakika 45 za kwanza zilimalizika Yanga SC wakiwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Msuva dakika ya 13, baada ya kuupitia mpira uliotemwa na kipa Kassim Abdallah kufuatia shuti la Mliberia, Kpah Sherman.
Kipindi cha pili nyota ya Msuva iliendelea kung’ara na akaifungia Yanga SC mabao mawili zaidi, huku pia akichaguliwa kuwa mchezaji bora mchezo huo.
Msuva alifunga bao la pili dakika ya 49 baada ya kuwachambua mabeki wa Taifa na kumvisha kanzu kipa wao, kufuatia pasi ya Salume Telela ‘Master’.
Msuva akakamilisha hat trick yake ya kwanza tangu ajiunge na Yanga SC mwaka 2012 na ya kwanza kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka huu, baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 63.
Msuva akampasia Mliberia Kpah Sherman kuifungia Yanga SC bao la nne dakika ya 90 na la kwanza tangu ajiunge na timu hiyo Desemba akitokea Cyprus.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inaongoza Kundi A, ikifuatiwa na Polisi yenye pointi tatu pia, lakini mabao mawili kufuatia ushindi wa 2-0 jana dhidi ya Shaba.
Michuano hiyo itaendelea kesho, kwa mechi mbili za Kundi C, kwanza JKU na Mtibwa Sugar na baadaye Mafunzo na Simba SC.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment