Wananchi wanahofu ya kutumia Condoms kwa madai zinachangia maambukizi ya VVU
Matumizi ya kondomu bado ni ya kiwango cha chini mkoani Njombe jambo linaloelezwa na shirika la TMarc Tanzania kwamba linachangia kuyafanya maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) yawe juu.
Moja ya sababu ni uzushi kwamba kondomu zimepandikizwa magonjwa hazifai kutumika.
Kwa mujibu wa Meneja Mahusiano na Mawasiliano wa TMarc Tanzania, Maurice Chirimi shirika hilo linafanya kazi ya uraghibishi wa mambo ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Afya na washirika mbalimbali wanochangia sekta hiyo.
Takwimu za Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) za mwaka 2012 zinaonesha mkoa wa Njombe unaongoza kitaifa kwa kuwa na asilimia 14.8 ya maambukizi.
Chirimi alisema mbali na kutoa elimu, shirika lao limekuwa likisambaza kondomu za kiume aina ya dume, za kike aina yared pepetapamoja na vidonge vya uzazi wa mpango.
“Tunafanya yote hii katika jitihada zetu za kuunga mkono juhudi za serikali na washirika wake katika kukabiliana na janga la UKIMWI,”alisema.
Katika usambazaji wa kondomu hizo, Chirima alisema baadhi ya watu wamekuwa wakipuuza matumizi yake kwa madai kwamba zimepandikizwa magonjwa.
Alisema kwa mkoa wa Njombe muitikio wa matumizi yake ni mdogo hali inayochochea maambukizi ya VVU tofauti na mikoa mingine nchini.
Alisema mwaka uliopita TMarc ilisambaza kondomu dume milioni moja ambazo hata hivyo hazikwisha kwasababu ya mwitikio huo mdogo.
“Shida tunayoiiona katika mazingira haya ni kwamba watu hawaziamini kondomu lakini wanaamini sana katika matumizi ya dawa za kufubasha VVU”alisema.
Alisema ni muhimu kwa mtu anayeshindwa kuwa mwaminifu kwa mpenzi wake aliyepima akatumia kondomu ili kujinusuru na maambukizi mapya.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi alisema wanampango wa miaka mitatu wa kukabiliana na janga hilo.
Kwa kupitia mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai mwaka jana, Dk Nchimbi alisema mbali ya kuhimiza matumizi ya kondomu, mpango huo unaendelea kuboresha huduma za tohara.
“Mkoa una vituo 13 vya kutolea huduma ya tohara na lengo letu ni kuona ifikapo mwaka 2017 jumla ya wanaume 163,495 mkoani hapa ambao hawajatahiriwa wawe wametahiriwa,”alisema.
0 comments:
Post a Comment