RAIS JAKAYA KIKWETE ASAMEHE WAFUNGWA 4969

RAIS Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,969 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Uhuru. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyotolewa Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema msamaha huo utawahusu wafungwa 4,969, ambapo 887 kati yao wataachiwa huru na wafungwa 4,082 watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki. Alisema wafungwa waliopata msamaha ni wale wanaougua magonjwa ya Ukimwi, TB na saratani, ambao wako kwenye ‘terminal stage,’ na wafungwa hao watathibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya. Wafungwa wengine ni wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi; na umri huo pia utathibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya na wafungwa wa kike walioingia gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya. Wengine waliopata msamaha ni wenye ulemavu wa mwili na akili na ulemavu huo utathibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa na Wilaya. Hata hivyo, msamaha huo hautahusisha wafungwa waliofanya makosa na kuhukumiwa kunyongwa, waliohukumiwa adhabu ya kifo na adhabu hiyo ikabadilishwa kifungo, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Wengine ni wale ambao wanatumikia kifungo kwa makosa ya kupokea na kutoa rushwa, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na wafungwa wanaotumia kifungo kwa maoksa ya kupatikana na silaha au risasi. Wafungwa wengine ambao hawatahusishwa na msamaha huo ni wanaotumikia kifungo kwa kosa kuwapa mimba wanafunzi wa shule ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari kwa kutumia silaha, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa jamii na wafungwa waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali ambao watatumikia kifungo hicho gerezani. Wengine ambao hawatafaidika na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madarakani yao, wafungwa waliowahi kupata msamaha wa Rais na ambao bado wapo gerezani kutumikia sehemu ya kifungo kilichobakia, wanaotumikia kifungo kwa kosa la kufanya biashara haramu ya binadamu na wanaotumikia vifungo kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: