CHAMA CHA CUF CHAMLAANI DAVID KAFULILA KWA KUSEMA DTK SLAA ANAFAA KUGOMBEA URAIS KUPITIA UKAWA
SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kukaririwa na vyombo vya habari nchini akisema Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye anayefaa kubeba jahazi la urais kwa vyama vinavyounda umoja uliobatizwa kwa jina la UKAWA, Chama cha Wananchi (CUF),kimelaani hatua hiyo.
CUF kupitia Naibu Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya alisema kilichofanywa na Kafulila ni sawa na fitina yenye lengo la kuugawa umoja wao unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCRMageuzi na NLD.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kambaya alisema Kafulila ni mkomavu wa kisiasa hivyo hakupaswa kutoa kauli hiyo. “CUF ni miongoni mwa vyama vinavyounda umoja huo, lakini hatujawahi kutoa kauli yoyote juu ya mgombea tunayedhani anafaa kugombea kupitia Ukawa kwa kuwa tunaamini muda haujafika,” alisema Kambaya.
Alisema kufanya hivyo kwa utashi wa mtu au kwa misimamo iliyojificha ni kuhatarisha umoja huo. “Kafulila ni Mkurugenzi wa Habari wa NCCR-Mageuzi, ni mtu mwenye ufahamu wa kutosha na anaweza kupima athari ya jambo analolitolea maoni, kwa hiyo kama kiongozi alipaswa kufahamu athari zitakazojitokeza kutokana na kauli yake.
“Tunalaani vikali kuenezwa kwa taarifa za uteuzi wa Dk Slaa kama mgombea wa umoja huu na tunapinga kuendelea kuenezwa kwa habari hizo kwani mashauriano ya ushirikiano wa masuala mbalimbali ikiwemo mgombea urais yatajadiliwa kwa kadri muda utavyohitaji kufanya hivyo,” alisema.
Alisema umoja huo uliundwa kupitia wajumbe wa vyama hivyo kwa lengo la kutetea maoni ya wananchi yaliyowasilishwa katika Rasimu ya Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.
Lakini baadaye umoja huo ulisaini makubaliano ya kushikamana zaidi katika masuala yenye maslahi kitaifa na pia katika uchaguzi, wakikubaliana kuachiana nafasi za uongozi kuanzia katika uchaguzi za Serikali za Mitaa na hata ya Rais, Wabunge na Madiwani.
“Tangu kutangazwa kwa makubaliano hayo, zimezushwa kauli mbalimbali zenye lengo la kupotosha dhamira ya dhati ya Ukawa, ikiwemo hili la kutajwa kwa mgombea wa urais. Aidha, alimtaka Kafulila na Makamu Mwenyekiti wa Bawacha, Hawa Mwaifunga kueleza kikao kilichokaa na kushiriki katika kutoa uamuzi ya uteuzi huo.
Alisema kama ni maoni yao binafsi walipaswa kuzungumza katika vikao vya vyama vinavyounda UKAWA na sio kuzungumza katika vyombo vya habari kama walivyofanya.
“CUF tunaamini kuwa huu ni mwendelezo wa sumu iliyoanzwa kupandikizwa na ripoti ya Utafiti wa Twaweza kuiaminisha jamii kuwa mgombea wa Ukawa ni Dk Slaa.CUF kinalaani vikali mwendelezo wa viongozi tena wanaounda Ukawa kuzungumza uongo wa wazi bila kujali ushiriki wa vyama vyao, kwani taarifa hizi zina lengo la kuwachanganya watanzania ambao wanahitaji mabadiliko,” alisema.
Alitaka vyama ambavyo wanachama wake wake waliotoa kauli hizo zilizoripotiwa na vyombo vya habari kupewa onyo na kuwahitaji kukanusha wenyewe kupitia vyombo vya habari. Aidha, alitaka Watanzania na wanachama wa CUF kupuuza taarifa hizo ambazo lengo ni kuwagawa Watanzania.
Wakati CUF wakilaani kauli ya Kafulila, Chadema kwa upande wao wamedai kuwa, muungano huo hauwezi kuyumba.
0 comments:
Post a Comment