19Dec2014WAFUNGWA MIAKA 40 JELA KWA MAUAJI YA MWINGEREZA

WANAUME wanne wataishi gerezani miaka 40 kila mmoja kwa kumuua mwanajiolojia Campbell Rodney Bridges wa Uingereza miaka mitano iliyopita. Jaji Maureen Odero wa Mahakama Kuu ya Mombasa, aliwapa adhabu hiyo Mohamed Dadi Kokane mwenye umri wa miaka 42, Alfred Njuruka Makoko (58), Samwel Mwachala Mwaghania (49) na James Chacha Mwita wa miaka 56 siku moja baada ya kuwapata na hatia ya kumuua Bridges. Jaji Odero alisema kwenye hukumu yake kwamba kosa walilotenda ni mbaya na walikatiza maisha ya marehemu aliyeacha mjane na mtoto mvulana. Ingawa upande wa mashtaka uliomba mahakama iwahukumu kunyongwa, jaji alisema kuna tashwishi kuhusu ikiwa adhabu hiyo ni ya lazima kwa sababu ya maamuzi mawili tofauti ya mahakama ya rufaa. Kabla ya kuhukumiwa, kiongozi wa mashtaka George Muriithi alisema walitenda kosa mbaya ambalo walipanga. “Hakuna kinachoweza kuzuia adhabu katika kesi hii, lazima wanyongwe”. Kulingana na ripoti ya waathiriwa wa mauaji iliyowasilishwa kortini, mjane wa marehemu Judith Bridges alisema uchungu wa kumpoteza mumewe uliathiri familia yake. Kwenye malilio yao, washtakiwa kupitia mawakili Steve Kithi na Fredrick Mwawasi, walisema wana familia na wakaomba wapewe adhabu nafuu. Aidha, waliomba korti itilie maanani muda ambao baadhi yao wamekuwa rumande na walipoachiliwa kwa dhamana kesi ikiendelea. Jaji Odero alisema kwamba walikuwa miongoni mwa kundi la watu waliomshambulia Bridges akielekea katika kambi yake. “Nimeridhika upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, pili, tatu, nne na kundi lao kwa kutekeleza nia ya kutenda uhalifu waliopanga,” akasema. Jaji Odero aliongeza kuwa washtakiwa walivunja sheria kwa kufunga barabara na kumzuia marehemu asifike kambi yake. “Washtakiwa wanawajibika kwa kupotea kwa maisha ya marehemu. Walimvamia na kundi lake licha ya kuwa hakuwa na silaha, hakuwawatisha,” akasema. Marehemu aliuawa mnamo Agosti 11, 2009 katika eneo la Kambaga Mwasui, Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta. Alikuwa mwanajiolojia aliyehusika na uchimbaji nchini tangu 1974 na alikuwa na kampuni mbili. Jaji alisema kwamba mashahidi walithibitisha kulikuwa na mzozo wa muda mrefu kati ya marehemu na kundi la 'wachimbaji eneo hilo’ kuhusu maeneo ya kuchimba madini ya Mwasui na Mkuki. Ushahidi wa kutosha “Mzozo huu ulipelekea kifo cha ghafla cha marehemu alasiri ya Agosti 11 2009,” akasema Jaji Odero na kuongeza kuwa waliomshambuliwa walifahamika na mashahidi. “Walikutana kila mara na wote walihusika na uchimbaji madini, kwa hakika mashahidi walimtambua kila mmoja kwa jina lake,” akasema. Jaji Odero alisema utetezi wa Kokane haukufaa, ilhali wa Makoko hakuweza kumshawishi. Alisema Mwachala alitambuliwa vyema na mashahidi wote kama mmoja wa waliomshambulia marehemu ilhali utetezi wa Mwita haukuwa na chochote cha kutiliwa maanani. Hata hivyo, aliwaachilia Daniel Mdachi Mnene, Osman Abdi Hussein na Crispus Mkunguzi Mngolia walioshtakiwa kwa kuhusika na mauaji ya Bridges. Jaji alisema kulikuwa na shaka ikiwa Mnene na Mkunguzi walihusika na shambulio dhidi ya marehemu, na akamwachilia huru. Alisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya Hussein. Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 26 katika kesi hiyo akiwemo mke wa marehemu na mwanawe.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: