KIYOGO WAIPONGEZA SERIKALI KWA ZAHANATI NA SHULE LAKINI WAIOMBA KUTATULIWA KERO YA MAJI.

Wananchi wa kijiji cha Kiyogo wilayani Ludewa Katika mkoa wa Njombe wameimwagia sifa Serikali ya wilaya hiyo kwa kuweza kuwatatulia kero ya muda mrefu ambayo ilikuwa ni ukosefu wa Zahanati na uchakavu wa mejengo ya shule ya msingi ambayo yalihatarisha maisha ya wanafunzi wa shule hiyo msimu wa mvua. Akizugumza mwenyekiti wa kijiji hicho Bw.Thomas Magnas alisema mpaka sasa tayari Zahanati yao inamganga mmoja ambaye anafanya kazi nzuri licha ya kuwa anazidiwa na mzigo mzito wa wagonjwa wengi lakini amekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi hao ambao awali walikuwa wakitibiwa katika mkoa wa Ruvuma. Alisema awali kulikuwa na shida kubwa kuanzia majengo ya shule ya msingi ambayo yalijengwa na shirika la consein na kusahauliwa na Serikali pia Zahanati haikuepo hali ambayo ilikuwa ni hatari kutokana na wananchi kuugua homa ya matumbo kutokana na uchafuzi mkubwa wa maji ya mto Ruhuhu ambao unachafuliwa na wachimba madini. Kijiji hicho ambacho tokea enzi za mababu hakijawahi pata maji safi na salama ya bomba wananchi wake wamekuwa wakiugua magonjwa ya matumbo kutokana na kutumia maji ya mto Ruhuhu ambayo ni machafu yanayotumika na wachimba madini kuoshea madini maeneo ya wialaya ya Mbinga na kijiji cha Amani wilayani Ludewa. Bw.Magnas alisema Kuwa ni miaka mingi sasa wananchi wa kijiji hicho wanakunywa maji machafu pia rangi ya maji hayo inatisha kutokana na chanzo cha mto huo kuwepo wachimba madini wanaoyachafua maji hayo hali hiyo imesababisha watu wengi wa kijiji hicho kupoteza maisha kutokana na homa za matumbo lakini Zahanati imekuwa mkombozi kwa tiba wanazozipata wananchi wa kijiji hicho. “Tunaisifu Serikali kwa haya waliyo yafanya maana tunayaona kwa macho yetu tofauti na awali tulikuwa tumesahaulika kama si watanzania ila bado suala la maji kwani maji tunayoyatumia hayafai kutumiwa na binadamu hali ambayo bado ni hatari kwa afya zetu”,alisema Bw.Magnas. Alisema kutokana na magonjwa ya mripuko yanayosababishwa na uchafuzi wa maji hayo inawalazimu kwenda vijiji vya jirani ambavyo ni Lihagule na Masasi wakati mwingine kuvuka mto Ruhuhu kwa mitumbwi na kwenda mkoa jirani wa Ruvuma kufuata huduma za Afya lakini kwa sasa huduma hiyo inapatikana kijijini hapo. Licha ya kupata huduma za Afya wananchi hao wameilalamikia Serikali kwa kutowatendea haki hasa katika suala zima la huduma ya maji safi kwani kila siku zinavyozidi kwenda ndivyo maji ya mto Ruhuhu yanavyozidi kuchafuliwa hali ambayo ni hatari licha ya kuwa Mbunge wa jimbo la Ludewa Mh.Deo Filikunjombe aliahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo. Akizungumza kwa uchungu Bi.Gaudesia Jonh alisema wamekuwa wakiyatumia maji hayo ambayo ni machafu hata ukiyaangalia kwa rangi hali ambayo ni hatari kwa afya hasa kwa watoto wadogo ambao huugua mara kwa mara. Bi.Gaudesia alisema hali hiyo imewafanya kuzarauliwa na vijiji vingine vya mkoa wa jirani kwa kutotatuliwa kero ya maji kwa muda mrefu tokea Tanzania ilipopata uhuru mpaka sasa wakiwa ni miongoni mwa wapiga kura wa nchi hii. Wananchi hao wlisema bado wanamaswali mengi vichwani mwao kama kweli Tanzania ilipata uhuru mwaka 1961 na kusherekea miaka 50 ya uhuru huo wakati kunawananchi ambao hawana huduma muhumu kama maji safi na salama. Naye kaimu muhandisi wa maji wilaya ya Ludewa,Muhandisi Marichela Maisha alisema Serikali bado iko katika mpango wa kutatua kero hiyo hivyo bajeti ikipitishwa kijiji hicho kitapata maji safi na salama kupitia bomba la kata ya Luilo. Muhandisi Maisha alisema tatizo la kijiji hicho ni kutokuwa na chanzo cha maji hivyo ni lazima utaalamu utumike kutafuta vyanzo katika vijiji vingine ili kulitatua tatizo hilo ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Kiyogo. Mwisho.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: