Juisi ya kabichi inaelezwa kuwa na faida nyingi tumboni, hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda vya tumbo (peptic ulcers). Kabichi ni mboga ya majani ambayo licha ya kulimwa kwa wingi na kupatikana masokoni karibu katika kipindi chote cha mwaka lakini wapishi wengi huwa hawaitumii sana katika milo. Hata hivyo kama unataka kuwa na ngozi inayong'aa na mfumo wa kinga ya mwili ulioimarika ili kupambana na maradhi ya aina yoyote pengine unapaswa kutoishia tu kutumia kabichi kwenye saladi na kachumbari na kuanza kula mara kwa mara mboga hiyo. Hii ni kwa sababu, kabichi ni mboga yenye nguvu hali iliyowapelekea waganga wa jadi kusema kuwa kabichi ina nishati inayotokana na mwezi kwa kuwa inakua katika mwanga wa mwezi. Hata kama hatutoamini ngano hizo lakini wataalamu wa sasa wa lishe wanasema kuwa, nishati inayopatikana kwenye kabichi inatokana na kiwango kikubwa cha sulphur na vitamin C na kwa ajili hiyo si vibaya ukizingatia chakula hicho katika mlo wako. Miongoni mwa faida za kabichi ni kusaidia katika kupunguza unene, na sifa hiyo inatokana na kalori ndogo ilizonazo na ufumwele wingi. Kikombe kimoja cha kabichi kina kalori 33 tu, hivyo ni chakula kinachofaa kwa ajili ya kupunguza unene. Kabichi pia huongeza akili, na hii ni kutokana na kuwa na vitamini K na mada ya anthocynins inayosaidia ubongo kufanya kazi vizuri na kuzingatia mambo. Virutubsho hivyo pia huzuia neva kuharibika, kuimarisha siha dhidi ya ugonjwa wa kusahau na Alzheimers. Kabichi yenye rangi nyekundu ina virutubisho hivyo kwa wingi. Ingawa mboga zote zina faida kwa ngozi, lakini kabichi inaongoza! Kutokana na kuwa na sulfur, kabichi husaidia kukausha ngozi yenye mafuta na chunusi. Ndani ya mwili pia sulfur ni muhimu kwa ajili ya kutengeneza keratin, protini ambayo ni muhimu kwa ajili ya afya ya nywele, kucha na ngozi Miongoni mwa faida nyingi zinazopatikana kwa kula kabichi (nyeupe na nyekundu), inayoongoza ni kuukinga mwili na ugonjwa hatari wa saratani. Inaelezwa kuwa, zaidi ya tafiti 475 zimefanyika kuhusu virutubisho vinavyopatikana kwenye kabichi na kuthibitisha kwamba, vina uwezo wa kuzuia ugonjwa wa saratani na wakati mwingine hata kutibu. Kabichi imeonekana kuwa na uwezo wa kipekee wa kupambana na ugonjwa huu kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha aina tatu muhimu za mada za 'Antioxidant', 'Anti-inflammatory' na 'Glucosinolates,' ambazo zina uwezo wa kudhibiti magonjwa kadhaa nyemelezi yanayosababisha saratani za aina mbalimbali mwilini. Kwa kuzingatia madhara na mateso yatokanayo na ugonjwa wa saratani, na kwa kuzingatia upatikanaji wa kabichi usiokuwa na gharama, huna sababu ya kupuuza ulaji wake. Laiti kama watu wote tungejua sawasawa faida za kabichi, bila shaka mboga hii ingekuwa ghali kuliko hata samaki. Faida za kabichi haziishii hapo, kwani mboga hiyo ina kiwango cha kutosha cha aina mbalimbali za vitamin hasa vitamini K, B1, B2, vitamin A na C. Aidha, kabichi ina kiasi kingi cha ufumwele au kamba lishe kwa maana ya fiber kwa kimombo, manganizi, potashiamu na fatty acids. Vyote hivyo ni kinga ya mwili dhidi ya magonjwa nyemelezi. Mbali na kuwa na uwezo wa kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani, juisi ya kabichi inaelezwa kuwa na faida nyingi tumboni, hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda vya tumbo (peptic ulcers). Ikitumika mara kwa mara huwa kama tiba kwao, na mfumo wa usagaji chakula tumboni, huwa imara.

ninakuhabarisha kutoka ludewa njombe tanzania
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: