ZAIDI ya wananchi 200 wa wilaya ya Kaliua

ZAIDI ya wananchi 200 wa wilaya ya Kaliua  mkoani Tabora wameandamana hadi kwa mbunge wa jimbo la Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, wakitaka mkuu wa wilaya Saveli Maketa na OCD Mnubi wa wilaya hiyo waondoke  kwa madai kuwa wananyanyasa na kuwabambikia kesi wananchi.
Maandamano hayo yalianza Ijumaa na kuendelea tena hadi Jumatatu asubuhi, wananchi hao wakishinikiza viongozi hao kuondoka.
Waandamanaji hao walishinikiza watu saba walioko rumande kwa kesi ya wizi wa pochi na simu ya askari mmoja wa kike, waachiwe huru kwani wamesingiziwa.
Chanzo cha maandamano hayo kimedaiwa kuwa ni baadhi ya wananchi saba waliowekwa ndani na Kamanda wa Polisi wa wilaya Kaliua ODC Mnubi, kutokana na wizi uliotokea katika baa yake na washirika wake wawili iitwayo ‘Polisi Mesi’.

Kesi hiyo yenye RB 1333/1247/2013 ya wizi  wa pochi na simu yenye thamani ya sh 150,000, fedha taslimu sh 750,000 na aliyeibiwa ni askari polisi WP Noela.
Tukio la wananchi hao saba lilitokea siku ya  Jumatano ya Oktoba 23, 2013, majira ya saa mbili za usiku, katika baa ya hiyo wilayani Kaliua.
Wananchi hao walisema wamechoshwa na uonevu wa OCD na mkuu wa wilaya na wameamua kuandamana baada ya kuchoka na ghiliba za viongozi hao.
Hata hivyo baada ya kufika kwa Kapuya aliwasikiliza na aliitikia maombi yao na mbunge huyo kuamua kwenda kituo cha polisi kujua hatma ya wananchi saba walioko rumande.
Mkuu wa polisi wilaya ya Kaliua, OCD Mnubi, alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini alikataa kuongelea zaidi kwa kudai kuwa msemaji ni Kamanda wa Polisi wa mkoa.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kaliua Saveli Maketa alipotakiwa kutoa ufafanuzi kwa nini wananchi wameandamana kumkataa, alisema hayuko katika kituo chake cha kazi kwani yuko jijini Mbeya akimuuguza baba yake mzazi.
“Niko jijini Mbeya namuuguza baba yangu mzazi……sina taarifa wanalalamikia nini na nimewanyanyasa kwa lipi sijui chochote ndugu ila nakushukuru kwa taarifa,” alisema.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Peter Ouma, alikiri kuwepo kwa tukio hilo.
Alisema tayari suala hilo limeshashughulikiwa na watuhumiwa watapatiwa dhamana.
Kwa upande wake askari aliyeibiwa pochi ya mkononi na simu WP Noela alipotakiwa kuongelea mwenendo wa kesi yake alikataa.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: