JULIO: YANGA KAMA TYSON, WANA NGUVU DAKIKA 25 TU


Ama kweli sare ya mabao 3-3 ya mchezo wa Ligi Kuu ya Bara ulizokutanisha Simba na Yanga imezua mambo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ amesema kikosi cha Yanga kinamudu kucheza vizuri na kwa kasi ndani ya dakika 25, na kwenda mbele inaweza kufungwa idadi yoyote ya mabao.

Katika mchezo huo uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilitangulia kufunga mabao 3-0 ndani ya dakika 45 za kwanza, lakini Simba ilirudi kipindi cha pili na kuweza kusawazisha mabao hayo na kumaliza mechi kwa sare ya mabao 3-3.

Mara baada ya mchezo huo, Julio amesema Yanga ilicheza vizuri ndani ya dakika 25 tu za kipindi cha kwanza na baada ya hapo kwenda hakuna inachofanya inaweza kufungwa hata na timu nyanya. Julienda alienda mbali kwa kutolea mfano wa bondia wa zamani wa uzito wa juu raia wa Marekani, Mike Tyson ambaye alikuwa anapigana kwa nguvu ndani ya raundi za kwanza lakini akifika raundi ya tano, anakuwa hana ujanja na kuweza kupigwa na bondia yeyote.

Kumbukumbu nzuri ya Tyson kumaliza pambano lake mapema ni Septemba 7, 1996 alipopambana na Bruce Seldon katika pambano la uzito wa juu (WBA Heavyweight) kwenye Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena huko Paradise, Nevada, Marekani ambapo Tyson alishinda KO katika dakika 1:12 raundi ya kwanza.

Juni 28, 1997, Tyson alipigwa na Evander Holyfield katika pambano la uzito wa juu la WBA katika raundi ya 11 kwa TKO, na mambo yalianza kumwendea vibaya katika raundi ya sita na hakuweza kufanya vizuri katika raundi zilizofuata. Tyson alikuwa na nguvu hadi raundi ya tano na kwenda mbele alikuwa hana pumzi ya kupambana ulingoni.

“Yanga kama Tyson tu, ukiweza kutoka nje ya dakika 25 za mwanzo unaweza kuwafunga kwani kasi yao inakuwa imepungua. Siku moja nilikosa pambano la Tyson kutokana na yeye kumpiga bondia ndani ya raundi ya kwanza, sasa kama ukiweza kuimudu Yanga ndani ya dakika hizo basi unaweza kuifunga unavyotaka.

“Kama Mtibwa na timu nyingine zilizofungwa na Yanga zingeweza kukaza vizuri basi zisingefungwa na Yanga kwani soka lao ni la muda mfupi na baada ya hapo timu nzima inakuwa imechoka na kushindwa kufanya mipango yoyote ile,” anasema Julio maarufu kama Alberto Pereira.

Julio kama ilivyo kwa Kibadeni, alikiri kwa kikosi chake kucheza chini ndani ya kipindi cha kwanza na kuiruhusu Yanga kupata mabao 3-0, lakini baada ya kutoa maelekezo muhimu na kufanya mabadiliko ndipo mambo yalipobadilika.

“Mwanaume lazima upambane kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho ili kuhakikisha kwamba unafanya vizuri katika vita yako, na hicho ndicho tulichofanya na ndiyo sababu ya kufanya vizuri japokuwa tumetoka sare,” anasema Julio ambaye amewahi kuichezea Simba na Taifa Stars siku za nyuma.

Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Mrisho Ngassa an Hamisi Kiiza aliyefunga mawili huku mabao ya Simba yakifungwa na Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: