BEKI
wa kati wa Simba, Gilbert Kaze amefurahi kufunga bao lake la kwanza
katika Ligi Kuu ya Bara pia kuisawazishia timu yake bao la tatu dhidi ya
Yanga jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kaze
raia wa Burundi aliyezaliwa Januari 25, 1992 ambaye amejiunga na Simba
msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi, aliifungia Simba bao la tatu na
kuisawazishia klabu yake dakika ya 83 kufanya matokeo kuwa mabao 3-3.
Katika
mahojiano yake muda mfupi baada ya mchezo huo, Kaze beki mrefu
mwembamba anayezungumza kwa taratibu, aliuambia mtandao huu kwamba,
anajisikia fahari kufunga bao hilo na kuifanya timu yake kupata matokeo
ya sare wakitoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa mabao 3-0.
“Sikujua
kama nitafunga bao, lakini nikauona mpira upo peke yake nami nikajituma
na kuuwahi mpira wa faulo uliopigwa na Chollo, nashukuru kufunga bao
langu la kwanza katika ligi hii pia kuifunga Yanga timu ambayo ni
pinzani na hii ninayoichezea.
“Nashukuru
jinsi mashabiki wa Simba walivyotuvumilia wakati tulipokuwa nyuma kwa
bao 3-0 na hata makocha walifanya kazi nzuri ya kutuweka sawa
kisaikolojia wakati wa mapumziko na tukaweza kufanya vizuri na
kusawazisha mabao yote,” anasema Kaze.
Kuhusu ligi kuu ya bara...
Kaze
anasema Ligi Kuu ya Bara ni ngumu kuliko ligi ya Burundi aliyoichezea
msimu uliopita na kukiri kila timu anayokutana nayo ni nzuri na
inayoonekana imejiandaa kwa kucheza ligi.
Anasema
kila mechi alizocheza katika ligi kuu ya bara anakutana na
washambuliaji na viungo hatari na wenye nguvu nyingi hivyo analazimika
kutumia nguvu nyingi na yeye wakati mwingine ili aweze kuendana na
wapinzani wake.
“Unajua
ligi hii ya Tanzania ni ngumu kulinganisha na ile ya Burundi
niliyocheza msimu uliopita, hapa kila timu inaonekana imejiandaa
kupambana na sioni kama wanakamia bali ndivyo wanavyocheza na ndiyo
maana hata wakati mwingine tunashinda kwa taabu sana,” anasema Kaze.
Vipi anaonekana hana nguvu uwanjani..
Katika
mechi nyingi alizoichezea Simba, Kaze amekuwa akionekana kama mchezaji
asiye na nguvu na kushawishi washambuliaji wa timu pinzani ‘kumtamani’
na kumfuata kutaka kupambana naye tofauti na beki mwenzake Joseph Owino.
Lakini
mwenyewe anakiri kuwepo kwa hali hiyo lakini anawataka wadau wa soka
kutofautisha nguvu na kucheza polepole, kwani yeye hachezi kwa kasi sana
kulingana na aina ya wachezaji au timu pinzani anayocheza nayo.
“Naweza
kuonekana sina nguvu, lakini si kweli. Unajua hata Ulaya si kweli
kwamba wachezaji wote wana nguvu sawa. Sasa kama naonekana nina nguvu
kidogo hicho ni kitu cha kawaida kwani pamoja na hali hiyo mbona nacheza
na kocha anashukuru kwa kazi yangu.
“Mimi
wakati fulani huwa nacheza taratibu kutegemea na mchezo ulivyo, huwezi
kucheza kwa papara mbele ya wapinzani wenye akili ya mpira na nguvu pia.
Kuna wakati beki unatakiwa kucheza kwa akili zaidi kuliko nguvu,”
anasema Kaze.
‘Partinership’ yake na Owino
Katika
kikosi cha Yanga, nafasi ya beki wa kati wapo Nadir Haroub ‘Cannavaro’
na Kelvin Yondani, hawa wamecheza muda mrefu na wanamudu kucheza
sambamba ndani ya kikosi cha Yanga na wakati mwingine katika timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Hata
Arsenal kwa sasa wapo Per Mertesacker na Laurent Koscielny, ukienda
Manchester United utakutana na Nemanja Vidic na Rio Ferdinand, ndani ya
kikosi cha Simba kwa sasa wapo Kaze na Joseph Owino.
Tofauti
na safu zote hizo, Kaze na Owino wanaonekana hawaelewani na pia
wanacheza bila kuwasiliana na ndiyo maana wanaruhusu mabao mengi rahisi,
lakini Kaze anasema ni hali ya kimchezo tu inayofanya wafungwe na siyo
kutoelewana kwao.
“Ukuta
wetu ni mpya, nasi hatujakaa kwa muda mrefu na ndiyo maana hadi leo
tunacheza. Tatizo langu lililokuwepo ni kutokaa pamoja kwa muda mrefu
lakini nadhani si tatizo sana kwetu,” anasema Kaze.
0 comments:
Post a Comment